1. Ada
 2. Magonjwa
 3. Maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI)

Maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI)

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Maambukizi ya mfumo wa mkojo ni nini?

Maambukizi ya mfumo wa mkojo (maarufu kwa kiingereza kama UTI) ni maambukizi katika sehemu yoyote ya njia ya mkojo.

 • Mfumo wa mkojo una undwa na sehemu mbili, sehemu ya juu na ya chini;
 • Sehemu ya juu hujumuisha figo pamoja na ureta, mirija inayosafirisha mkojo kutoka kwenye figo hadi kwenye kibofu cha mkojo.

Sehemu ya chini hujumuisha kibofu cha mkojo pamoja na mirija inayotoa mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili (urethra).

Maambukizi haya husababishwa na bakteria. Ugonjwa huu hutokea zaidi kwa wanawake kuliko wanaume. Dalili za ugonjwa huu hujumuisha homa, maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo na maumivu wakati wa kukojoa. Kwa matibabu ya antibiotiki watu wengi hupona haraka. 1

Visababishi

Mara nyingi maambukizi ya mfumo wa mkojo husababishwa na bakteria ambao hupanda kupitia mrija wa mkojo (urethra) kwenda kwenye kibofu. Wakati mwingine hupanda juu zaidi na kwenda kwenye figo. Wakati mwingine virusi au fangasi huweza kusababisha hali hii. Hii hutokea zaidi kwa watu wenye upungufu wa kinga ya mwili. 2

Vihatarishi

Wanawake wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi haya kuliko wanaume. Hii ni kwa sababu ya ukaribu wa njia ya mkojo na njia ya haja kubwa pamoja ufupi wa urethra, mrija unaotoa mkojo nje ya mwili. Sababu nyingine zinazowaweka wanawake kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo ni:

 • Ujauzito
 • Kujamiiana, hii huweza kusaidia bakteria au vimelea vingine vilivyopo kwenye njia ya haja kubwa kusogea karibu na njia ya mkojo
 • Mabadiliko ya homoni baada ya hedhi kukoma.

Wanaume pia huweza kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo. Vihatarashi kwa wanaume ni pamoja na hali zinazosababisha kuziba kwa njia ya mkojo ikiwemo kuvimba kwa tezi dume. Watoto wachanga ambao hawajatahiriwa pia huweza kupata hali hii kirahisi. 3

Kuwa na udhaifu wa mfumo wa kinga ya mwili, kutumia mipira ya mkojo na kisukari humuweka mtu kwenye hatari ya kupata maambukizi haya. 4

Dalili za UTI

Dalili za maambukizi ya njia ya mkojo (dalili za UTI) zinatofautiana baina ya mtu na mtu. Pia dalili hutegemea na sehemu ya mfumo wa njia ya mkojo iliyoathirika.

Dalili za kawaida za maambukizi ya sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo ni pamoja na: 5

 • maumivu wakati wa kukojoa,
 • kukojoa mara kwa mara,
 • maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo
 • Kukojoa mkojo wenye harufu kali,
 • Damu kwenye mkojo ingawa hii hutokea mara chache

Dalili za kawaida za maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo: 6

 • Homa,
 • Kuhisi baridi,
 • Kujihisi vibaya.
 • Maumivu katika sehemu ya ubavu au mgongo huweza kuashiria kuwa maambukizi yamesambaa kwenye figo.

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na dalili pamoja na uchunguzi wa kimwili. Kipimo cha mkojo huchukuliwa maabara ili kuthibitisha uwepo wa bakteria wanaosabisha hali hii.  Wakati mwingine vipimo damu au usaha kama upo pia hufanyika. Hii husaidia kutambua kama ugonjwa umesambaa sehemu nyingine mwilini. 

Ultrasound ya kibofu cha mkojo na figo huweza kuhitajika ikiwa mtu anapata maambukizi haya mara kwa mara. 3

Matibabu

Maambukizi ya mfumo wa mkojo hutibiwa kwa antibiotiki. Kunywa maji ya kutosha husaidia kutoa bakteria kutoka kwenye kibofu. Watu hushauriwa kupumzika ikiwa maambukizi yameathiri figo. Kama maambukizi haya yanasababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa mkojo au kitu kinachoziba kibofu cha mkojo, basi matibabu ya ziada huhitajika.

Kinga

Usafi mzuri wa eneo ambalo mkojo hutoka mwilini husaidia kuzuia maambukizi ya mfumo wa njia ya mkojo. Kuelimisha watoto wa kike kujisafisha kuanzia mbele kwenda nyuma wanapomaliza kukojoa pia husaidia. Kukojoa baada ya kujamiiana pia huweza kusaidia wanawake kujikinga na maambukizi haya. Kwa baadhi ya watu ambao maambukizi haya hujirudia, huweza kushauriwa kutumia dawa za antibiotiki. 7

Utabiri

Kwa matibabu sahihi ya antibiotiki, maambukizi ya kibofu cha mkojo hupona ndani ya siku chache bila madhara yoyote. Maambukizi ya figo kwa kawaida huchukua muda mrefu zaidi na huweza kusababisha makovu kwenye figo. Maambukizi ya mfumo wa mkojo huweza kujirudia, hasa kwa watu wenye magonjwa mengineyo.