Mtoto wa Jicho
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Mtoto wa jicho ni nini?
Mtoto wa jicho ni hali ya lenzi ya jicho kuwa na ukungu, ambayo husababisha kupungua kwa uwezo wa kuona na, kwa baadhi ya visa, upofu. Hali hii hutokea pale ambapo protini zinapojikusanya kwenye jicho moja au yote mawili, na kuzuia retina kufanya kazi vizuri. Ugonjwa wa mtoto wa jicho kwa kawaida huathiri wazee, lakini unaweza kuwepo tangu utotoni, kusababishwa na mionzi au majeraha, pamoja na matatizo yanayotokana na upasuaji. 2
Mtoto wa jicho ni miongoni mwa sababu kuu za upofu duniani na ni mojawapo ya sababu za kawaida za kupoteza uwezo wa kuona kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40. 3 Mtoto wa jicho unaweza kutibiwa kwa njia ya upasuaji, na hatua zinaweza kuchukuliwa ili kusaidia kuzuia kuanza kwa tatizo hili.
Aina za Mtoto wa Jicho
Kuna aina kadhaa za mtoto wa jicho, ambazo huainishwa kulingana na jinsi na sehemu zinazojitokeza kwenye jicho: 4
- Mtoto wa jicho katika kiini: Hii hutokea katikati ya lenzi ya jicho (kiini) na mara nyingi husababisha jicho kuwa na rangi ya kahawia au njano. Kwa kawaida, huambatana na uzee.
- Mtoto wa jicho wa kapsuli ya nyuma (posterior capsule): Aina hii huathiri sehemu ya nyuma ya jicho na kawaida hujitokeza kwa haraka sana.
- Mtoto wa jicho katika korteksi (Cortical): Hii hutokea kwenye korteksi ya lenzi linalozunguka kiini cha jicho. Huwa na umbo la mviringo lenye rangi nyeupe.
- Mtoto wa jicho wa kuzaliwa nayo (Congenital cataracts): Hii ni aina nadra ambayo hujitokeza utotoni au mtu huzaliwa nayo.
- Mtoto wa jicho wa mionzi: Hii husababishwa na athari za mionzi, mara nyingi kama matokeo ya matibabu ya saratani.
- Mtoto wa jicho kutokana na majeraha: Aina hii husababishwa na madhara fulani katika macho na inaweza kujitokeza muda mrefu baada ya jeraha la awali.
- Mtoto wa jicho anayesababishwa na matokeo ya matumizi ya dawa au magonjwa (secondary cataracts): Hii ni pamoja na dawa za steroidi kama prednisone, na magonjwa kama kisukari na glakoma.
Dalili za Mtoto wa Jicho
Mtoto wa jicho kwa kawaida hutokea polepole, hivyo dalili zake zinaweza kuwa ngumu kugundua au kudhaniwa ni dalili za kawaida za uzee. Dalili hizi ni pamoja na: 2
- Kutokuona vizuri, kuona ukungu au vitu vilivyofifia
- Kuathirika na mwanga, hasa usiku
- Vitu kuonekana na kivuli cha njano au rangi iliyofifia
- Kuona maumbo ya duara karibu na mwangaza (halos)
- Kuhitaji kuvaa miwani yenye nguvu zaidi ili kuweza kuona vizuri
Wakati mwingine, mtoto wa jicho anapojitokeza, anaweza kusababisha kuboreka kwa uwezo wa kuona mbali. Hali hii hufahamika kama kuona mara ya pili (second sight), na ni hali ya muda ambayo huisha kadiri mtoto wa jicho anavyoendelea. 5
Nini Husababisha Mtoto wa Jicho?
Lenzi ya jicho huchuja mwanga kuelekea kwenye retina, na kusaidia mtu kuona vizuri. Kwa kiasi kikubwa, lenzi hii imetengenezwa na maji na protini. Mtoto wa jicho husababishwa wakati protini hizi zinaanza kukusanyika ndani ya lenzi, na kusababisha hali ya mtu kuona kuanza kufifia, na kuwa na ukungu ambao unaweza kuzidi kuwa mbaya zaidi kulingana na muda. Ugandaji huu kwa kawaida ni matokeo ya uzee, ingawa haijulikani kwa nini baadhi ya watu wanapata tatizo hili na wengine hawapati.
