1. Ada
 2. Magonjwa
 3. Maumivu ya Tumbo

Maumivu ya Tumbo

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Maumivu ya tumbo ni nini?

Maumivu ya tumbo ni hali ya kawaida ambayo karibu kila mtu hukabiliwa nayo wakati fulani maishani. Hii ni kwa sababu kuna visababishi vingi vinavyoweza kuchangia maumivu ya tumbo. Maumivu yanaweza kutokea bila kuwa na ugonjwa wowote unaotambulika. Hata hivyo, inaweza pia kusababishwa na matatizo ya mmeng'enyo wa chakula, inflamesheni, au maambukizi.

Maumivu ya tumbo yanaweza kutofautiana kwa kiwango cha ukali wa maumivu na yanaweza kujitokeza kwa njia tofauti. Mara nyingi huambatana na kichefuchefu, kutapika, au matatizo ya mmeng'enyo wa chakula. Karibu kila mtu anaweza kupata maumivu ya tumbo, lakini hali hii ni ya kawaida zaidi miongoni mwa wanawake vijana.

Uchunguzi wa kiafya unaweza kusaidia kubaini ikiwa kuna matatizo mengine ya kiafya yanayosababisha maumivu ya tumbo. Hata hivyo, katika visa vingi, maumivu ya tumbo yanaweza kudhibitiwa nyumbani bila kuhitaji matibabu zaidi..

Kuna tiba za nyumbani ambazo mara nyingi hutumika kukabiliana na maumivu ya tumbo, kama vile chai maalum, kuchua mwili, mazoezi mepesi na lishe sahihi. Ikiwa hayajasababishwa na matatizo mengine yoyote ya kiafya, maumivu ya tumbo kwa kawaida hupungua ndani ya saa chache.

Maumivu ya tumbo husababishwa na nini?

1. Maumivu ya tumbo bila sababu maalum

Mara nyingi, maumivu ya tumbo hujitokeza bila sababu maalum. Katika visa hivi, madaktari hushindwa kutambua ugonjwa maalum unaosababisha maumivu ya tumbo. Mara nyingi maumivu ya tumbo yanaweza kutibiwa nyumbani na hupona ndani ya muda mfupi.

Karibu kila mtu hupata maumivu ya tumbo wakati fulani maishani. Hii si lazima iwe ishara ya ugonjwa fulani. Hata hivyo, ikiwa maumivu yanaendelea au yanajirudia mara kwa mara, inapaswa kumuona daktari ili kubaini sababu nyingine zinazoweza kuwa zinasababisha hali hiyo.

Kuna uwezekano kwamba maumivu ya tumbo yanaweza kujirudia mara kwa mara kwa kipindi cha zaidi ya miezi 6 bila sababu inayotambulika. Katika visa hivi, inawezekana kwamba ugonjwa unaotambulika kama ‘functional abdominal pain,’ umetokea. Ugonjwa huu huwa hauponi kwa matibabu ya kawaida. 1

2. Hali za kiafya zinazoweza kusababisha maumivu ya tumbo

Maumivu ya tumbo yanaweza kusababishwa na hali mbalimbali za kiafya, zikiwemo:

 • Magonjwa ya tumbo na utumbo, kwa mfano maambukizi, inflamesheni au vidonda vya tumbo
 • Aina mbalimbali za matatizo ya mmeng'enyo wa chakula
 • Magonjwa yanayoathiri ini, figo, bandama, kibofu cha nyongo, kongosho, kidole tumbo, kibofu cha mkojo, moyo, mapafu, au uti wa mgongo
 • Matatizo ya kimetaboliki
 • Sababu za kisaikolojia au kiakili, kwa mfano wasiwasi au mashambulizi ya hofu

Ikiwa kuna shaka, daktari anapaswa kushirikishwa kwa ushauri zaidi. 2

3. Maumivu ya Tumbo Baada ya Kula

Wakati mwingine, maumivu ya tumbo hujitokeza mara moja au saa kadhaa baada ya mlo. Katika hali hiyo mara nyingi kuna kuwa na matatizo ya mmeng'enyo wa chakula yanayohusishwa na vyakula vyenye mafuta. Hali hii inaweza kusababisha gesi kujaa tumboni.

Vyakula vifuatavyo vinaweza kusababisha matatizo ya mmeng'enyo wa chakula na maumivu ya tumbo:

 • Mboga mbichi
 • Mboga jamii ya kunde kama maharagwe
 • Brokoli au kabichi vifundo (Brussels sprouts)
 • Kiasi kikubwa cha peremende
 • Milo yenye mafuta kama vile vyakula vya kuchoma

Sababu nyingine za maumivu ya tumbo baada ya mlo ni kiungulia, mawe kwenye kibofu cha nyongo, au mzio wa vyakula fulani. Hali hizi zinahitaji kufanyiwa uchunguzi na kutambuliwa na mtaalamu wa afya.

