1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Virusi vya UKIMWI (HIV)

Virusi vya UKIMWI (HIV)

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

VVU ni nini?

Maambukizi ya awali ya VVU (HIV), ni hali inayotokea wiki mbili hadi nne baada ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI (VVU). Hii pia hujulikana kama maambukizi ya awali ya VVU.

VVU hushambulia seli za kinga za mwili, ambazo hupambana na maambukizi. Dalili zinafanana na maambukizi mengine ya virusi, kama vile mafua au homa. Kwa sababu hii, watu wengi hawatambui kuwa wamepata maambukizi. Kipimo cha damu ni njia bora ya kuthibitisha maambukizi ya VVU.

Ikiwa umetambuliwa kuwa na VVU, ni muhimu kuanza matibabu haraka iwezekanavyo. Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia kuzuia virusi kuharibu mfumo wako wa kinga na kusababisha matatizo makubwa ya kiafya. Kuna dawa kadhaa za ARV (antiretroviral), na daktari anaweza kutoa ushauri wa dawa itakayokufaa zaidi. Kwa matibabu, inawezekana kudhibiti VVU na kuishi maisha marefu yenye afya.

Je, mtu anayetumia ARV anaweza kuambukiza wengine? Watu walio na VVU wanaotumia ARV na kudumisha kiwango cha virusi kisichoweza kugundulika hawana hatari ya kusambaza VVU kwa kujamiiana na wenzi wao wasio na VVU. 1

Vihatarishi vya Virusi vya UKIMWI (HIV)

Virusi vya UKIMWI (Ukosefu wa kinga mwilini) husambazwa kwa kugusa damu, shahawa au majimaji ya ukeni yenye maambukizi. Wanawake wenye VVU wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au mara chache sana, wakati wa kunyonyesha.

VVU inaweza kuwaathiri watu wenye umri wowote, jinsia au rangi. Baadhi ya tabia, kama vile kutumia sindano zilizotumiwa na wengine na kutotumia kinga wakati wa kujamiiana, huweza kuongeza uwezekano wa kupata virusi hivi. Kumgusa mtu, kama vile kumshika mkono, kumbusu au kumkumbatia, hakuwezi kusambaza virusi vya UKIMWI.

Dalili za UKIMWI (HIV symptoms)

Dalili za kawaida hufanana na dalili za maambukizi mengine ya virusi kama vile homa ya mafua na huweza kujumuisha: 2

Dalili nyingine ni pamoja na:

  • Upele mwekundu
  • Kutokwa jasho usiku
  • Kupoteza hamu ya kula
  • kupungua uzito

Dalili hizo nyingine hutokea ndani ya siku 30 baada ya kuambukizwa virusi, na huweza kudumu kwa wiki kadhaa. Watu wengi walioambukizwa VVU hawana dalili zozote, au wanaweza kuwa na dalili zisizo kali na zisizo leta madhara.

Utambuzi

Je, virusi vya ukimwi huonekana baada ya muda gani? Kupima VVU ni njia pekee ya kuthibitisha utambuzi. Hivyo basi, mtu yeyote anayeshuku kuwa ameambukizwa virusi anapaswa kupimwa haraka iwezekanavyo kwa ajili ya utambuzi. 3 Inaweza kuwa vigumu kuthibitisha utambuzi katika hatua za mwanzo za maambukizi, kwa sababu kipimo hutambua vigangamwili (protini zinazopambana na maambukizi) vya VVU ambavyo huzalishwa wiki au miezi baada ya maambukizi ya awali.

Kwa sababu hii, daktari anaweza kupendekeza tena kipimo cha ukimwi, ikiwa kipimo cha kwanza kimefanywa muda mfupi baada ya kuambukizwa virusi.

Matibabu ya UKIMWI

VVU hutibiwa na dawa maalum dhidi ya virusi vya UKIMWI. Dawa hizi wakati mwingine, lakini sio lazima, huanzishwa wakati wa maambukizi ya awali.

Watu wenye VVU wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa mengine, kwahiyo wanaweza kunufaika na mienendo mizuri ya maisha kama vile kuwa na lishe bora, kutumia kinga wakati wa kujamiiana na kupunguza msongo wa mawazo. Hali hii mara nyingi ina athari kubwa ya kihisia na kisaikolojia. Hivyo basi, ushauri na msaada wa kijamii vinapaswa kuwa sehemu ya matibabu.

Kinga dhidi ya UKIMWI

Kutumia kinga wakati wa kujamiiana, matumizi salama ya sindano (ikiwa ni pamoja na watu katika kazi fulani, kama wauguzi na wachora ngozi (tattoo)) na kutambuliwa mapema ni hatua zinazosaidia kuzuia maambukizi ya VVU na kuzuia kusambaza virusi kwa watu wengine.

Ubashiri

Ingawa hamna tiba ya VVU, watu wengi wanaishi maisha mazuri kwa msaada wa dawa dhidi ya virusi vya ukimwi. Watu ambao hali hii haijatambuliwa mapema huweza kupata udhaifu wa mfumo wa kinga, na wana uwezekano mkubwa wa kusambaza virusi kwa wengine, na hatimaye wanaweza kupata UKIMWI.