Hata hivyo, kuna baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuongeza nafasi ya mtu kuugua mtoto wa jicho, yakiwemo: 6
- Kuathiriwa na mionzi ya ultraviolet, kutoka kwenye mwanga wa jua au tiba ya mionzi
- Kisukari
- Magonjwa ya macho kama vile uveitis na glakoma
- Jeraha la jicho au upasuaji wa macho
- Matumizi ya kortikosteroidi
- Historia ya mtoto wa jicho katika familia
Mambo mengine yanayohusishwa na mtoto wa jicho ni pamoja na:
- Kuvuta sigara
- Kunywa pombe
- Matumizi ya madawa ya kulevya
- Upungufu wa vitamini, ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitamini D, vitamini K, na vitamini B12.
Utajuaje Kama Una Mtoto wa Jicho?
Mtoto wa jicho hutambuliwa kupitia uchunguzi kamili wa macho unaofanywa na mtaalamu au daktari wa macho. Wale wanaopata matatizo ya kuona wanapaswa kwenda kwa mtaalamu wa macho haraka iwezekanavyo. Aidha, watu walio na umri wa zaidi ya miaka 40 wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa macho angalau mara moja kila baada ya miaka miwili. 2
Matibabu ya Mtoto wa Jicho
Ikiwa dalili za mtoto wa jicho si kali, kubadilisha miwani au vibandiko vya macho (contact lenses) kunaweza kusaidia kuboresha uwezo wako wa kuona. Hata hivyo, kwa kawaida madhara ya mtoto wa jicho huongezeka kulingana na muda. Iwapo hali hii itatokea, kuna uwezekano mkubwa kwamba upasuaji utahitajika. 7
Upasuaji wa mtoto wa jicho ni utaratibu wa kawaida na kwa kawaida hufanywa kwa kuchoma sindano ya ganzi katika sehemu husika. Watu wengi wanaofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho huweza kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kuona, na watu 9 kati ya 10 huweza kuona kati ya 20/20 na 20/40 baada ya upasuaji. Hata hivyo, madaktari wa upasuaji wengi hulenga kurekebisha uwezo wa kuona mbali, kwa maana kwamba miwani bado inaweza kuhitajika ili kuona vitu vilivyo karibu.
Ni vyema kufahamu: 20/20 na 20/40 ni vipimo vya ukali wa kuona.
Hii kwa kawaida hupimwa kwa kutumia mfumo wa kuona wa Snellen:
- Namba ya juu katika jumla ya sehemu inahusu umbali wa kutazama kati ya mgonjwa na chati ya macho.
- Namba ya chini katika jumla ya sehemu inahusu umbali ambao mtu anayeona vizuri angeweza kuona takwimu kwenye chati ya macho vizuri.
Kwa hivyo, mtu mwenye uwezo wa kuona wa 20/40 anaweza kuona takwimu kwenye chati ya macho vizuri akiwa umbali wa futi 20, wakati mtu anayeona vizuri zaidi anaweza kuona takwimu hizo vizuri akiwa umbali wa futi 40 kutoka kwenye chati ya macho.
Katika nchi nyingi, uwezo wa kuona hupimwa kwa umbali wa mita 6, na hivyo uwezo wa kuona wa mtu unaweza kuonyeshwa kama sehemu ya 6.