Dalili za Maumivu ya Tumbo

Maumivu ya tumbo mara nyingi huambatana na dalili zingine, kama vile:

 1. Kichefuchefu
 2. Kutapika
 3. Kujaa gesi tumboni
 4. Kuharisha
 5. Kufunga choo (constipation)

Ni muhimu kuzingatia eneo halisi na muda ambao maumivu hutokea. Taarifa hizi zinaweza kusaidia madaktari wakati wa uchunguzi. 3

Majibu ya maswali yafuatayo yanaweza kusaidia sana katika uchunguzi:

 • Je, maumivu yapo katika sehemu ya juu au ya chini ya tumbo au karibu na kitovu?
 • Je, maumivu yapo katika sehemu moja au yanasogea?
 • Je, maumivu yanachoma (sharp) au yanashinikiza (pressing)?
 • Je, maumivu hujitokeza asubuhi, jioni, usiku au baada ya mlo tu?

Utambuzi wa Maumivu ya Tumbo

Kama ilivyo kwa maumivu mengi, maumivu ya tumbo hayawezi kutambuliwa kwa aina yoyote ya kipimo. Kwa watu wengi, maumivu yanaweza kutofautiana sana kwa kiwango cha ukali. Kuna njia mbalimbali za kujaribu kupima kiwango cha ukali wa maumivu, kwa mfano kupitia kipimo kuanzia 0 (= hakuna maumivu kabisa) hadi 10 (= maumivu makali sana). Aidha, kwa maumivu ya tumbo, ni muhimu kujiridhisha ikiwa maumivu hayasababishwi na ugonjwa mwingine.

Matibabu ya Maumivu ya Tumbo

Kwa maumivu ya tumbo, kanuni ya jumla kuhusiana na hatua za kuchukua ili kujipatia nafuu ni kwamba unapaswa kuzingatia jinsi vitendo au tiba mbalimbali zinavyokufanya uhisi. Ikiwa kitendo au tiba fulani inapunguza maumivu na kukufanya ujihisi vizuri, kwa kawaida inakubalika kuwa ni vizuri kuendelea kuitumia. Kinyume chake, ikiwa kitendo au tiba inakuongezea maumivu na kujihisi hovyo, inapaswa kuepukwa. Kanuni hii inasisitiza kuzingatia mwitikio wa mwili wako ili kubaini njia bora ya kupunguza maumivu.

Watu wengi huripoti kwamba baadhi ya mambo yafuatayo yanaweza kusaidia kupunguza maumivu: 4

 • Unywaji wa chai ya mimea inayosaidia utulivu mwilini, kama vile jira au shamari (kiungo jamii ya karoti)
 • Kupasha mwili joto, kwa mfano kwa chupa ya maji ya moto au mto
 • Ufanyaji wa mazoezi mepesi kama kutembea
 • Kupumzika kwa wingi
 • Kuepuka msongo wa mawazo
 • Kunywa maji mengi, hasa ikiwa mtu anaharisha
 • Kukanda tumbo taratibu kwa mtindo wa kuanzia juu na kuzunguka kuelekea kulia (clockwise)
 • Kupumzika kwenye mazingira tulivu, kwa mfano kwa muziki wa taratibu

Lishe Sahihi kwa Maumivu ya Tumbo

Mara nyingi, lishe sahihi inaweza kusaidia kutuliza maumivu ya tumbo. Tabia zifuatazo za ulaji wenye manufaa kiafya zinapendekezwa kwa watu wenye maumivu ya tumbo:

 • Chakula chepesi, chenye mafuta kidogo
 • Tufaha zilizopondwa au ndizi (epuka ulaji wa matunda ya machungwa yenye asidi, kama vile malimau au balungi)
 • Tosti, wali, na pasta (kama vile, tambi, n.k.)
 • Karoti, shamari, au boga (zilizopikwa)
 • Kunywa maziwa kidogo kwa kadiri iwezekanavyo
 • Kunywa maji mengi (angalau lita 1.5 kwa siku kwa watu wazima)
 • Kuepuka pombe

Dawa za Maumivu ya Tumbo

Kuna dawa za kupunguza maumivu zinazopatikana kwenye duka la dawa. Dawa hizi mara nyingi zinaweza kusaidia kupunguza maumivu ya tumbo. Wafamasia pia wanaweza kupendekeza tiba za ziada za mitishamba. Mchanganyiko wa mitishamba mbalimbali kwa kawaida hutumika sana. 5 Probiotiki (virutubisho vinavyosaidia uwepo wa bakteria wazuri mwilini) inaweza kusaidia kustawisha afya ya utumbo. Hata hivyo, ni muhimu kila wakati kusoma maelezo ya matumizi ya Probiotiki ili kutumia kwa usahihi. 

