1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Pumu

Pumu

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Pumu ni nini?

Pumu ni ugonjwa wa inflamesheni ambao huathiri njia za hewa kwenye mapafu. Ni mojawapo ya magonjwa yasiyoambukiza, ukikadiriwa kuathiri takriban watu milioni 235 duniani, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 1 Ugonjwa huu unaweza kuathiri wanaume, wanawake na watoto wa rika zote. Kwa kawaida huanza utotoni, lakini pia unaweza kujitokeza kwa mara ya kwanza kwa watu wazima.

Pumu huathiri hasa mirija ya bronchi (bronchial tubes) kwenye mapafu. Wakati wa shambulio la pumu, ambapo dalili za pumu huongezeka, watu hupata matatizo ya kupumua kutokana na inflamesheni ya njia za hewa, inayosababisha kupungua kwa mtiririko wa hewa kwenye mapafu. Pumu inaweza kutofautiana kwa ukali; dalili zake zinaweza kuwa kila siku au tu wakati wa shambulio la pumu. Dalili za kawaida za pumu ni pamoja na kutoa mlio kama wa filimbi wakati wa kupumua (wheezing), maumivu ya kifua na kupumua kwa shida. 1 2

Sababu za kwanini baadhi ya watu wanapata pumu na wengine hawapati bado hazijabainika kisayansi, lakini inaaminika kuwa vinasaba (jeni) vinachangia kwa kiwango kikubwa. Wakati pumu inapoanza, inaaminika kuwa ni kutokana na kuvuta vitu hewani, vinavyosababisha mzio katika njia za hewa.

Uchafuzi wa hewa, chavua na vizua mzio vinavyopatikana hewani ni baadhi ya vichochezi vya kawaida ambavyo husababisha mtu kupata pumu na/au vinaweza kuwa vichochezi vya mashambulizi ya pumu. Mtu anaweza kugundua kuwa visababishi vya mashambulizi yake ya pumu hubadilika baada ya muda. Kwa mfano, visababishi vya pumu utotoni vinaweza kuacha kusababisha dalili wakati wa utu uzima. 3

Kwa matibabu sahihi, pumu inayojitokeza katika umri wowote inaweza kudhibitiwa kwa ufanisi ili kupunguza athari zake kwenye ubora wa maisha ya mtu. Matibabu ya pumu uhusisha kuuelewa ugonjwa na kuepuka vichochezi vinavyosababisha dalili na matumizi ya dawa kadiri inavyohitajika ili kupunguza dalili na kutibu mashambulizi ya pumu. Dawa hizi mara nyingi huvutwa moja kwa moja kwenye mapafu kwa njia ya mvuke kwa kutumia nebulizer au inhaler, vifaa ambavyo ni rahisi kutumia na vimeundwa kwa ajili ya kusudi hili.

Vihatarishi vya pumu

Kuna sababu kadhaa zinazoongeza hatari ya kupata pumu, ikiwemo hizi zifuatazo: 4 5 6

  • Kuwa na magonjwa ya kurithi yanayohusiana na mzio kama vile pumu ya ngozi (atopic dermatitis), mafua ya mzio, au homa ya mzio (hay fever)
  • Historia ya magonjwa ya kurithi katika familia
  • Kuathirika na moshi kutoka bidhaa za tumbaku, ikiwa ni pamoja na kutumia tumbaku, kuwa eneo au maeneo ya watu wanaovuta sigara, na kuathirika na moshi wa sigara utotoni au kabla ya kuzaliwa kutokana na mama kuvuta sigara wakati wa ujauzito
  • Kuvuta hewa yenye vitu vinavyochochea dalili za pumu kutokana na mazingira ya kazi
  • Kuishi katika maeneo yenye uchafuzi mkubwa wa hewa
  • Maambukizi ya njia za hewa utotoni kama vile mkamba (bronchitis), ingawa uhusiano kati ya maambukizi haya na pumu bado haufahamiki
  • Unene kupita kiasi, ambao huongeza uwezekano wa kupata inflamesheni mwilini kwa ujumla, ikiwemo katika njia za hewa

Vihatarishi vya pumu vinavyohusiana na jinsia ya mtu hutegemea na umri wa mtu husika: wavulana wana uwezekano mkubwa wa kuugua pumu wakati wa utotoni kuliko wasichana, wakati wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuugua pumu katika utu uzima. Hali hii pengine inatokana na mabadiliko ya homoni yanayohusiana na mzunguko wa hedhi. 5

Aina za pumu kutokana na vichochezi maalum

Kuna aina kadhaa za pumu ambazo zinahusishwa na aina fulani za vichochezi, kwa mfano:

  1. Pumu ya mzio: Inasababishwa na vichochezi vya mzio kwa watu wenye mzio.
  2. Pumu inayosababishwa na mazoezi: Hutokea tu wakati wa kufanya mazoezi ya mwili.
  3. Pumu ya kazini: Husababishwa na vichochezi fulani (irritant particles) katika sehemu ya kazi (mfano, kutoka kwa bidhaa za kusafisha, moshi, vumbi la nafaka, au unga).

