1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Kipindupindu

Kipindupindu

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Muhtasari

  • Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na kumeza bakteria aitwaye Vibrio cholerae.
  • Dalili za kipindupindu zinazofahamika zaidi ni kuharisha sana na kutapika, ambazo zinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini.
  • Matibabu ya kipindupindu yanahusisha zaidi kurejesha maji mwilini na pengine matumizi ya antibiotiki.
  • Kipindupindu kwa kawaida hutokea katika maeneo yenye ukosefu wa usafi, upatikanaji mdogo wa maji safi ya kunywa, na miundombinu duni ya usafi.

Kipindupindu ni ugonjwa ambao unaweza kusababisha kuharisha sana na hata kusababisha kifo. Kujua dalili za kipindupindu na matibabu yake ni muhimu, hasa ikiwa unaishi au unasafiri katika eneo ambalo kipindupindu hutokea. Katika makala hii, timu yetu ya maarifa ya kitiba inakupa maelezo ya kina kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili uweze kuchukua hatua zinazofaa katika kutunza afya yako.

Kipindupindu ni nini?

Kipindupindu ni maambukizi yanayosababishwa na bakteria aitwaye Vibrio cholerae. Kipindupindu kilianzia karne ya 19 nchini India, kisha kikaanza kusambaa duniani kote. Kulikuwa na milipuko kadhaa ya kipindupindu katika historia, ambayo ilisababisha vifo vya mamilioni ya watu. Kwa sasa, kipindupindu bado kipo na kinachukuliwa kuwa ni ugonjwa wa kawaida katika nchi nyingi, ikimaanisha kwamba ni ugonjwa unaotokea mara kwa mara ndani ya nchi husika. Kila mwaka, kuna takriban visa milioni 1.3 hadi 4 vya kipindupindu duniani kote. 1

Dalili za kipindupindu ni zipi na hatari zinazoweza kutokea?

Dalili za kipindupindu kwa kawaida hujitokeza ndani ya masaa 12 hadi siku 5 baada ya kula chakula chenye bakteria anayesababisha ugonjwa huu. Watu wengi wanaougua kipindupindu hupatwa tu na dalili za kuhara kwa kiwango kidogo hadi cha kati. Katika baadhi ya visa, kipindupindu kinaweza kusababisha kuharisha sana, hali ambayo inaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini. Ikiwa hali hiyo haitatibiwa, inaweza hata kusababisha kifo. 1

Mbali na kuharisha sana, kipindupindu pia kinaweza kusababisha: 2

  • Kutapika
  • Kukakamaa kwa misuli ya miguu
  • Kukosa utulivu au kukereka kirahisi
  • Mapigo ya moyo ya haraka
  • Shinikizo la chini la damu
  • Upungufu wa maji mwilini

Kipindupindu husababishwa na nini?

Kipindupindu kinasababishwa na bakteria. Bakteria hawa wanaweza kuingia mwilini baada ya kula au kunywa chakula au maji yaliyoathiriwa na bakteria husika. Hali hii huathiri zaidi watu wanaopata shida kupata maji safi na miundombinu ya msingi ya usafi.

Kipindupindu kinaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kutokana na ukosefu wa miundombinu ya msingi ya usafi. Ikiwa mtu ameambukizwa na bakteria, basi bakteria hao watakuwepo kwenye kinyesi chake kwa muda wa hadi siku 10. Katika maeneo kama vile maeneo ya makazi duni (slums) na kambi za watu waliokimbia makazi yao au wakimbizi, hatari ya kupata maambukizi ya kipindupindu huongezeka sana. 1

Kipindupindu hudumu kwa muda gani?

Dalili za kipindupindu kwa kawaida hudumu kwa takriban wiki 1 kwa wale wenye dalili zisizo kali. Watu wenye dalili kali pia hupona ndani ya wiki 1, mradi tu wanapata matibabu wanayohitaji.

Kipindupindu huweza kutambuliwaje?

Ikiwa mtoa huduma wako wa afya atashuku kuwa una kipindupindu baada ya kutathmini dalili zako, sampuli ya kinyesi itachukuliwa kwa uchunguzi zaidi. Ikiwa vipimo vya maabara vitagundua sumu inayozalishwa na kipindupindu katika sampuli ya kinyesi, basi utambuzi wa kipindupindu unaweza kuthibitishwa. Kuthibitisha utambuzi wa kipindupindu ni muhimu, kwani hii inaweza kusaidia kuepusha ugonjwa huu kusambaa kwa wengine. 3

Je, kipindupindu hutibiwaje?

Matibabu ya kipindupindu yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo, kwani upungufu wa maji mwilini kutokana na kipindupindu kisichotibiwa unaweza kuhatarisha maisha ndani ya masaa machache. Ikiwa kipindupindu kitatibiwa mapema, wagonjwa wengi hupata nafuu.

