1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Trikomonasi au Trichomoniasis

Trikomonasi au Trichomoniasis

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Trikomonasi ni nini?

Trikomonasi ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya kujamiiana (STD) unaosababishwa na vimelea vijulikanavyo kama Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu mara nyingi huathiri wanawake wenye umri wa miaka 40 hadi 49, lakini unaweza kumuathiri mtu yeyote anayeshiriki tendo la kujamiiana, ikiwemo na wanaume pia ingawa mara nyingi wanaume wanaweza wasionyeshe dalili zozote za maambukizi.

Dalili za kawaida zinaweza kujumuisha kutoka kwa uchafu uumeni au ukeni, kuwashwa kwa sehemu za siri, hisia ya kuungua unapotoa mkojo, na maumivu wakati wa kujamiiana. 1 Dawa za antibiotiki hutibu kwa ufanisi maambukizi ya trikomonasi.

Maambukizi ya Trichomonas vaginalis yanaweza kusababisha inflamesheni ya viungo vya uzazi kama vile: 2

  • Urethritis: Inflamesheni katika mrija wa mkojo (mrija unaoruhusu mkojo kutoka nje ya mwili)
  • Cystitis: Inflamesheni katika kibofu cha mkojo
  • Vaginitis (kwa wanawake): Inflamesheni katika uke
  • Epididymitis (kwa wanaume): Inflamesheni katika epididymis, ambao ni mrija ulio nyuma ya kila korodani ambapo mbegu za kiume hupevuka 
  • Prostatitis (kwa wanaume): Inflamesheni katika tezi dume

Vihatarishi vya Trikomonasi

Trikomonasi inaweza kuambukizwa kwa kujamiiana bila kinga. 3 Hata hivyo, vimelea hawa hawadhaniwi kuenezwa kwa kujamiiana kwa njia ya mdomo (oral sex) au haja kubwa (anal sex). Vihatarishi vya maambukizi vinaweza kujumuisha:

  • Kujamiiana bila kutumia kondomu
  • Kuwa na wapenzi wengi unaoshirikiana nao tendo la kujamiiana
  • Kuwa na historia ya kuugua magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana (STDs)
  • Kutumia vifaa vya ziada kama midoli (sex toys), ambavyo havijasafishwa vizuri wakati wa kujamiiana

Dalili za Trikomonasi

Dalili za Trikomonasi hutofautiana kulingana na mtu aliyeathirika. Kwa wanawake, dalili zinaweza kujumuisha: 2 1

  • Kutokwa na uchafu usio wa kawaida ukeni; unaweza kuwa kidogo au mwingi, wenye povu, rangi ya njano-kijani na harufu ya samaki
  • mwasho, maumivu na kuvimba katika eneo linalozunguka uke
  • Maumivu wakati wa kukojoa: pia hali hii hufahamika kitaalamu kama dysuria
  • Maumivu wakati wa kujamiiana: pia hali hii hufahamika kitaalamu kama dyspareunia

Wanaume kwa kawaida huwa hawaonyeshi dalili zozote. Hata hivyo, ikiwa wana inflamesheni katika kiungo cha uzazi, wanaweza kuwa na dalili zifuatazo: 3 2 1

  • Kutokwa na uchafu mweupe kwenye uume
  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Maumivu, wekundu na kuvimba katika eneo linalozunguka uume

Ni muhimu pia kukumbuka kwamba ingawa wanaume wanaweza wasionyeshe dalili zozote, bado wanaweza kuwaambukiza wenzi wao. 1

Jinsi ya kutambua trichomoniasis

Maambukizi ya Trikomonasi hushukiwa kwa wanaume na wanawake wanaoonyesha viashiria na dalili za inflamesheni ya viungo vya uzazi zinazosababishwa na vimelea vya Trikomonasi. Daktari anaweza kushuku maambukizi na kuchukua historia ya mgonjwa pamoja na kufanya uchunguzi wa kimwili. 5

Baada ya hatua tajwa hapo juu, vipimo vya maabara huweza kufanyika, na daktari au muuguzi anaweza kuchukua sampuli kutoka kwenye uume au uke. Sampuli hizo huchunguzwa na vipimo hujumuisha: 2 5

  • Hadubini (Microscopy): kuchunguza sampuli kwa kutumia hadubini ili kubaini vimelea vya Trikomonasi haraka.
  • Utaratibu wa ukuzaji wa vimelea (culture) au ‘kalcha’: sampuli kutoka kwenye uume au uke hupelekwa maabara na hukuzwa (cultured) kwa siku kadhaa ili kubaini uwepo wa vimelea.