Kazi zenye hatari kubwa ya kusababisha pumu ni pamoja na: 7

  • Wazima moto
  • Wafanyakazi wanaoshughulika na kemikali
  • Wafanyakazi wa maandalizi au usindikaji wa chakula
  • Wafanyakazi wa hospitali
  • Wapiga rangi na wajenzi
  • Walezi wa wanyama
  • Wafanyakazi wa masuala ya kilimo

Kuelewa hatari hizi na vichochezi vya pumu kunaweza kusaidia katika kudhibiti na kuzuia pumu kwa ufanisi.

Dalili za pumu

Dalili za kawaida za pumu ni pamoja na: 1 8

  • Kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua (wheezing)
  • Kukohoa
  • Kifua kubana
  • Kupumua kwa shida

Kwa kawaida, dalili hizi: 8

  • Hujirudia mara kwa mara
  • Huweza kuwa kali zaidi asubuhi na/au usiku
  • Huwa mbaya zaidi baada ya shughuli fulani, kama vile baada ya kuwa karibu na kichochezi (trigger) kama moshi wa tumbaku au kufanya mazoezi

Pumu inaweza kuathiri mtu kwa viwango tofauti vya ukali, ambavyo hupimwa kitabibu kulingana na: 9

  • Mara ngapi dalili hujitokeza
  • Athari zake kwa uwezo wa mtu wa kufanya shughuli za kila siku na kuishi maisha yenye ubora
  • Athari za pumu kwa utendaji wa mapafu, hupimwa kwa vipimo vya utendaji wa mapafu
  • Kasi ya kupumua hewa nje, kipimo kinachofahamika kama Peak Flow

Ili kufuatilia dalili zao, watu walioathirika na pumu mara nyingi hufanya vipimo vya Peak Flow au Peak Expiratory Flow (PEF) mara 2 kwa siku, wakitumia kifaa kinachobebeka mkononi kiitwacho ‘Peak Flow Meter.’ Hii humruhusu mtu kugundua mabadiliko katika mpangilio wa kupumua, kubaini ikiwa hali inakuwa mbaya na hivyo kutumia dawa za kujikinga mapema ikiwa inahitajika.

Dalili za shambulio la pumu

Wakati wa shambulio la pumu, dalili za pumu huwa mbaya zaidi kwa muda mfupi. Katika mwili, shambulio la pumu husababishwa na uvimbe wa mirija ya hewa, na kusababisha mirija hiyo kuwa membamba ghafla, na kuzuia hewa kuingia kwenye mapafu.

Dalili za awali za shambulio la pumu ni pamoja na: 10

  • Dalili za pumu kuwa mbaya zaidi, hasa kukohoa na kupumua kwa shida
  • Haja ya kutumia dawa zinazotoa nafuu haraka mara nyingi zaidi kuliko kawaida
  • Muda wa kutokuwa na dalili baada ya kutumia dawa za kuleta nafuu (quick relief medications) kupungua isivyo kawaida, kwa mfano chini ya masaa 4 11
  • Kuchoka haraka zaidi baada ya shughuli fulani, hasa mazoezi

Wakati wa shambulio la pumu, mtu anaweza kupata baadhi au zote za dalili zifuatazo: 1 10

  • Dalili za kawaida za pumu, yaani kutoa sauti kama filimbi wakati wa kupumua, kukohoa na kupumua kwa shida ‒ zinaweza kuwa kali zaidi, na/au za kudumu
  • Kukakamaa kwa misuli ya shingo na kifua
  • Mlio wa kugongagonga kifuani
  • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
  • Kuhisi kuzimia au kuzimia
  • Kuishiwa pumzi, hali ambayo inaweza kuathiri kula, kuongea au kulala
  • Hisia za wasiwasi au hofu
  • Uso kubadilika rangi (mpauko)
  • Vidole au midomo yenye rangi ya bluu
  • Kutokwa jasho
  • Hali ya kusinzia
  • Uchovu
  • Kuchanganyikiwa
  • Kizunguzungu

Muda wa shambulio la pumu unaweza kutofautiana, kulingana na jinsi inflamesheni ilivyoathiri njia za hewa, na kwa muda gani. Shambulio la pumu linaweza kudumu kwa dakika chache, au katika visa vikali zaidi, masaa au siku. Shambulio la pumu la kawaida linaweza kuisha lenyewe au kwa dawa, wakati shambulio kali zaidi linaweza kuhitaji matibabu ya dharura ili kudhibiti dalili.

