1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Sinusitis ya Virusi (Maambukizi ya Sinus)

Sinusitis ya Virusi (Maambukizi ya Sinus)

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Sinusitis (Maambukizi ya Sinus) ni Nini?

Sinusitis, ambayo pia inajulikana kama maambukizi ya sinus au rhinosinusitis, ni inflamesheni ya sinus. Sinus ni vishimo vilivyojaa hewa ndani ya mifupa ya uso na pua; sinusitis hutokea wakati vishimo hivi vinavyopata inflamesheni na kuziba, na kusababisha kujikusanya kwa makamasi na hewa. Ni hali ambayo kwa kawaida hutokea baada ya mafua. 1

Dalili za sinusitis ni pamoja na kutokwa na kamasi, pua kuziba, maumivu na kichwa kuuma kikiguswa, na maumivu ya kichwa ya sinus (kuhisi kukandamizwa kwenye eneo la macho, mashavu, na paji la uso).

Kwa ujumla, sinusitis siyo ugonjwa hatari na unaweza kudhibitiwa kwa kuitunza afya yako na kwa kutumia dawa zinazopatikana kwenye maduka ya dawa. Katika visa vingi, dalili huisha ndani ya wiki 2 hadi 3.

Aina za Sinusitis

Kuna aina 2 za sinusitis: 2

  1. Sinusitis ya muda mfupii: Sinusitis ya muda mfupi (acute) ni maambukizi yanayojitokeza ghafla na hudumu kwa muda mfupi. Maambukizi yanaweza kudumu kwa takriban wiki 1, ingawa ni kawaida pia kwa maambukizi haya kudumu kwa muda wa wiki 2 hadi 3. Watu wanaopata mafua mara nyingi pia hupata aina hii ya sinusitis isiyo na dalili kal, na watu wengi hupata sinusitis ya muda mfupi mara 1 au mara 2 tu maishani.
  2. Sinusitis sugu (Chronic): Sinusitis sugu ni nadra zaidi kuliko sinusitis ya muda mfupi. Hufahamika kama sinusitis sugu inapodumu kwa zaidi ya wiki 12. Katika visa vingi, sinusitis sugu husababishwa na sinusitis ya muda mfupi.

Dalili za Sinusitis (Maambukizi ya Sinus)

Sinusitis mara nyingi hutokea baada ya kuugua mafua. Ikiwa dalili zifuatazo zitajitokeza sambamba na dalili mbalimbali za mafua, inaweza kuashiria uwepo wa maambukizi ya sinusitis: 3 4

  • Kutokwa na majimaji ya njano au kijani puani
  • Pua kuziba au kutiririsha
  • Maumivu na maeneo y sinus kuuma yakiguswa (kwa kawaida maumivu siyo makali sana katika sinusitis sugu)
  • Mkandamizo kwenye sinus
  • Homa (zaidi ya 38°C / 100.4°F)
  • Maumivu ya meno
  • Kupungua kwa uwezo wa kunusa (hii hutokea zaidi katika sinusitis sugu)
  • Harufu mbaya kinywani

Katika visa vya sinusitis sugu, ukali wa dalili unaweza kubadilika kulingana na muda. Mwanzoni mwa sinusitis ya muda mfupi, dalili zinaweza kuwa kali lakini hupungua baada ya muda wa siku au wiki kadhaa, na kuacha dalili zisizo kali kama vile maumivu kiasi katika sinus na pua kuziba. Sinusitis ya muda mfupi inaweza kujirudia, na kufanya tena dalili kuwa kali. 

Dalili kama vile koo kuuma, maumivu ya kichwa, na kikohozi, zinaweza kujitokeza wakati wa maambukizi ya UVIKO-19 na sinusitis.