Ni wakati gani unapaswa kumwona Daktari?

Kwa kawaida, maumivu ya tumbo si sababu ya kuhofia. Hata hivyo, inaweza kuwa ni vizuri kuzungumza na daktari wakati wa miadi yako ijayo.

Unapaswa kumwona daktari ikiwa maumivu ya tumbo: 6

 • Yanakuwa makali zaidi
 • Hayavumiliki
 • Yanabadilika
 • Yanajirudia mara kwa mara
 • Yanadumu kwa zaidi ya siku 2

Maumivu ya tumbo kama hali ya dharura

Ikiwa maumivu ya tumbo yanaambatana na changamoto nyingine kubwa za kiafya kama kupumua kwa shida, kupoteza fahamu, au kutokwa na damu, unapaswa kupiga simu kwa msaada wa dharura.

Maumivu ya tumbo yanawezaje kuzuilika?

Hakuna njia inayotumika duniani kote ya kuzuia maumivu ya tumbo. Bali kuna mbinu kadhaa kulingana na hali ya mtu binafsi na visababishi vya msingi vya maumivu husika.

Watu wengi wanapendekeza kwamba mbinu hizi zinaweza kusaidia kuzuia maumivu ya tumbo:

 • Kula lishe yenye manufaa kiafya
 • Ufahamu kuhusu mzio na vyakula ambavyo mtu hupata shida kumeng’enya (food intolerance)
 • Kuepuka msongo wa mawazo
 • Kupunguza matumizi ya pombe na bidhaa za tumbaku
 • Mazoezi ya mara kwa mara au kutembea umbali mrefu
 • Matibabu thabiti ya matatizo ya kiafya yaliyokwisha tambulika

Je, Maumivu ya tumbo yanaweza Kutibika?

Ikiwa maumivu ya tumbo hayajasababishwa na ugonjwa wowote, kwa kawaida hupungua baada ya masaa machache bila matibabu ya ziada. Matatizo mengi ya kiafya yanayosababisha maumivu ya tumbo ni rahisi kutibiwa. Ikiwa maumivu yanakuwa makali au yanadumu kwa muda mrefu, unapaswa kumwona daktari. Matibabu sahihi yanaweza kupunguza maumivu kwa ufanisi.

Hitimisho

Maumivu ya tumbo ni hali ya kawaida inayoweza kuathiri mtu yeyote. Ingawa mara nyingi huisha yenyewe, yanaweza kuwa ishara ya matatizo mengine ya kiafya. Ni muhimu kufuatilia dalili na kumwona daktari ikiwa maumivu yanakuwa makali, yanadumu kwa muda mrefu, au yanaambatana na dalili nyingine zenye kusababisha hofu. Kwa matibabu sahihi, maumivu ya tumbo yanaweza kudhibitiwa kwa ufanisi.

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Maumivu ya tumbo kwa mjamzito husababishwa na nini?
J: Maumivu ya tumbo kwa mjamzito yanaweza kusababishwa na mabadiliko ya homoni, kutanuka kwa mfuko wa uzazi (uterus), au matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Ikiwa maumivu ni makali au yanaambatana na dalili nyingine, ni muhimu kumwona daktari mara moja.

S: Madonda ya tumbo ni nini na husababishwa na nini?
J: Madonda ya tumbo ni vidonda vidogo vinavyotokea kwenye ukuta wa ndani wa tumbo au utumbo mdogo. Mara nyingi husababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori au matumizi ya muda mrefu ya dawa za kupunguza maumivu kama vile ibuprofen.

S: Maumivu ya tumbo upande wa kushoto husababishwa na nini?
J: Maumivu ya tumbo upande wa kushoto yanaweza kusababishwa na matatizo ya utumbo mkubwa, kidole tumbo, figo, au viungo vingine vya ndani. Maumivu haya yanaweza pia kuwa ishara ya ugonjwa wa Crohn, diverticulitis, au mawe kwenye figo.

S: Maumivu ya tumbo wakati wa hedhi husababishwa na nini?
J: Maumivu ya tumbo wakati wa hedhi, yanayojulikana kama dysmenorrhea, husababishwa na kukaza kwa misuli ya mfuko wa uzazi wakati wa kutoa utando wa ndani. Hali hii inaweza pia kuchangiwa na magonjwa kama vile endometriosis au fibroids.