Watu wote walio na pumu huwa na maelekezo ya wazi yaliyoandikwa, yanayojulikana kama mpango wa kudhibiti pumu (asthma action plan), ambao hutoa ushauri juu ya jinsi ya kudhibiti pumu kwa ujumla, pamoja na kudhibiti wakati wa shambulio la pumu. Wakati shambulio la pumu linapotokea, mtu anapaswa kufuata mpango wa udhibiti na kutafuta matibabu ya dharura ikiwa dalili hazitokwisha kama inavyotarajiwa.

Dalili za pumu kwa watoto

Ikiwa mtoto ana kikohozi cha mara kwa mara, anaotoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua, maumivu au kubanwa kifua, au kupumua kwa shida, ni muhimu kumuona daktari, kwani moja au zaidi ya dalili hizi zinaweza kuashiria pumu ya utotoni.

Kama ilivyo kwa watu wazima, dalili za kawaida za pumu kwa watoto ni pamoja na: 8

  • Kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua
  • Maumivu ya kifua
  • Kupumua kwa shida

Dalili hizi zinaweza kuwa za kila siku au tu wakati wa shambulio la pumu. Pumu inaweza kusababisha usumbufu mkali na kuwa na athari kubwa kwa afya ya jumla ya mtoto, ikiwa ni pamoja na dalili kama uchovu, kupungukiwa nguvu, na kikohozi cha mara kwa mara.

Ishara na dalili zinazowezekana za pumu ya utotoni ni pamoja na:

  • Kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua
  • Maumivu ya kifua
  • Kubanwa kifua
  • Kupungukiwa nguvu baada ya kucheza au kufanya mazoezi
  • Kupungukiwa na nguvu siku nzima
  • Kupumua kwa shida
  • Kikohozi cha mara kwa mara, hasa usiku
  • Ngozi na misuli kwenye kifua kuingia ndani wakati wa kupumua (Chest retractions)

Watoto huathirika na pumu zaidi kuliko watu wazima, na kwa kawaida huanza kuonekana utotoni, mara nyingi kabla ya umri wa miaka mitano. Licha ya uwepo wa dalili zinazofanana za pumu, inaweza kuwa vigumu kugundua pumu kwa watoto wachanga na wadogo, kwani mapafu yao yanaweza kuwa hayajakomaa vya kutosha kufanya vipimo fulani.

Athari za pumu ya utotoni kwa ubora wa maisha na afya ya muda mrefu ya mtoto zinaweza kupunguzwa sana kwa kutambua njia sahihi za matibabu ili kudhibiti dalili zao. Watoto wenye pumu ambayo haijatibiwa huchoka haraka baada ya mazoezi kuliko wenzao na huwa na kikohozi na hutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua.

Kwa matibabu yanayofaa, inawezekana kupunguza dalili za pumu, ili watoto wenye pumu waweze kufanya shughuli zao za kila siku kama kawaida, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mazoezi na shughuli za nje ya nyumba. Kwa maelezo zaidi, unaweza kusoma makala hii kuhusu pumu ya utotoni.

Utambuzi wa pumu

Utambuzi wa pumu unahusisha mchanganyiko wa historia ya afya, uchunguzi wa mwili, na vipimo. Mchakato kwa ujumla hujumuisha: 12

  • Historia ya afya: Daktari atauliza kuhusu dalili, mara ngapi dalili hutokea, na vichochezi vyovyote vinavyojulikana. Historia ya ugonjwa wa pumu katika familia au mizio pia ni muhimu.
  • Uchunguzi wa Mwili: Uchunguzi wa kina wa mfumo wa upumuaji (respiratory system) ili kuchunguza dalili za pumu.
  • Kipimo cha Spirometry: Kipimo cha kawaida ambacho hupima kiasi (ujazo) na kasi (mtiririko) wa hewa inayoweza kuvutwa na kutolewa. Husaidia kutathmini kubana kwa mirija ya hewa.