Wakati wa Kumuona Daktari

Mara nyingi, dalili za sinusitis zisizo kali hazimlazimu muathirika kumuona daktari. Hata hivyo, ikiwa dalili zifuatazo zitajitokeza, inashauriwa kwenda kwa daktari kwa ajili ya matibabu:

  • Dalili ni kali
  • Dalili zinazidi kuwa mbaya
  • Maambukizi ya sinus yanajirudia mara kwa mara

Visababishi vya Sinusitis

Visababishi vya sinusitis ya muda mfupi na sinusitis sugu hutofautiana

Visababishi vya Sinusitis ya Muda Mfupi

Katika visa vingi, sinusitis ya muda mfupi husababishwa na maambukizi ya virusi. Hii mara nyingi huwa ni virusi vilivyosababisha mafua. Hali hii pia inaweza kusababishwa na bakteria, ingawa ni nadra. Maambukizi ya bakteria hutokea katika takriban asilimia 0.5 hadi 2 ya visa. 5

Visababishi vya Sinusitis Sugu

Visababishi vya sinusitis sugu ni venye vyanzo vingi kuliko vile vya sinusitis ya muda mfupi. Ingawa maambukizi ya virusi yanaweza kuchangia sinusitis sugu, inflamesheni ya muda mrefu mara nyingi hutokea kutokana na sababu zingine za kiafya. 6 7

Wataalamu wa masuala ya kitiba wamebaini aina 3 za sinusitis sugu, kila moja ikiwa na visababishi tofauti:

1. Sinusitis sugu bila polipsi (vivimbe) ya pua: Aina iliyoenea zaidi; husababishwa na mzio wa vitu vinavyopatikana hewani, mwasho kutoka kwa vitu vinavyopatikana hewani, na maambukizi.

2. Sinusitis sugu yenye polipsi ya pua: Polipsi za pua ni vinyama visivyo vya kawaida vinavyoota ndani ya pua. Wakati polipsi zinapokuwa kubwa au nyingi, zinaweza kuziba njia za hewa na kusababisha sinusitis. Sababu za baadhi ya watu kupata polipsi za pua hazifahamiki.

3. Sinusitis sugu na mzio wa kuvu: Hewa mara nyingi huwa na kiasi kidogo cha kuvu, ambacho watu wengi wanaweza kuvuta bila tatizo. Hata hivyo, wengine wanaweza kupata mzio kwa kuvu hii, ambayo husababisha kamasi nzito kujikusanya kwenye sinus. Hali hii inaweza kusababisha sinusitis sugu.

Mambo kadhaa yanaweza kuongeza hatari ya kupata sinusitis sugu au kusababisha dalili kuwa mbaya zaidi. Mambo hayo ni pamoja na:

  • Mizio, hasa ile ambayo hutokea majira yote ya mwaka, inaweza kuongeza hatari ya sinusitis sugu na kuzidisha dalili zake. Mizio hii ni pamoja na ile ya vijidudu vya vumbini, manyoya ya wanyama, na kuvu.
  • Vitu vinavyopatikana hewani na kuweza kukera au kuathiri mwili: Hii ni pamoja na moshi wa tumbaku na kemikali ya fomaldehidi (formaldehyde), ambavyo huweza kuongeza hatari ya kupata sinusitis sugu.
  • Watu wenye tatizo la mfumo wa kinga wako kwenye hatari kubwa ya kupata sinusitis sugu.

Utambuzi wa Sinusitis

Mara nyingi, sinusitis hupona yenyewe bila matibabu maalum ndani ya wiki 1 hadi 3. Hata hivyo, ikiwa mtu anahofia dalili zake, dalili ni kali sana, au zinadumu kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida, inashauriwa kumuona daktari.

Unapokuwa kwa daktari, utaulizwa maswali kuhusu dalili zako na kufanyiwa uchunguzi wa kimwili. Hii inaweza kujumuisha uchunguzi wa pua (anterior rhinoscopy), ambapo daktari hutumia kifaa maalum chenye mwanga kuchunguza pua na sinusi. Kupitia uchunguzi huu, daktari huweza kuthibitisha utambuzi wa sinusitis. Ikiwa dalili zinadumu kwa zaidi ya wiki 12, daktari ataweza kuthibitisha utambuzi wa sinusitis sugu.

