1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Nimonia

Nimonia

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Nimonia ni nini?

Nimonia ni maambukizi ya vifuko vya hewa (alveoli) katika mapafu, ambayo husababisha inflamesheni na mapafu kujaa maji au usaha. 1 Hali hii huathiri uwezo wa mapafu kupumua vizuri na kusambaza oksijeni mwilini, na kusababisha dalili mbalimbali kama kikohozi, homa, na kupumua kwa shida, pamoja na dalili kali zaidi. Maambukizi haya husababisha inflamesheni ambayo inaweza kuathiri tishu katika maeneo kadhaa, ikiwemo:

  • Mirija ya hewa katika mapafu, inayojulikana kama nimonia ya mrija wa hewa (bronchopneumonia)
  • Sehemu moja au zaidi za mapafu (nimonia ya sehemu ya mapafu)
  • Athari katikati ya vifuko vya hewa (nimonia ya katikati ya alveoli)

Aina za nimonia

Kuna zaidi ya visababishi 30 tofauti vya nimonia, vikiwemo bakteria, virusi, kuvu, na kemikali. 1 Visababishi hivi huathiri dalili na matibabu ya ugonjwa huu.

Nimonia pia huelezewa kulingana na mahali ilipopatikana, ambapo nimonia inayopatikana hospitalini inafahamika kuwa hatari zaidi kuliko nimonia inayopatikana katika jamii kutokana na uwezekano wa kupata maambukizi ya bakteria yenye usugu dhidi ya dawa za antibiotiki (antibiotic-resistant bacteria).

Vihatarishi vya nimonia

Mtu yeyote anaweza kupata nimonia katika umri wowote, lakini watu walio na umri chini ya miaka miwili au zaidi ya miaka 65 wako katika hatari kubwa zaidi. Pia, watu walio na hali duni ya afya kutokana na ugonjwa, lishe duni, au mfumo wa kinga ulio dhaifu kutokana na magonjwa kama vile pumu, UKIMWI/VVU, limfoma, kisukari, saratani ya damu (lukemia), au ugonjwa wa moyo wako hatarini zaidi. Wavutaji sigara na watu wanaokunywa pombe kupita kiasi pia wana uwezekano mkubwa wa kupata nimonia.

Pamoja na matatizo haya ya kiafya, watu waliolazwa hospitalini, hasa kama wanatumia mashine ya kusaidia kupumua (ventilator), wako katika hatari ya kupata nimonia inayofahamika kama ‘nimonia inayopatikana hospitalini.’ Watu wanaopata kemotherapi (tiba ya dawa zenye kemikali), watoaji na wapokeaji wa viungo vya mwili, au watu wanaotumia dawa za steroidi kwa muda mrefu wanaweza kuwa na mfumo wa kinga ulio dhaifu ambao huwafanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kuambukizwa nimonia. 2

Dalili za nimonia

Kwa kuwa nimonia inaweza kutofautiana kutoka hali isiyo kali hadi ile inayoweza kuhatarisha maisha na inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, kuna dalili tofauti zinazohusiana nayo. Dalili za kawaida za nimonia inayosababishwa na bakteria na virusi ni pamoja na: 1

  • Homa, kuhisi baridi, au kutokwa jasho
  • Kikohozi kinachoweza au kisichoweza kuwa na makohozi ya njano, kijani, au yenye damu
  • Uchovu
  • Kukosa pumzi
  • Maumivu ya kifua yanayoongezeka wakati wa kupumua kwa kina
  • Mapigo ya moyo kwenda kasi
  • Kupumua haraka
  • Kutokwa na jasho nyingi
  • Kuchanganyikiwa
  • Midomo au kucha kuwa na rangi ya bluu

Katika visa vya nimonia inayosababishwa na virusi, dalili hizi zinaweza kuwa mbaya zaidi na kujumuisha:

  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu ya misuli
  • Kudhoofika
  • Kikohozi kikali na kupumua kwa shida

Ni vyema kufahamu: Mtu ambaye anapumua kwa shida, anahisi baridi kali sana, au anayetoa kamasi za kijani au nyeusi anapaswa kuwasiliana na daktari mara moja.

