Ugonjwa wa malaria
Malaria ni moja ya changamoto kubwa za kiafya ambazo dunia inakabiliana nazo hivi sasa. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), watu 409,000 walikufa kutokana na ugonjwa huu mwaka 2019, na takriban watu milioni 229 wameambukizwa hivi karibuni.1 Na haya yote ni pamoja na ukweli kwamba ugonjwa wa malaria unatibika na unaweza kuzuilika.
Ikiwa unaishi au unapanga kutembelea maeneo ambayo yana tishio kubwa la malaria, kuelewa ugonjwa huu kunaweza kukusaidia kuitunza afya yako.
Hivyo basi, embu tujifunze zaidi kuhusu malaria, dalili zake, na kupata vidokezo kadhaa kuhusu jinsi unavyoweza kujikinga wewe na wapendwa wako.
Malaria inaambukizwaje?
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na kimelea kiitwacho Plasmodium. Aina 5 tofauti za Plasmodium zinaweza kusababisha malaria, na kwa kawaida kimelea hiki husambazwa miongoni mwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anofelesi.2 Wakati mbu hawa wanapomng’ata mtu aliye na malaria, huchukua vimelea vya Plasmodium. Halafu wanaweza kusambaza vimelea hivyo wanapomng’ata mtu mwingine baadaye.3 Kwa kuwa malaria huambukizwa kupitia damu kutoka mtu mmoja kwenda mwingine, inaweza pia kuenea kupitia kuongezewa damu iliyoambukizwa malaria, upandikizaji wa kiungo, na kutumia sindano na mtu mwingine aliyeambukizwa.3
Vimelea vya malaria hupata taabu kuishi maeneo yenye baridi zaidi duniani.3 Ndiyo maana kwenye nchi za Kiafrika, ambako hali ya hewa kwa kawaida ni ya kitropiki, hutoa mazingira mazuri kwa Plasmodium kuishi na kuzaliana kwa muda wa mwaka mzima. Mwaka 2019, nchi za Nigeria, Kongo, Tanzania, Msumbiji, Niger, na Burkina Faso zilikuwa na idadi ya 51% ya vifo duniani vitokanavyo na malaria.1 Hata hivyo, siyo maeneo yote katika nchi zilizoathirika na malaria yenye tishio sawa la maambukizi ya malaria. Kwa mfano, ikiwa unaishi au kutembelea wilaya ya Rufiji nchini Tanzania, unapaswa kujua kwamba ni mojawapo ya maeneo yenye hatari kubwa ya maambukizi ya malaria. Mwaka 2017, wilaya hii ilikuwa na viwango vya maambukizi ya 14% - karibu mara mbili ya wastani wa maambukizi kitaifa.4
Malaria ni ugonjwa hatari. Lakini madaktari wanaweza kuutibu kupitia dawa za malaria wanazopendekeza ambazo huua vimelea vya Plasmodium.3 Kwa kupata matibabu ya haraka, inawezekana kupona kabisa malaria. Kwahiyo, ni muhimu kufahamu ni dalili gani za kuzingatia na wakati gani unapaswa kwenda kwa daktari.
Dalili ni zipi?
Dalili za malaria zinaweza kuanza kujitokeza siku 7 baada ya kuambukizwa. Dalili za awali ambazo ni kawaida kujitokeza ni pamoja na:2
- Homa
- Kutetemeka
- Maumivu ya kichwa
- Kichefuchefu
- Kutapika
- Maumivu ya misuli
- Kuharisha
Dalili kali zaidi zinaweza kujumuisha:2
- Figo kushindwa kufanya kazi ghafla
- Mapafu kujaa maji
- Kifafa
- Mzunguko hafifu wa damu mwilini
Kuna magonjwa kadhaa yenye dalili zinazofanana na dalili za malaria. Hii inaweza kusababisha kuwa vigumu kwa madaktari kufanya utambuzi wa malaria.2 Hivyo basi, njia nzuri kuliko zote ya utambuzi wa ugonjwa wa malaria ni kwa daktari kuchunguza damu yako kwa hadubini (microscope).3
Ikiwa unahisi unaweza kuwa na malaria, unapaswa kwenda kwa daktari mara moja. Kwa kufanya hivyo, utafanyiwa vipimo ili uweze kuanza matibabu haraka iwezekanavyo kabla ya dalili zako kuwa mbaya zaidi.3
Naweza kufanya nini ili kujilinda mimi na familia yangu?
Ufahamu mwongozo wa kujikinga na malaria kutoka Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC). Mwongozo huu unaweza kuwa na manufaa kwa wageni wanaotembelea nchi au maeneo yenye tishio kubwa la malaria na pia unaweza kuwa na manufaa kwa wale ambao tayari wanaishi katika nchi au maeneo hayo:3
- Kunywa dawa za kuzuia malaria kabla kusafiri katika maeneo yenye tishio kubwa la ugonjwa huu.
- Ongea na daktari kuhusu kubeba dawa za kutibu malaria wakati wa safari yako ili kuhakikisha unakuwa na akiba ya dawa hizo iwapo utazihitaji.
- Ikiwa utaugua ndani ya mwaka 1 baada ya kurudi kutoka safarini, mwambie daktari kuhusu safari hiyo na uombe kupimwa malaria.
- Tumia dawa ya kuua mbu, haswa wakati wa usiku.
- Vaa shati la mikono mirefu wakati wa usiku, au lala kwenye kitanda chenye chandarua kilichopakwa dawa ya kuua mbu.
Uchaguaji wa dawa sahihi ya kuzuia malaria unaweza kutegemea mipango yako ya safari, historia ya afya, umri, mizio, na hali ya ujauzito.3 Kwahiyo hakikisha unazungumza na daktari kabla ya kutumia dawa yoyote ya kuzuia malaria.
Je, kuna chanjo ya malaria?
WHO inapendekeza chanjo mpya ya malaria ya RTS, S kwa watoto wanaoishi katika maeneo hatarishi. Tafiti zimeonyesha kuwa chanjo hii inaweza kupunguza hatari ya malaria kali kwa watoto wadogo kwa 30% na kiwango chake cha usalama ni kizuri.5 Chanjo hii inaweza kuwa ni hatua nyingine muhimu katika mapambano dhidi ya malaria kwa nchi kama Tanzania na nyingine zinazokabiliwa na changamoto ya ugonjwa huu.
Kwa kuelewa dalili za malaria na kujua wakati wa kumuona daktari, unaweza kujikinga wewe na familia yako dhidi ya malaria.
WHO. “World Malaria Report 2020: 20 Years of Global Progress and Challenges.” Kimetumika tarehe 28 Oktoba 2021.
WHO. “Malaria.” Kimetumika tarehe 9 Novemba 2021.
CDC. “Frequently Asked Questions (FAQs).” Kimetumika tarehe 9 Novemba 2021.
WHO. “Tanzania Intensifies Malaria Fight in Hotspots.” Kimetumika tarehe 7 Desemba 2021.
WHO. “WHO Recommends Groundbreaking Malaria Vaccine for Children at Risk.” Kimetumika tarehe 10 Novemba 2021.