Dalili za VVU na UKIMWI
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Muhtasari
- Maambukizi ya VVU na UKIMWI yanaweza kusababisha dalili mbalimbali kujitokeza, kuanzia dalili za mafua hadi kusababisha matatizo makubwa zaidi kiafya.
- Kuelewa umuhimu wa kupima afya mapema kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uthibiti na matibabu ya VVU na UKIMWI.
- Kwa waliotambuliwa kuwa na maambukizi ya VVU, maendeleo katika matibabu kama vile upatikanaji wa tiba ya kudhibiti virusi (antiretroviral therapy) yamekuwa yakirefusha maisha.
- Utambuzi wa dalili za awali na uhamasishaji wa upimaji afya wa mara kwa mara ni hatua muhimu katika kuzuia kuenea kwa maambukizi ya VVU na hatimaye UKIMWI.
Maambukizi ya VVU na UKIMWI yana dalili zinazoweza kutofautiana kulingana na hatua ya maambukizi 1. Makala hii inalenga kuangazia dalili za maambukizi ya hatua za awali na za mwisho. Pia, makala hii inaweka msisitizo katika jukumu muhimu la upimaji wa afya kwa wakati na ufanisi wa matibabu ya kisasa, na kuzingatia utofauti wa dalili kati ya wanaume na wanawake.
Kuna tofauti gani kati ya VVU na UKIMWI?
Virusi Vya UKIMWI (VVU) husababisha Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) kwa kushambulia kinga ya mwili (immune system), hasa seli za CD4 au T (T cells), ambazo husaidia kupambana na maambukizi mwilini. Iwapo maambukizi ya VVU hayatotambuliwa na kutibiwa, mtu hupoteza zaidi seli za T mwilini, na kusababisha iwe rahisi kushambuliwa na magonjwa. UKIMWI ni hatua ya mwisho na mbaya zaidi ya maambukizi ya VVU, ambapo mfumo wa kinga mwilini huwa dhaifu katika kukabiliana na magonjwa 2.
Dalili za VVU
Baada ya maambukizi ya awali, inawezekana mtu asionyeshe dalili yoyote kwa muda mrefu. Hata hivyo, ndani ya wiki chache baada ya kuambukizwa virusi husika, watu wengi hupata ugonjwa wa mithili ya mafua, ambao unaweza kudumu kwa wiki kadhaa. Dalili za mwanzo za UKIMWI au VVU ni pamoja na: 3
- Homa
- Maumivu ya kichwa
- Maumivu ya misuli na viungo
- Upele
- Maumivu ya koo na maumivu ya vidonda kinywani
- Kuvimba kwa tezi za limfu , haswa kwenye shingo
- Kuharisha
- Kupungua uzito
- Kikohozi na kupumua kwa shida
Katika hatua hii ya awali, VVU huzaliana kwa haraka na kuenea mwilini kote, na kusababisha kupungua kwa kinga ya mwili.
Unaambukizwaje VVU na kuwa kwenye hatari ya kuugua UKIMWI?
Mtu anaweza kuambukizwa VVU na mtu mwingine aliye na kiwango cha virusi hivyo kinachoweza kutambulika (detectable viral load). Majimaji fulani ya mwili yanaweza kuwa na virusi husika, kwa mfano: 4
- Damu
- Shahawa na majimaji kabla ya shahawa
- Majimaji kwenye njia ya haja kubwa
- Majimaji ya ukeni
- Maziwa ya mama
Majimaji haya yanapaswa kuingia kwenye mkondo wa damu ya mtu ili maambukizi yatokee. Hivyo basi, maambukizi yanaweza kutokea kwa njia ya kujamiiana, majeraha mabichi, au kudungwa sindano iliyotumika kwa mtu aliyeathirika na VVU. Aidha, mama anaweza kuambukiza mtoto wake VVU wakati wa ujauzito, kuzaa, au kunyonyesha.
Je, UKIMWI unatibika?