Kutoka kwa sampuli zilizokusanywa, kipimo kinachofahamika kama Nucleic Acid Amplification (NAAT) pia kinaweza kutumika kubaini Trikomonasi na kinachukuliwa kama kipimo bora (gold standard) zaidi ya vipimo vilivyopo. Mbinu hii ya kipimo cha NAAT hufanya vijidudu viwe rahisi kubaini na pia hupatikana kama kifaa cha kujipima mwenyewe (self-test kit).

Kwa wanaume, sampuli ya mkojo pia inaweza kutumika kutambua Trikomonasi. Sampuli ya mkojo inaweza kufanyiwa kalcha, na hivyo kuongeza uwezekano wa utambuzi. Ikiwa Trikomonasi inashukiwa, matibabu ya antibiotiki yanaweza kuanza kabla ya matokeo ya vipimo ili kuhakikisha muathirika anapata matibabu ya haraka na kuzuia asiambukize wengine. 5

Matibabu ya Trikomonasi

Matibabu ya Trikomonasi yanahusisha dawa za antibiotiki. Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kwa sasa kinapendekeza kutumia Metronidazole kutibu Trichomonasi. CDC inapendekeza: 6

  • Metronidazole 500 mg mara 2 kwa siku kwa siku 7 (kwa wanawake)
  • Metronidazole 2 g mara 1 kwa dozi 1 (kwa wanaume)

Ni muhimu kwa mwenzi au wenza wa muathirika pia kutibiwa ili kuweza kutibu maambukizi ya Trikomonasi kikamilifu. Metronidazole inaweza kuwa na madhara, ikiwa ni pamoja na hisia ya ladha ya chuma kinywani, na ikitumiwa na pombe, inaweza kusababisha kichefuchefu na ngozi kuwa nyekundu. 2

Kutumia dozi 1 ya Tinidazole 2 g ni dawa inayoweza kutumika badala ya metronidazole. 6 Tinidazole inaweza kuwa na ufanisi zaidi na madhara machache; hata hivyo, inaweza kuwa ghali. 6

Kuna hatua za msingi ambazo unaweza kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya trikomonasi; na hatua hizo ni pamoja na: 2 7

  • Matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya kondomu
  • Kuepuka tabia za kingono zisizo salama kama vile kubadilisha wapenzi mara kwa mara au kushiriki tendo la kujamiiana na mpenzi ambaye ana wapenzi wengi
  • Kuepuka kushiriki vifaa vya ziada kama vile midoli (sex toys) wakati wa tendo la kujamiiana

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Kutokwa na majimaji ukeni ni dalili ya nini?
J: Kutokwa na majimaji ukeni kunaweza kuwa dalili ya maambukizi kama vile trikomonasi, fangasi, au bakteria. Pia inaweza kuwa dalili ya mabadiliko ya homoni au mzunguko wa hedhi. Ni muhimu kumuona daktari kwa uchunguzi na matibabu sahihi.

S: Magonjwa ya ngono yanaweza kuzuiliwa vipi?
J: Magonjwa ya ngono (STDs) yanaweza kuzuiliwa kwa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana, kuwa na mpenzi mmoja aliye mwaminifu, kupima na kutibu magonjwa ya ngono mara kwa mara, na kuepuka kushiriki vifaa vya ngono (sex toys) bila kuvisafisha vizuri. Elimu kuhusu ngono salama pia ni muhimu katika kujikinga na maambukizi.

S: Magonjwa ya zinaa huweza Kutibiwa?
J: Baadhi ya magonjwa ya zinaa kama vile kisonono na klamidia yanaweza kutibiwa na kupona kabisa kwa kutumia dawa za antibiotiki. Pia, magonjwa mengine kama VVU yanaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa za kupunguza makali au kuzuia kusambaza maambukizi kwa wengine.