Sehemu muhimu zaidi ya matibabu ya kipindupindu ni kurejesha maji mwilini. Hii inaweza kufanyika kwa kunywa ORS, ambayo huundwa kwa poda yenye chumvi na madini iliyochanganywa na maji safi. Njia nyingine ya kurejesha maji mwilini ni kupitia elekroliti (electrolytes) na kuongezewa maji kupitia mishipa ya damu (intravenous fluids). Ikiwa hauna upatikanaji wa bidhaa hizi, inashauriwa kunywa kiasi kikubwa cha maji kama vile maji safi au supu. Vinywaji vyenye sukari havishauriwi, kwani vinaweza kufanya hali ya kuharisha kuwa mbaya zaidi.

Watu walio na hali mbaya sana wanaweza kutumia dawa za antibiotiki sambamba na matibabu ya kurejesha maji mwilini. Antibiotiki zinaweza kusaidia mwili kupambana na bakteria wanaosababisha kipindupindu, na hivyo kupunguza muda wa kuumwa. 4

Unawezaje kujikinga na kipindupindu?

Kuna njia mbalimbali za kujikinga na kipindupindu. Kudumisha usafi mzuri, kama vile kunawa mikono kwa sabuni, kuandaa na kuhifadhi chakula kwa usalama, na kuondoa kinyesi kwa njia salama kiafya, kunaweza kukusaidia kuepusha kueneza bakteria wanaosababisha kipindupindu. Aidha, kuwa na upatikanaji wa maji safi ya kunywa na miundombinu ya msingi ya usafi ni jambo muhimu katika kuzuia kipindupindu.

Mashirika ya afya yana jukumu muhimu katika kuzuia kipindupindu. Ili kugundua haraka na kudhibiti milipuko, mashirika ya afya yanachunguza visa vya kipindupindu kwa ufuatiliaji wa karibu. Vilevile, mashirika ya afya uhakikisha kwamba matibabu ya kipindupindu yanapatikana kwa urahisi, kwani kipindupindu kinaweza kutibika kirahisi mradi matibabu yanaanzishwa mapema.

Ikiwa unaishi katika maeneo yanayojulikana kuwa na ugonjwa wa kipindupindu (endemic), kupata chanjo ya kipindupindu inaweza pia kusaidia kujikinga na ugonjwa huu. Watu wanaosafiri kupitia maeneo haya wanashauriwa kupata chanjo ya Dukoral, ambayo inaweza kutoa kinga dhidi ya kipindupindu kwa kipindi cha miaka miwili. 1

Hitimisho

Kipindupindu kinaweza kusababisha kuharisha sana na kutapika, ambavyo vinaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini. Kwa matibabu sahihi, kipindupindu kinaweza kutibiwa kirahisi na dalili zake hudumu kwa muda wa wiki 1, hata katika hali kali zaidi. Hata hivyo, ikiwa hakitatibiwa, kipindupindu kinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kutokana na upungufu mkubwa wa maji mwilini. Hivyo basi, ni muhimu kuwasiliana na daktari haraka iwezekanavyo ikiwa unapata dalili zozote za kipindupindu.

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Kipindupindu husababishwa na nini?
J: Kipindupindu husababishwa na bakteria aitwaye Vibrio cholerae. Bakteria huyu anaweza kuingia mwilini baada ya mtu kula au kunywa maji yenye bakteria hawa. Mara nyingi, kipindupindu huathiri watu wanaoshindwa kupata maji masafi ya kunywa na huduma za msingi za usafi.

S: Ugonjwa wa kipindupindu ni nini?
J: Kipindupindu ni maambukizi yanayosababishwa na bakteria Vibrio cholerae. Ugonjwa huu husababisha kuharisha sana na kutapika, ambavyo vinaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini. Ikiwa hautotibiwa, ugonjwa wa kipindupindu unaweza kusababisha kifo ndani ya masaa machache kwa baadhi ya watu.

S: Dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni zipi?
J: Dalili za kipindupindu kwa kawaida huanza kati ya masaa 12 hadi siku 5 baada ya kula chakula au kunywa maji yenye bakteria wa Vibrio cholerae. Dalili hizo ni pamoja na: Kuharisha sana, hasa kinyesi cha majimaji; Kutapika; na dalili nyinginezo.

S: Njia za kujikinga na kipindupindu ni zipi?
J: Kuna njia kadhaa za kujikinga dhidi ya kipindupindu, ikiwemo: kunawa mikono kwa sabuni baada ya kutumia choo na kabla ya kula; Kuweka na kuhifadhi chakula kwa usalama; Kutumia maji safi na salama ya kunywa; na kupata chanjo ya kipindupindu ikiwa unaishi au unasafiri maeneo yanayojulikana kuwa na kipindupindu.