Ikiwa sinusitis sugu itathibitishwa, vipimo vya ziada vinaweza kuhitajika ili kubaini aina gani ya sinusitis sugu. Hii inaweza kujumuisha kipimo cha endoscopy puani (nasal endoscopy), ambapo bomba lenye mwanga na kamera maalum huingizwa kwenye tundu la pua na sinusi kwa ajili ya uchunguzi. 8

Matibabu ya Sinusitis

Sinusitis ya muda mfupi na sinusitis sugu mara nyingi huitaji mbinu tofauti za matibabu.

Matibabu ya Sinusitis ya Muda Mfupi

Katika visa vingi, sinusitis ya muda mfupi haitahitaji matibabu maalum ya daktari. Kwa kuwa ugonjwa huu hupona wenyewe ndani ya wiki chache, mchanganyiko wa mbinu za kutunza afya na dawa za kununua kwenye  duka la dawa hutosha. Hii hujumuisha: 8 4

  • Dawa za maumivu: Dawa kama ibuprofen na paracetamol zinaweza kusaidia kupunguza maumivu.
  • Dawa za kupulizia puani (nasal sprays): Huweza kuleta ufanisi kwa muda mfupi katika kuzibua pua. Hata hivyo, haishauriwi kutumia kwa muda mrefu (zaidi ya siku 5 hadi 7).
  • Kunywa maji mengi na kupumzika vya kutosha: Hii hushauriwa ili kusaidia uponaji.
  • Kukanda uso kwa kitambaa cha vuguvugu: Hii huweza kusaidia kupunguza kujaa na kuziba kwa pua.

Ikiwa dalili ni kali sana, daktari anaweza kukuandikia:

  • Dawa za antibiotiki: Hizi huweza kupendekezwa katika visa nadra. Kwa kuwa sinusitis kali mara nyingi husababishwa na virusi, antibiotiki haziwezi kutumika kama tiba. Hata hivyo, zinaweza kutumika wakati dalili ni kali, wakati mtu ana tatizo la moyo, fibrosisi (cystic fibrosis), au mfumo dhaifu wa kinga, au wakati dalili zinazidi kuwa mbaya.
  • Dawa za steroidi za kupulizia puani (Steroidal nasal sprays): Unaweza kuandikiwa ili kusaidia kupunguza inflamesheni kali ya sinusi.

Matibabu ya Sinusitis sugu

Sinusitis sugu kwa kawaida huitaji uangalizi wa muda mrefu. Watu tofauti huitaji mbinu tofauti za matibabu kulingana na aina ya sinusitis, ukali wake, na ikiwa wanasumbuliwa na magonjwa mengine pia.

Matibabu ni pamoja na:

  • Mabadiliko ya mtindo wa maisha: Watu wenye sinusitis sugu wanaovuta sigara hupaswa kuacha, kwani moshi wa sigara unaweza kuzidisha hali hiyo. Aidha, watu wenye mizio inayochangia hali yao wanapaswa kuepuka kadiri iwezekanavyo vizua mzio. Hii inaweza kujumuisha kufanya mabadiliko ya kimazingira nyumbani au kazini.
  • Mchanganyiko wa saline (sodiumu kloridi na maji): Kuosha njia za puani kila siku kwa mchanganyiko huu huweza kusaidia kupunguza inflamesheni.
  • Dawa za steroidi za kupulizia puani: Dawa za kupulizia puani zenye steroidi zina ufanisi katika kupunguza inflamesheni. Madaktari kwa kawaida hupendekeza dozi, na muda wake wa matumizi utategemea ukali wa maambukizi husika. Ikiwa inflamesheni ni kali sana, daktari anaweza kukuandikia vidonge vya steroidi. Hata hivyo, vidonge hivi huwa kwa kawaida havitumiki sana kutokana na hatari ya madhara kama vile matatizo ya kupata usingizi na kupata chunusi.
  • Dawa za antibiotiki: Katika baadhi ya visa, sinusitis inaweza kutokana na maambukizi ya bakteria. Katika visa hivi, dawa za antibiotiki zinaweza kupendekezwa. Dozi yake kwa ujumla huitajika kuwa ndefu (wiki 3 hadi 4).
  • Dawa za kupunguza maumivu: Ikiwa dalili za sinusitis ya muda mfupi zinajitokeza wakati wa dalili za sinusitis sugu, dawa za kupunguza maumivu kama ibuprofen na paracetamol zinaweza kuwa na ufanisi katika kupunguza maumivu. Dawa za kupuliza za kupunguza pua kuziba pia zinaweza kuwa na ufanisi. Hata hivyo, dawa hizi za kupulizia puani hutoa tu nafuu ya muda mfupi na hazipaswi kutumiwa kwa zaidi ya siku 5 hadi 7 kwa wakati mmoja.