Hakuna tiba ya VVU au UKIMWI, lakini watu walio na VVU bado wanaweza kuishi maisha ya kawaida ikiwa watafuata masharti ya matibabu yao kwa usahihi. Kwa ujumla, kwa kadiri utambuzi (diagnosis) na matibabu vinavyofanyika mapema, ndivyo matokeo ya dalili za ugonjwa wa UKIMWI yanavyokuwa mazuri zaidi. Watu wengi wanaweza hata kuzuia maambukizi ya VVU yasifikie hatua ya UKIMWI kwa kutumia dawa maalum zinazodhibiti viwango vyao vya virusi kuwa vya chini kiasi cha kushindwa kutambulika (undetectable viral load).
Zaidi ya hayo, kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kuzuia kuambukizwa VVU. Mambo hayo ni pamoja na: 5
- Kujizuia kushiriki tendo la kujamiiana au kushiriki tendo hilo kwa njia salama ya matumizi ya kondomu kwa usahihi.
- Matumizi salama ya sindano.
- Matumizi ya PreP (pre-exposure prophylaxis), ambayo ni dawa inayotumika kama kinga kabla ya kushiriki tendo la kujamiiana lenye uwezekano wa kusababisha maambukizi ya VVU.
- Matumizi ya PeP (post-exposure prophylaxis), ambayo ni dawa inayoweza kuzuia VVU ikiwa itatumika ndani ya masaa 72 baada ya kushiriki tendo la kujamiiana lenye uwezekano wa kusababisha maambukizi ya VVU.
Dalili za UKIMWI kwa mwanaume na mwanamke
Ingawa dalili za awali zinafanana, baadhi ya dalili za VVU na UKIMWI zinaweza kutofautiana kulingana na jinsia kutokana na miundo tofauti ya kibayolojia na mwitikio wa kingamaradhi ya wanaume na wanawake.
Dalili za kawaida kwa wanaume:
Dalili za UKIMWI kwa mwanaume katika hatua za awali za ugonjwa huu ni pamoja na:
- Vidonda kwenye uume
- Ugonjwa wa malengelenge ya neva ngozini (herpes)
- Kuvimba kwa tezi za limfu kwenye eneo la kinena
- Dalili zinazohusiana na magonjwa nyemelezi kutokana na kudhoofika kwa mfumo wa kingamaradhi
Dalili za kawaida kwa wanawake:
Dalili za UKIMWI kwa mwanamke ni pamoja na: 7 8
- Mabadiliko katika mzunguko wa hedhi
- Vidonda ukeni
- Ugonjwa wa inflamesheni kwenye pelvisi (PID) usioitibika kwa urahisi
- Maambukizi sugu ya fangasi ukeni (vaginal candidiasis)
- Virusi vya papilloma kwa binadamu (HPV), vinavyosababisha seli zisizo za kawaida kwenye shingo ya kizazi kujirudia mara kwa mara
- Dalili zinazohusiana na magonjwa nyemelezi kutokana na kudhoofika kwa mfumo wa kingamaradhi
Pia ni muhimu kutambua kwamba kadiri hatua za maambukizi ya VVU zinavyoendelea bila matibabu, dalili za UKIMWI hujitokeza zaidi na zinaweza kujumuisha: 9
- Kupungua uzito kwa haraka (kukonda)
- Kuhisi uchovu mwingi bila sababu
- Kuvimba kwa tezi za limfu kwa muda mrefu
- Homa ya muda mrefu na kutokwa na jasho jingi usingizini wakati wa usiku
- Kuharisha kunakodumu kwa zaidi ya wiki moja
- Vidonda kinywani, kwenye njia ya haja kubwa, au sehemu za siri
- Matatizo ya mfumo wa neva kama vile sonona na kupoteza kumbukumbu
Dalili za UKIMWI hujitokeza wakati gani na hudumu kwa muda gani?
