1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ugonjwa wa kisukari

Ugonjwa wa kisukari

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Kisukari ni nini?

Katika ugonjwa wa kisukari aina ya 2, seli za mwili haziathiriki na insulini jinsi ipasavyo. Insulini ni homoni inayozalishwa na kongosho ili kuitayarisha sukari iliyomo kwenye damu kutumika kama chanzo cha nguvu mwilini.

Watu wenye ugonjwa wa kisukari aina ya 2 huwa wana tatizo la sukari iliyo kwenye damu kushindwa kuingia kwenye seli za mwili. Matokeo yake ni viwango vya sukari kwenye damu kuwa juu.

Dalili huweza kujumuisha kukojoa mara kwa mara na kuwa na mkojo mwingi. Watu walioathirika huweza kupungua uzito na kuhisi uchovu na kiu kuliko kawaida.

Ugonjwa wa kisukari aina ya 2 mara nyingi huweza kudhibitiwa kwa lishe nzuri, mazoezi ya mara kwa mara, na dawa za kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu.

Dalili za kisukari

Dalili za awali za ugonjwa wa kisukari ni pamoja na:

  • Kuhisi kiu
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Kuwa na kiasi kikubwa cha mkojo
  • Kuhisi uchovu sana na muda wote
  • Kupungua uzito

Hata hivyo, watu wengi hawana dalili yoyote katika hatua za awali za ugonjwa wa kisukari. Utambuzi huweza kufanyika wakati wa uchunguzi wa kawaida wa kiafya.

Dalili za kisukari ambazo hujitokeza baadaye huweza kujumuisha:

  • Maambukizi ya mara kwa mara (kwa mfano maambukizi ya ngozi au kibofu cha mkojo)
  • Mikato au vidonda kuchukua muda mrefu kupona
  • Uwezo hafifu wa kuona (kuona ukungu)
  • Maumivu au ganzi kwenye miguu au mikono

Vihatarishi vya ugonjwa wa kisukari

Kongosho ni kiungo kinachopatikana nyuma ya tumbo. Kimeungana na utumbo na huzalisha dutu muhimu za umeng’enyaji wa chakula. Pia, kongosho hutengeneza homoni za insulini na glucagoni, ambazo hudhibiti viwango vya glukosi, aina ya sukari mwilini.

Aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari hutokea pale ambapo seli za mwili haziathiriki na insulini jinsi ipasavyo. Matokeo yake ni kwamba seli zinashindwa kuchukua sukari hii kutoka kwenye damu. Aina ya 2 ya kisukari hutambuliwa mara nyingi kwa watu wazima.

Hata hivyo, idadi ya vijana wanaotambuliwa kuwa na ugonjwa huu inaongezeka.

Vihatarishi vya ugonjwa wa kisukari aina ya 2 ni pamoja na:

  • Kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi
  • Kula lishe yenye kalori nyingi
  • Kutofafanya mazoezi mara kwa mara au kutojishughulisha kimwili
  • Kuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari aina ya 2 katika familia

Pia, wanawake wanaopata kisukari wakati wa ujauzito wapo kwenye hatari zaidi ya kupata aina ya 2 ya kisukari.

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na dalili na kupima kiwango cha sukari kwenye damu. Ikiwa bado haitambuliki kama mtu ana ugonjwa wa kisukari, utambuzi unaweza kuthibitishwa kwa kipimo cha ustahimilivu wa glukosi (glucose tolerance test). Katika kipimo hiki, mtu humeza kiasi fulani cha glukosi. Halafu kiwango cha sukari kwenye damu hupimwa baada ya muda ili kuona ikiwa mwili unatumia glukosi namna ipasavyo.

Tiba ya kisukari

Matibabu ya kisukari aina ya 2 hulenga kuwa na kiwango cha sukari katika damu ambacho ni salama kiafya. Hii hulenga kuboresha athari ya insulini kwenye mwili na kuzuia madhara ya ugonjwa wa kisukari.

Hatua za kwanza za matibabu hujumuisha kuongeza kufanya mazoezi na kuboresha lishe. Kuwa na uzito mzuri kiafya ni muhimu. Hata hivyo, baada ya muda, dawa huweza kuhitajika kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu.

Kadiri ugonjwa unavyoendelea, mtu aliyeathirika anaweza kuhitaji kufundishwa jinsi ya kufanya baadhi ya mambo kama vile kuchunguza wenyewe viwango vyao vya sukari. Wataalamu wa afya huweza kutoa maelezo na kusaidia katika hatua zote za matibabu.

Ufuatiliaji wa mara kwa mara ni muhimu. Ufuatiliaji unaweza kusaidia kutambua na kutibu madhara yanayosababishwa na kisukari. Madhara haya yanaweza kuwa ni pamoja na uharibifu wa neva na macho.

Kinga

Baadhi ya visa vya aina ya 2 ya kisukari huweza kuzuiliwa. Kudumisha uzito mzuri kiafya, kula lishe nzuri kiafya na kufanya mazoezi mara kwa mara ni muhimu katika kujikinga na ugonjwa huu.

Ubashiri

Aina ya 2 ya kisukari haiwezi kuponywa. Hata hivyo, kwa usaidizi na elimu, watu wengi hujifunza kumudu viwango vyao vya sukari kwenye damu. Watu wasiodhibiti viwango vyao vya sukari huweza kupata madhara zaidi. Madhara haya hujumuisha kupoteza uwezo wa kuona, uharibifu wa neva kwenye mikono na miguu pamoja na ugonjwa wa moyo.


Washirikishe wengine kwenye makala hii: