Mzunguko wa hedhi
Mzunguko wa hedhi ni nini?
Hedhi ni kipindi ambacho wanawake hutokwa na damu ukeni. Wanawake wengi hupata hedhi kila baada ya siku 28. Kwa baadhi ya wanawake hedhi hutokea baada ya siku chache zaidi au siku nyingi zaidi.
Umri wa kupevuka au maarufu wa "kuvunja ungo" hutofautiana baina ya mtu na mtu. Wasichana wengi huanza hedhi katika umri wa miaka 12. Wasichana wengine huanza katika umri mdogo zaidi na wengine katika umri mkubwa zaidi. 1
Mzunguko wa hedhi hutokea kwasababu ya mabadiliko ya homoni katika mwili wa mwanamke.
Dalili kabla ya hedhi
Dalili kabla ya hedhi ni mabadiliko mbalimbali ya kimwili na kihisia yanayoweza kutokea kwa mwanamke siku chache kabla ya kupata hedhi. Hali hii ni ya kawaida sana, na huwaathiri wanawake wengi katika hedhi kwa njia moja au nyingine.
Mabadiliko haya hujumuisha:
- Kuongezeka kwa hamu ya kula,
- Matiti kuuma yakiguswa,
- Mabadiliko ya hisia mara kwa mara,
- Kukasirika kirahisi,
- Hamu ya vyakula maalumu,
- Matatizo ya kupata usingizi,
- Kichefuchefu,
- Kuishiwa nguvu,
- Maumivu ya tumbo,
- Maumivu ya mgongo, na
- Chunusi. 2
Ukali wa dalili hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Dalili hizi huwa zinajirudia kwa namna zinazoweza kutabirika kabla ya hedhi.
Matibabu hujumuisha kudhibiti dalili. Hii inaweza kuwa kwa kufanya mabadiliko ya mienendo ya maisha au kwa kutumia dawa. Kufanya mazoezi mara kwa mara, kuwa na mtandao mzuri wa msaada na kujifunza njia za kupumzika huweza kusaidia kupunguza dalili. 3
Maumivu wakati wa hedhi
Maumivu wakati wa hedhi, au kwa kitaalamu "dysmenorrhea," ni tatizo la kawaida, na linawaathiri karibia wanawake wote wakati fulani wa maisha yao. Watu wenye hali hii mara nyingi hupata dalili za kwanza wanapoanza kupata hedhi. Licha ya maumivu ya tumbo na sehemu ya chini ya mgongo, baadhi ya watu wenye hali hii wanaweza kupata maumivu ya kichwa, tumbo kujaa gesi na kuharisha siku chache kabla ya au wakati wa hedhi.
Hakuna kipimo maalum cha hali hii, lakini vipimo vya damu na ultrasound huweza kuhitajika kuhakikisha hamna ugonjwa mwingine unaosababisha dalili hizi.
Kuna aina tofauti za matibabu; ya kawaida ni kutumia dawa za maumivu kama inahitajika, au kutumia vidonge vya majira. Wanawake wengi huona kuwa wanaweza kuwa na udhibiti mzuri wa dalili zao. Maumivu yanapokuwa makali, mtu hushauriwa kumuona mtaalamu wa afya kwa matibabu zaidi. 4
Kukoma hedhi
Kukoma hedhi ni kipindi ambacho mwanamke huacha kupata siku zake. Hii hutokea kwa kawaida kati ya umri wa miaka 45 na 55. Kukoma hedhi huanza taratibu, na hii huweza kuonekana kwa kupungua kwa siku za hedhi hadi kutopata hedhi hedhi kabisa.
Wakati wa Kipindi cha kukoma hedhi wanawake huweza kupata dalili mbalimbali, ikiwemo:
- Kutokwa jasho kwa wingi,
- Kichwa kuuma,
- Kukosa usingizi, na
- Kukosa hamu ya kujamiiana. 5
Udhaifu wa mifupa pia huweza kutokea kwa wanawake katika kipindi hiki. Hali hii huweza kusababisha mifupa kuvunjika kirahisi hata baada ya kupata jeraha dogo. 6
NHS. 2022. Periods. Accessed Sept 7th 2022.
AMBOSS. 2022. Menstrual Cycle and Menstrual cycle abnormalities. Accessed Sept 7th 2022.
NHS. 2021. (Premenstrual Syndrome). Accessed Sept 7th 2022.
Acog.org (2022). Dysmenorrhea: Painful periods. Accessed Sept 7th 2022.
AMBOSS. 2022. Menopause. Accessed Sept 7th 2022.
Mary Jane Minkin. 2019 Menopause: Hormones, Lifestyle and Optimizing Aging. Accessed Sept 7th 2022.