Vihatarishi vya Upasuaji wa Mtoto wa Jicho
Hatari ya kupata madhara wakati au baada ya upasuaji wa mtoto wa jicho ni ndogo.. Changamoto inayojitokeza mara nyingi ni ukungu kwenye kapsuli ya nyuma, unaojulikana kama Posterior Capsule Opacification (PCO). Hali hii husababishwa na ukuaji wa utando juu ya lenzi bandia iliyowekwa, na kusababisha kupungua tena kwa uwezo wa kuona. Kwa bahati nzuri, PCO inaweza kutibiwa kwa upasuaji wa miale ya leza, kurejesha uwezo wa kuona kwa ufanisi. 8 7
Kuna vihatarishi vingine ambavyo ni nadra sana. Vihatarishi wakati wa upasuaji ni pamoja na:
- Hitilafu kwenye lenzi
- Kushindwa kuondoa mtoto wa jicho
- Kutokwa na damu kwenye jicho
- Uharibifu wa bahati mbaya katika maeneo mengine ya jicho
Vihatarishi baada ya upasuaji ni pamoja na:
- Inflamesheni katika jicho
- Kuvimba kwa retina
- Kuvimba kwa cornea
- Kutengana kwa retina
- Maambukizi
Iwapo madhara yatatokea baada ya upasuaji, unapaswa kuwasiliana na daktari haraka iwezekanavyo. Katika visa vingi, madhara yanaweza kusahihishwa kwa matibabu au upasuaji zaidi.
Jinsi ya Kujikinga na Mtoto wa Jicho
Ingawa hakuna njia ya uhakika ya kujikinga na mtoto wa jicho, kuna hatua kadhaa za kujikinga ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kupunguza hatari. Hatua hizi ni pamoja na: 9
- Kufanyiwa uchunguzi wa macho mara kwa mara
- Kula mlo wenye manufaa kiafya na wenye vitamini nyingi
- Kuacha au kupunguza uvutaji wa sigara
- Kupunguza au kuacha kunywa pombe
- Kuepuka matumizi ya muda mrefu ya dawa za kortikosteroidi
Hitimisho
Mtoto wa jicho, ingawa ni hali ya kawaida, anaweza kuathiri sana uwezo wa kuona na ubora wa maisha ya mtu ikiwa hatatibiwa. Kuelewa dalili, visababishi, na matibabu ni muhimu kwa utambuzi wa mapema na udhibiti mzuri wa ugonjwa huu. Uchunguzi wa mara kwa mara wa macho, kudumisha mtindo wa maisha wenye manufaa kiafya, na kujua hatari zinazoweza kutokea kutokana na upasuaji wa mtoto wa jicho kunaweza kusaidia katika kuzuia au kuchelewesha kuanza kwa mtoto wa jicho.
Maswali Yanayoulizwa Mara Kwa Mara (FAQs)
S: Dawa ya mtoto wa jicho ni ipi?
J: Mtoto wa jicho kwa kawaida hutibiwa kupitia upasuaji, ambapo lenzi iliyoharibika huondolewa na kuwekwa lenzi bandia. Hakuna dawa maalum ya kuondoa mtoto wa jicho, lakini matumizi ya miwani yenye lenzi maalum yanaweza kusaidia kuboresha uwezo wa kuona kwa muda mfupi kabla ya upasuaji.
S: Dalili za mtoto wa jicho ni zipi?
J: Dalili za mtoto wa jicho ni pamoja na kuona ukungu, kushindwa kuhimili mwanga mkali, hasa usiku, rangi kuonekana kama zimefifia au za njano, na kuona miale ya mwanga inayozunguka taa. Baadhi ya watu wanaweza pia kuhisi kuboreka ghafla kwa uwezo wao wa kuona mbali, hali inayojulikana kama kuona mara ya pili (second sight), na huisha yenyewe kadiri mtoto wa jicho anavyoendelea.
S: Mtoto wa jicho husababishwa na nini?
J: Mtoto wa jicho husababishwa na mchakato wa kawaida wa uzee ambapo protini ndani ya lenzi ya jicho hukusanyika na kuunda ukungu. Sababu nyingine ni pamoja na kuathiriwa na mionzi ya jua au matibabu ya mionzi, kisukari, jeraha la jicho au upasuaji wa jicho, matumizi ya muda mrefu ya dawa za kortikosteroidi, na historia ya ugonjwa huu katika familia. Pia, uvutaji sigara na unywaji pombe kupita kiasi vinaweza kuchangia kuongezeka kwa hatari ya kupata mtoto wa jicho.