Nimonia kwa watoto

Nimonia inapotokea kwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 10, inaitwa nimonia ya watoto au nimonia ya utotoni. Virusi vina uwezekano mkubwa zaidi wa kusababisha nimonia kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 kuliko bakteria. Na watoto wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata nimonia ya kutembea (aina ya nimonia isiyo na dalili kali) ikilinganishwa na watu wazima, hasa kutokana na uwezekano wa ugonjwa huu kusambaa katika maeneo kama shuleni.

Visa vingi vya nimonia ya utotoni si vikali, na watoto wenye nimonia wanaweza kuonyesha dalili za kawaida zaidi na kuwa na uwezekano mdogo wa kupata homa kali. Kwa kuwa ni vigumu zaidi kugundua dalili za nimonia kwa watoto wachanga, wazazi wanapaswa kuwa makini ikiwa mtoto anatapika, anaonekana mgonjwa, ni mdhoofu, ngozi imepauka au hatulii na analia kuliko kawaida.

Nimonia inayosababishwa na bakteria huwa kali zaidi, lakini ni ya kawaida zaidi kwa watoto wenye umri mkubwa. 3

Ni vyema kufahamu: Wazazi wanapaswa kutafuta matibabu haraka ikiwa mtoto wao anapata shida kupumua mpaka pua inatanuka wakati wa kupumua, wanapumua kwa haraka, au wanatumia misuli ya ziada kupumua – kwa mfano misuli ya tumbo, eneo juu ya mifupa ya bega, au chini ya mbavu kuonekana kutikisika kila anapopumua. 

Kama ilivyo kwa watu wazima, ikiwa mfumo wa kinga wa mtoto umeathirika kwa sababu ya mambo kama vile kulazwa hospitalini hivi karibuni, pumu au ugonjwa sugu, wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata nimonia. Watoto ambao hawajapata chanjo zote za utotoni au chanjo ya PCV13 (Prevnar) wana uwezekano mkubwa wa kupata nimonia. 4

Nimonia kwa wazee

Watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata nimonia na wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi makali zaidi. Watu waliolazwa hospitalini au wanaoishi kwenye nyumba za kulelea wazee wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na vimelea vinavyoweza kusababisha nimonia inayopatikana hospitalini, na magonjwa mengi ambayo wazee wana uwezekano mkubwa wa kuwa nayo, kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo na ugonjwa wa mapafu, yanahusishwa na nimonia – ingawa haijulikani ikiwa kudhibiti magonjwa haya moja kwa moja hupunguza uwezekano wa mtu kupata nimonia.

Ni vyema kufahamu: Ingawa dalili za nimonia zinazowapata wazee zinaweza kuwa sawa na zile za watu wa rika zote, baadhi ya wazee hupata dalili za uchovu au kuchanganyikiwa zaidi kuliko dalili zingine.

Utambuzi wa nimonia

Hatua ya kwanza katika kutambua nimonia ni uchunguzi wa kimwili, ambapo daktari ataangalia ikiwa kuna kupumua kwa kasi na rangi ya bluu au zambarau kwenye midomo, kucha au mikono, ambayo inaweza kuashiria viwango vya chini vya oksijeni kwenye damu. Kama sehemu ya uchunguzi huu, daktari hupima kiwango cha oksijeni kwenye damu kwa kutumia kifaa maalum kinachowekwa kwenye kidole.

Daktari pia atasikiliza kifua kwa kutumia stethoskopu ili kuchunguza uwepo wa milio isiyo ya kawaida kifuani. 

Hatua inayofuata kwa kawaida ni kuthibitisha utambuzi kwa x-ray ya kifua, na uthibitisho huu unaweza kumpa daktari taarifa za kutosha kuanza matibabu. Kulingana na dalili na ukali wake, hata hivyo, daktari anaweza kuagiza uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na:

  • Vipimo vya damu ili kuchunguza uwepo, aina, au kuenea kwa maambukizi, pamoja na kiwango cha oksijeni kwenye damu.
  • Kipimo cha makohozi ili kuchunguza uwepo wa maambukizi na kutambua vimelea vinavyosababisha maambukizi haya.

Matibabu ya nimonia

Antibiotiki zinaweza kutumika kutibu nimonia inayosababishwa na bakteria, mykoplasma, na aina nyingine za nimonia, na dawa za kuua fangasi zinaweza kutumika kwa nimonia inayosababishwa na fangasi. Nimonia inayosababishwa na virusi haiwezi kutibiwa kwa antibiotiki, lakini kwa kawaida huisha yenyewe.

