1. Ada
 2. Magonjwa
 3. Maambukizi ya corona

Maambukizi ya corona

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Corona ni nini?

Ikiwa unahisi una COVID-19, unapaswa kupiga simu kabla ya kwenda kwa daktari au kitengo cha wagonjwa wa dharura. Utaongozwa kujua hatua muhimu zakufuata kwa ajili ya matibabu ya virusi vya corona katika eneo unaloishi.

COVID-19 ni maambukizi mapya ya virusi, yaliyoripotiwa kwa mara ya kwanza Desemba 2019 katika mji wa Wuhan, China. Virusi hivi vinaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia matone madogo ambayo mtu aliyeambukizwa hutoa pale anapokohoa au kupiga chafya. Wale waliokuwa karibu na mtu aliyeambukizwa wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu.

Dalili za corona

Dalili kuu ni pamoja na:

 • Homa
 • Kikohozi kikavu
 • Maumivu ya misuli na kutojihisi vizuri, ni miongoni mwa dalili kuu.

Pamoja na hayo kupungua kwa uwezo wa kunusa au kuonja, na dalili za mfumo wa kumeng'enya chakula, kama vile:

 • Kichefuchefu
 • Kutapika
 • Maumivu ya tumbo au kuharisha imetokea kwa baadhi ya watu. Dalili kali zaidi, kama vile shida ya kupumua, huweza pia kutokea.

Dalili za kupona corona zinategemeana na maendeleo ya dalili zilizopo na uchunguzi kupitia kipimo cha corona.

Ikiwa una mashaka kuwa inawezekana umeambukizwa corona, unaweza kufanya tathmini ya dalili bila malipo kwa kutumia app ya Ada wakati wowote. Tafadhali, kumbuka kuwa vipimo zaidi vitahitajika ili kufanya utambuzi wa COVID-19. Au pata maelezo zaidi kuhusu jinsi app yetu ya kukagua dalili inavyofanya kazi kabla ya kuijaribu.

Visababishi

Kwa kuwa hali hii inaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, wale waliokuwa na mawasiliano na mtu aliyeambukizwa wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi. Hali hii huweza kutokea katika umri wowote, na jinsia zote huathirika kwa usawa. Watu waliopata maambukizi ya COVID-19 awali huweza kuyapata tena.

Utambuzi wa corona

Watu wanapaswa kudhaniwa kuwa na ugonjwa wa corona ikiwa wanaonekana kuwa na dalili zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo, bado kuna ulazima wa kipimo cha corona kufanyika ili kudhibitisha uwepo wa virusi vya ugonjwa huu.

Matibabu

Dawa imeidhinishwa ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi makali, lakini bado haipatikani kila sehemu. Kwa hivyo, matibabu bado kwa kiwango kikubwa hujumuisha tiba ya kuusaidia mwili kupambana na dalili husika.

Sheria za afya huweza kutofautiana katika nchi tofauti. Katika baadhi ya maeneo, watu wasio na dalili kali huweza kushauriwa kukaa na kujitibu nyumbani. Katika maeneo mengine, watu hawa huweza kutengwa hospitalini. Watu wenye dalili kali huweza kuhitaji matibabu ya ziada.

Ubashiri

Watoto na vijana walioathirika mara nyingi huwa wana dalili zisizo kali na hupona vizuri. Tofauti na wazee ambao huweza kuhitaji matibabu zaidi. Zaidi ya hayo, madhara yanayoweza kuhatarisha maisha, kama vile moyo na mapufu kushindwa kufanya kazi, huweza kutokea kwa watu wenye umri wowote, hasa kwa wale wenye magonjwa mengine.

Kinga ya ugonjwa wa corona

Chanjo dhidi ya COVID-19 zimeidhinishwa. Hatari ya kupata madhara mabaya inapungua baada ya kupata chanjo kikamilifu. Kwa hivyo, inashauriwa kupata chanjo kamili au kupata nyongeza ya chanjo (booster) kulingana na mwongozo katika eneo unaloishi.

Hata hivyo, kuepuka kupata virusi hivi bado ni muhimu katika kuzuia maambukizi. Hivyo basi, pamoja na kudumisha vizuri usafii, unashauriwa kufanya yafuatayo:

 • Osha mikono mara kwa mara.
 • Vaa barakoa kwenye maeneo ya watu wengi ili kufunika mdomo na pua.
 • Epuka kukaa karibu na wagonjwa.
 • Kaa nyumbani wakati unaumwa, na
 • Epuka kusafiri katika maeneo yaliyoathirika ili kuweza kusaidia kupunguza usambazaji wa ugonjwa huu.

Uzingatiaji wa sheria za kujitenga na watu wengine (quarantine) katika nchi unayoishi pia ni muhimu.


Washirikishe wengine kwenye makala hii: