Chunusi
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Chunusi ni nini?
Chunusi (acne in Swahili) ni ugonjwa wa ngozi ambao hutokea pale mafuta na seli za ngozi zilizokufa zinapoziba vinyweleo na kusababisha upele. Chunusi hutofautiana na vipele (pimples in Swahili) vya kawaida kwa kuwa chunusi husababisha vipele vingi kwa wakati mmoja na mara nyingi vipele hivi hujirudiarudia. 1
Chunusi ni tatizo la kawaida na huwapata watu wengi japo mara moja katika maisha yao. Kwa kawaida, chunusi huanza wakati wa balehe na hupungua katika utu uzima. Chunusi huweza kusababisha makovu ya ngozi, lakini mara nyingi hazisababishi madhara ya afya ya kudumu.
Dalili za Chunusi
Dalili za chunusi ni vipele, vipele vyenye maji au vipele vigumu. Vipele hivi huweza kuwa vyeusi, vyeupe au vyenye usaha chini ya ngozi. Kwa kawaida vipele hivi hutokea usoni, ila wakati mwingine zinaweza kutokea mabegani, mgongoni, kifuani au sehemu nyingine ya mwili. Ngozi inayozunguka vipele huwa na maumivu na kuwa nyekundu. Baada ya muda vipele vinakuwa vyeusi au kusababisha makovu. 2
Nini Husababisha Chunusi?
Chunusi hutokea pale seli za ngozi zilizokufa au mafuta zinapoziba vinyweleo. Mafuta yanayoendelea kukusanyika husababisha kuvimba na kuuma kwa eneo lililoathirika. Chunusi mara nyingi huanza katika ujana, kutokana na homoni zinazoanza kuzunguka mwilini wakati wa kubalehe. Mara nyingi chunusi hupungua katika utu uzima ingawa wakati mwingine zinaweza kudumu kwa muda mrefu.
Wakati mwingine chunusi zinaweza kurithiwa. Matumizi ya krimu au mafuta mazito yanayoziba vinyweleo wakati mwingine huchochea chunusi kutokea. Watu wenye matatizo ya homoni wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata chunusi.
Utambuzi
Utambuzi wa chunusi hufanyika kwa kuchunguza idadi ya vipele na kiasi gani vimeathiri ngozi. 3
Matibabu ya Chunusi
Matibabu ya chunusi huetgemea ukubwa wa tatizo. Njia rahisi huweza kupunguza dalili zake. Hizi hujuimisha kuosha uso na nywele mara kwa mara ili kupunguza mafuta. Kuepuka kutumia vipodozi, mafuta mazito pamoja na kuacha kuvuta sigara huweza kusaidia kupunguza dalili.
Inapaswa kuepuka kuminya au kutumbua chunusi. Kufanya hivyo huziba vinyweleo na kufanya chunusi kuwa mbaya zaidi. Baadhi ya wanawake hupata chunusi kutokana na mabadiliko ya mzunguko wa hedhi, hivyo wanapotumia vidonge vya majira wanaona kuwa chunusi hupungua.
Mtaalamu wa Afya huweza kupendekeza matibabu mengineyo ya chunusi.Hii hujumuisha tiba na miale ya leza (laser therapy), sabuni za uso zenye dawa, kutoa tabaka lenye seli zilizo kufa kwenye uso (facial peeling), dawa za kunywa na ikiwa kuna maambukizi ya bakteria, antibiotiki. Ushauri kuhusu sabuni za kuondoa chunusi hupatikana kutoka kwa wataalamu wa afya.
Haishauriwi kutumia limao kuondoa chunusi au kama dawa ya chunusi. Hali kadhalika, haiishauriwi kutumia limao kuondoa chunusi kwenye uso wenye mafuta. Lishe bora husaidia kupunguza chunusi. Hii ni pamoja na mboga za majani, matunda na wanga usiokobolewa.
Kuzuia Chunusi
Kuepuka kutumia mafuta mazito na vipodozi husaidia kuepuka na chunusi. Kuepuka vitu vinavyo sugua ngozi kama vile vitambaa vya kichwa, nguo nzito na mikanda inavyotumika kukaza nguo za ndani huweza kusaidia kupunguza baadhi ya dalili za chunusi.
Ubashiri
Mara nyingi chunusi hupungua unapoingia utu uzima. Aina kali ya chunusi au chunusi sugu huweza kusababisha makovu ya ngozi. Hali hii huweza kufanya mtu kutojithamini au kupunguza uwezo wa kujiamini. Wakati mwingine tatizo hili humuathiri mtu maisha yake yote.