Ugonjwa wa Surua
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Surua ni nini?
Surua au kwa Kiingereza “measles” ni ugonjwa unaosababishwa na virusi. Ugonjwa wa surua unaweza kumpata mtu wa rika lolote ila huathiri zaidi watoto. Dalili za awali za surua ni koo kuuma, kikohozi , homa na madoa ya rangi ya kijivu au nyeupe kwenye sehemu ya ndani ya mashavu. Baada ya siku chache, upele mwekundu hutokea.
Hamna tiba maalum ya surua ingawa kupumzika na kunywa maji ya kutosha ni muhimu sana. Homa inaweza kudhibitiwa kwa dawa ikiwa inamfanya mtu kujihisi mgonjwa. Watu wenye surua wanaweza kuwaambukiza wengine wanapoanza kuwa na dalili za awali hadi siku 3 - 4 baada ya upele kutokeza. Watu wengi wenye surua hupata nafuu ndani ya wiki moja toka dalili za awali kujitokeza.
Dalili za Surua
Surua huweza kuambatana na dalili kama za mafua, kwa mfano kupiga chafya, macho kuwa mekundu na homa. Dalili nyingine ni kuonekana kwa madoa ya rangi ya kijivu au nyeupe kwenye sehemu ya ndani ya mashavu. Baada ya siku chache upele unatokea kwenye ngozi, mara nyingi unaanzia kichwani na shingoni. 1 2
Vihatarishi vya ugonjwa wa Surua
Surua husababishwa na virusi vinavyosambazwa kwa matone madogo hewani baada ya mtu mwenye surua kukohoa au kupiga chafya. 3 Watu ambao hawajapata chanjo ya ugonjwa huu wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa.
Utambuzi wa Surua
Utambuzi hufanywa kulingana na historia ya mgonjwa pamoja na uchunguzi wa kimwili. Inawezekana kufanya kipimo cha damu ili kuthibitisha maambukizi ya surua ya hivi karibuni, ingawa sio lazima kufanya hivyo.
Matibabu ya Surua
Hakuna matibabu maalumu ya surua zaidi ya kupumzika na kunywa maji mengi. Dalili kwa kawaida huisha ndani ya wiki moja. 4 Baadhi ya dawa huweza kutumika kupunguza homa na maumivu.
Kinga ya Surua
Surua ni ugonjwa unaoweza kuzuiliwa kwa chanjo. Hivyo basi, kuzingatia ratiba ya chanjo ya surua kwa watoto kunaweza kusaidia kuzuia maambukizi haya. 5 6 Mara chache sana mtu anaweza kupata surua hata baada ya kupata chanjo. Watu wenye surua wanapaswa kukaa nyumbani kwa angalau wiki baada ya upele kutokea ili kuepuka kuwaambukiza wengine.Watu ambao hawajapata chanjo na wamekutana na mtu mwenye surua wanapaswa kupata ushauri wa daktari juu ya namna ya kuzuia kusambaza maambukizi haya. 7
Ubashiri
Watu wengi hupona ndani ya wiki moja baada ya dalili zao kuanza na sio kawaida kupata madhara zaidi. Ugonjwa wa surua kwa watoto wenye matatizo mengine ya kiafya huweza kusababisha madhara zaidi, kama vile nimonia, homa ya uti wa mgongo, na ubongo kuvimba. 7