Watu wengi hupona wakiwa nyumbani badala ya hospitalini. Matibabu ya kawaida ya nimonia yanahusisha kusaidia afya ya mwili na mfumo wa kinga, kama kuboresha lishe ya mtu aliyeathirika, kuongeza unywaji wa maji, au kupumzika. Matibabu mengine yanaweza kujumuisha kupunguza joto la mwili au kumpa mgonjwa oksijeni ili kumsaidia kupumua. Mtu mwenye umri mdogo anaweza kupona nimonia ndani ya siku chache kwa kutumia antibiotiki, wakati mtu aliye na umri wa zaidi ya miaka 60 au mwenye ugonjwa sugu anaweza kulazwa hospitalini kwa uangalizi na matibabu.

Baadhi ya watu hutumia dawa za kupunguza maumivu zinazopatikana kwenye duka la dawa kama vile aspirini, acetaminophen (panadol) au ibuprofen. Ingawa wengine hutumia dawa za kuzuia kikohozi, kukohoa kidogo huhitajika ili kuondoa maji na kamasi zilizokusanyika kwenye mapafu na njia za hewa.

Kinga ya nimonia

Chanjo ya homa ya mafua inaweza kusaidia kuzuia aina zote za nimonia; mwili una uwezekano zaidi wa kuathiriwa na nimonia na maambukizi mengine wakati mfumo wa kinga umedhoofishwa na homa ya mafua. Hata hivyo, kuna chanjo mbili zinazopatikana nchini Marekani, yaani PPSV23 (Pneumovax) na PCV13 (Prevnar 13). 

Chanjo ya PCV13 pia imeingizwa katika mpango wa chanjo nchini Tanzania, ikisaidia kuzuia nimonia kwa watoto wadogo. Ingawa chanjo hizi haziwezi kuzuia visa vyote vya nimonia, zinatoa kinga muhimu dhidi ya maambukizi yanayosababishwa na bakteria wa Streptococcus pneumoniae.

Mtu yeyote anaweza kuchukua tahadhari za msingi za kujikinga na nimonia, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuka kuenea kwa maambukizi na kudumisha mtindo wa maisha wenye manufaa kiafya, kama vile kula chakula bora na kupata mapumziko na mazoezi ya kutosha.

Hitimisho

Nimonia ni ugonjwa hatari ambao unaweza kuathiri watu wa rika zote, lakini hasa watoto wadogo, wazee, na wale wenye magonjwa sugu. Chanjo na hatua za kimsingi za kujikinga, kama kunawa mikono na kudumisha afya njema, zinaweza kusaidia kupunguza hatari ya kuambukizwa. Ni muhimu kufahamu dalili za nimonia na kuchukua hatua za haraka ikiwa zitatokea ili kuepusha matatizo zaidi. Kwa matibabu sahihi na ya haraka, watu wengi wanaweza kupona nimonia na kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Maswali yanayoulizwa mara kwa mara (FAQs)

S: Nimonia ni nini?
J: Nimonia ni maambukizi ya vifuko vya hewa (alveoli) kwenye mapafu, ambayo husababisha inflamesheni na mapafu kujaa maji au usaha. Hali hii huathiri uwezo wa mapafu kupumua na kusambaza oksijeni mwilini.

S: Dalili za nimonia kwa watoto ni zipi?
J: Dalili za nimonia kwa watoto zinaweza kuwa tofauti kidogo na za watu wazima. Watoto wanaweza kuwa na kikohozi, homa, kukosa hamu ya kula, kupumua kwa kasi, na kuziba pua. Pia, watoto wachanga wanaweza kuonekana wamechoka, ngozi kupauka rangi au kuwa na rangi ya bluu, na kulia zaidi kuliko ilivyo kawaida.

S: Dalili za nimonia kwa watu wazima ni zipi?
J: Dalili za nimonia kwa watu wazima ni pamoja na kikohozi kinachoweza kutoa makohozi ya rangi ya kijani, njano au damu, homa, kutetemeka kwa mwili, jasho jingi, kupumua kwa shida, maumivu ya kifua hasa unapopumua kwa kina, na kuchoka kupita kiasi. Watu wazee wanaweza pia kuhisi kuchanganyikiwa au kuchoka zaidi kuliko kawaida.