Matibabu ya pumu

Ingawa hakuna tiba ya pumu, matibabu yanaweza kudhibiti dalili kwa ufanisi, na kuwezesha watu kuishi maisha ya kawaida. Matibabu ya msingi ni pamoja na matumizi ya vifaa vya kuvutia dawa mapafuni au vivutia dawa (inhalers), na vidonge na tiba nyingine zinazohitajika kwa mashambulizi makali ya pumu. Kwa kawaida, mpango wa kudhibiti pumu kulingana na dalili za mtu binafsi hutayarishwa na mtoa huduma wa afya, unaoorodhesha dawa, mikakati ya ufuatiliaji, na hatua za kuchukua wakati wa shambulio la pumu. 13

Vifaa vya kuvutia dawa mapafuni (Inhalers)

Vifaa vya kuvutia dawa mapafuni hutumika kama sehemu kuu ya matibabu ya pumu, ambavyo husaidia kuleta nafuu na kuzuia dalili: 13

  • Inhaler za kupunguza dalili: Kwa kawaida ni za rangi ya bluu, hizi hutoa nafuu ya haraka wakati wa shambulio la pumu, na hufanya kazi ndani ya dakika chache. Ikiwa zinatumika zaidi ya mara 3 kwa wiki, matibabu ya ziada yanaweza kuhitajika.
  • Inhaler za kuzuia dalili: Hutumika kila siku, na hupunguza inflamesheni katika njia za hewa na kuzuia dalili. Zinakuwa na dawa ya steroid na zinapaswa kutumiwa hata bila uwepo wa dalili.
  • Inhaler za mchanganyiko: Hizi huleta nafuu na kuzuia dalili kwa wakati mmoja, husaidia katika udhibiti wa dalili wa muda mrefu na nafuu ya haraka inapohitajika. Zinapaswa kutumiwa mara kwa mara, hata bila uwepo wa dalili.

Dawa

Ikiwa vifaa vya kuvutia dawa mapafuni pekee havitoshi, vidonge mbalimbali vinaweza kusaidia kudhibiti dalili za pumu: 13

  • Leukotriene Receptor Antagonists (LTRAs): Hutumika kila siku kuzuia dalili, hupatikana katika muundo wa kidonge, shira, au unga.
  • Theophylline: Hutolewa ikiwa matibabu mengine yameshindwa, hutumika kila siku kudhibiti dalili.

Dawa za Steroidi: Hutumika ama katika kuleta nafuu ya haraka wakati wa shambulio la pumu au kama tiba ya muda mrefu kwa pumu kali. Ufuatiliaji wa kawaida huhitajika kutokana na madhara yanayoweza kutokea.

Matibabu ya ziada

Katika visa nadra, matibabu mengine, kama sindano au upasuaji, yanaweza kuhitajika.

Hitimisho

Udhibiti wa pumu kwa ufanisi unahitaji mchanganyiko wa dawa sahihi, marekebisho ya mtindo wa maisha, na ufuatiliaji wa mara kwa mara. Ingawa hakuna tiba, matibabu kama ya vifaa vya kuvutia dawa mapafuni, vidonge, na tiba nyingine zinaweza kusaidia sana kuboresha maisha ya kila siku. Daima pata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuwa na mpango binafsi wa kudhibiti dalili za pumu. 

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Pumu ni ugonjwa gani?
J: Pumu ni ugonjwa sugu unaoathiri njia za hewa kwenye mapafu. Husababisha inflamesheni na kuziba kwa njia za hewa, na hivyo kufanya iwe vigumu kupumua. Dalili za pumu ni pamoja na kukohoa, kifua kubana, kupumua kwa shida, na kutoa sauti kama ya filimbi wakati wa kupumua (wheezing).

S: Dawa ya pumu sugu ni nini?
J: Dawa za pumu sugu ni pamoja na vifaa maalum vya kuvutia dawa mapafuni (inhalers au nebulizers) za kudhibiti na za kupunguza dalili. Inhaler za kuzuia dalili hutumiwa kila siku ili kupunguza inflamesheni na kuzuia dalili, wakati inhaler au nebulizer za kupunguza dalili hutumika wakati wa dalili za ghafla za pumu ili kupunguza athari za dalili kwa haraka. Aina nyingine za dawa ni pamoja na vidonge vya steroidi.

S: Ni zipi dalili za pumu kwa watu wazima?
J: Dalili za pumu kwa watu wazima ni pamoja na: kupumua kwa shida; kukohoa, hasa usiku au mapema asubuhi; kifua kubana; kutoa sauti kama filimbi wakati wa kupumua.

S: Ni zipi dalili za pumu kwa watoto?
J: Dalili za pumu kwa watoto ni pamoja na: kupumua kwa shida; kukohoa, hasa usiku au wakati wa kucheza; kifua kubana au maumivu ya kifua; kutoa sauti kama filimbi wakati wa kupumua.