Upasuaji

Kwa kawaida, upasuaji hutumika kama chaguo la mwisho katika matibabu, lakini huweza kuwa muhimu katika baadhi ya visa. Hali zinazoweza kuhitaji upasuaji ni pamoja na:

  • Wakati matumizi ya dawa hayajaleta ufanisi
  • Kipimo cha CT (CT scan) kinaonyesha kuna viashiria vya ugonjwa sugu wa sinus
  • Polipsi (vivimbe) za pua hazitibiki
  • Katika visa vya maambukizi ya rhinosinusitis kutokana na mzio wa fangasi (ambayo kwa kawaida inajumuisha kuziba kabisa kwa sinus 1 au zaidi)
  • Katika hali mbaya ya kupinda kwa ukuta wa pua (septum deviation)

Upasuaji kwa ujumla una ufanisi katika kupunguza inflamesheni na kuondoa dalili kwa muda mfupi. Hata hivyo, hata baada ya upasuaji, sinusitis sugu kwa kawaida huitaji uangalizi wa kudumu, na kiini cha tatizo hilo kitahitaji kushughulikiwa.

Hitimisho

Maambukizi ya sinus (sinusitis) yanaweza kuathiri sana ubora wa maisha ya mtu, hususan ikiwa yatakuwa sugu. Ingawa njia nyingi za matibabu zinaweza kusaidia kupunguza dalili na kuzuia maambukizi ya mara kwa mara, ni muhimu kutafuta matibabu ya kitaalam ikiwa dalili zinaendelea au kuwa kali. Kwa kuzingatia utaratibu wa maisha wenye manufaa kiafya na kufuata ushauri wa daktari, watu wengi huweza kudhibiti athari za ugonjwa huu.

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Maambukizi ya Sinus ni nini?
J: Maambukizi ya sinus, pia hujulikana kama sinusitis au rhinosinusitis, ni inflamesheni ya sinus. Sinus ni vishimo vya hewa ndani ya mifupa ya uso na pua; sinusitis hutokea wakati vishimo hivi hupatwa na inflamesheni na kuziba, na kusababisha mkusanyiko wa kamasi na hewa.

S: Sinusitis ya muda mfupi hudumu kwa muda gani?
J: Sinusitis ya muda mfupi kwa kawaida hudumu kwa muda wa wiki 1 hadi 3. Hata hivyo, ni kawaida kwa ugonjwa huu kudumu kwa muda wa wiki 2 hadi 3.

S: Maumivu ya kichwa ya sinus hudumu kwa muda gani?
J: Maumivu ya kichwa yanayosababishwa na sinusitis yanaweza kudumu kwa muda wa siku chache hadi wiki 2 au 3, kulingana na ukali wa maambukizi na jinsi yanavyotibiwa.

S: Ni lini unapaswa kumuona daktari kwa maambukizi ya sinus?
J: Inashauriwa kutafuta matibabu ya daktari ikiwa dalili ni kali, zinazidi kuwa mbaya, au ikiwa unapata maambukizi ya sinus mara kwa mara.