Dalili za awali za VVU huweza kutokea ndani ya wiki 2 hadi 4 baada ya maambukizi na kwa kawaida hudumu kwa wiki kadhaa. Hata hivyo, suala la dalili kujitokeza linaweza kutofautiana miongoni mwa watu, kwani baadhi ya watu huwa hawana dalili yoyote kwa miaka kadhaa. Iwapo maambukizi hayatodhibitiwa kwa matibabu, VVU hudhoofisha polepole mfumo wa kingamaradhi, na kusababisha dalili kali zaidi, na hatimaye kufikia hatua ya ugonjwa wa UKIMWI. Hatua ya maambukizi ya VVU hadi ugonjwa wa UKIMWI inaweza kuchukua miaka kadhaa. Lakini, ikiwa maambukizi ya VVU hayatodhibitiwa kwa matibabu, muda wa kuishi baada ya kufikia hatua ya UKIMWI ni takriban miaka 3. 10
Umuhimu wa kupima afya na kupata matibabu mapema
Kufahamu dalili za VVU ni muhimu, lakini kwa walio hatarini kuambukizwa, hakuna kitu kinachozidi umuhimu wa kupimwa afya mara kwa mara ili kubaini maambukizi ya VVU na magonjwa mengine yanayoenezwa kwa njia ya kujamiiana (STDs). Kwa maendeleo ya kisasa katika huduma ya matibabu, maambukizi ya VVU sasa ni hali inayoweza kudhibitiwa ikiwa itatambuliwa mapema na kutibiwa kwa usahihi kwa matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi hivi (Antiretroviral therapy). Hivyo basi, njia bora zaidi ya kuthibitisha maambukizi ya VVU ni kupima kwasababu magonjwa mengine yanaweza pia kusababisha dalili zinazofanana na zile za waathirika wa VVU. Kuwa na ufahamu wa hali yako kuhusiana na VVU kunakuwezesha kuchukua hatua zinazolinda afya yako na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya VVU katika jamii. 11 12
Hitimisho
Uelewa wa kina wa dalili za VVU na UKIMWI, pamoja na uelewa wa utofauti wa dalili hizo baina ya wanaume na wanawake, unaweza kusababisha utambuzi wa mapema na pia hatua za matibabu kuchukuliwa mapema. Maarifa ya kina yanayoenda sambamba na upimaji wa afya wa mara kwa mara ni kinga bora dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya VVU na hatimaye kufikia hatua ya UKIMWI. Ikiwa wewe binafsi au mtu unayemfahamu anaweza kuwa hatarini au anakabiliwa na dalili za VVU, ni muhimu kumuona mtaalamu wa afya haraka kwa ajili ya kupimwa na kupata ushauri kuhusu huduma za matibabu zinazoweza kupatikana.
Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)
S: Dalili za UKIMWI huchukua muda gani?
J: Pindi dalili za UKIMWI zinapojitokeza, zinaweza kuendelea na kuwa mbaya zaidi ikiwa muathirika hatopata matibabu. Ni muhimu kwa watu wanaokabiliwa na dalili zinazofanana na zile za waathirika wa VVU kutafuta msaada wa matibabu mara moja.
S: Virusi vya UKIMWI vinaishi muda gani nje ya mwili?
J: Virusi vya UKIMWI haviishi kwa muda mrefu nje ya mwili wa binadamu (kama vile kwenye vitu mbalimbali), na haviwezi kuzaliana. Huishiwa nguvu haraka katika mazingira makavu.
S: Dalili za mtu mwenye UKIMWI ni zipi?
J: Dalili za ugonjwa wa UKIMWI uliofikia hatua mbaya ni pamoja na kuharisha sana, homa kali, saratani fulani mwilini, kupungua uzito haraka, na magonjwa nyemelezi, ambayo ni magonjwa yanayotokea mara kwa mara au ni makali zaidi kwa watu walio na kinga dhaifu.
S: VVU ni nini?
J: VVU humaanisha Virusi Vya UKIMWI (Ukosefu Wa Kinga Mwilini), ambavyo hushambulia seli zinazosaidia mwili kupambana na maradhi, na hivyo kumfanya mtu kuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa na magonjwa. Yasipotibiwa, maambukizi ya VVU yanaweza kusababisha UKIMWI.