1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Malaria

Malaria

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Malaria ni nini?

Malaria ni ugonjwa hatari ambao mara nyingi sana hutokea katika maeneo ya kitropiki na yanayozunguka tropiki tu. Ugonjwa huu unasababishwa na maambukizi ya vimelea vinavyoitwa Plasmodium, ambavyo husambazwa kwa kung’atwa na mbu jike wanaobeba vimelea hivi. 1

Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2016 lilisema kuwa takribani nusu ya idadi ya watu wote duniani walikuwa hatarini. 2Matukio mengi ya malaria hutokea kwa wale wanaoishi au waliotembelea maeneo ya kusini mwa jangwa la Sahara au Asia ya Kusini-Mashariki. Hata hivyo, Mashariki mwa Mediterania, Oceania (pasifiki), na Amerikas pia ni maeneo hatari.

Nchini Marekani, Kitengo cha Kudhibiti na Kuzuia magonjwa (CDC) kinaripoti takribani visa 1700 vya malaria kila mwaka. 3

Dalili kuu za malaria ni homa na ugonjwa unaofanana na mafua. Ikiwa mtu anapata dalili za malaria baada ya kusafiri katika eneo lililoathirika (angalia ramani ya maeneo yaliyoathirika, anapaswa kuongea na daktari haraka iwezekanavyo.

Malaria isipotibiwa, inaweza kusababisha madhara mabaya sana, na kusababisha matokeo mabaya pamoja na uwezekano mkubwa wa kufa. Hata hivyo, matokeo huwa ni mazuri ikiwa malaria inatambuliwa mapema na kutibiwa jinsi ipasavyo.

Malaria kwa kawaida inaweza kuzuilika kwa kutumia dawa dhidi ya malaria pale mtu anapotembelea maeneo yenye ugonjwa huu. Dawa ya mbu na vyandarua vinapaswa kutumiwa usiku, kwa kuwa mbu kawaida hung’ata na kusambaza malaria nyakati za usiku.

Dalili kwa kawaida hutokea ndani ya wiki kadhaa baada ya kuambukizwa, lakini wakati mwingine huweza kuchukua muda mrefu zaidi. Kipindi hiki huweza kutofautiana, kulingana na mtu aliyeambukizwa na aina halisi ya vimelea vya malaria. Kwa hivyo ugonjwa wa malaria unapaswa kuchunguzwa kama kisababishi kinachowezekana kwa visa vyote vya homa ndani ya mwaka mmoja baada ya kutembelea eneo lenye malaria.

Dalili

Dalili za malaria kawaida hutokea ndani ya wiki chache baada ya kuambukizwa, ingawa ikiwa mtu ameshawahi kuugua malaria au ana kinga dhidi ya malaria hizi huweza kuathiri dalili na muda ambao zinaweza kuchukua kujitokeza. Katika baadhi ya matukio, kimelea hiki kinaweza kukaa mwilini na kutosababisha dalili zozote kwa miezi mingi, hata hadi mwaka mmoja baada ya kusafiri kwenye eneo lenye malaria.

Dalili kuu za malaria

Dalili za malaria kwa kawaida hujumuisha: 4

  • Vipindi vya homa kali sana
  • Kutetemeka
  • Kutokwa jasho

Shambulio la ghafla (paroxysms) – kujirudia ghafla au shambulio la homa, kutetemeka na kutokwa jasho kwa pamoja - hutokea kila baada ya masaa 24, 48 au 72, kulingana na aina halisi ya kimelea cha malaria. Kila shambulio hudumu takribani saa moja au masaa wawili na hutokea katika hatua tatu zinazofuatana. Hatua ya kwanza ni kutetemeka na kuhisi baridi. Hii hufuatwa na homa kali sana. Baada ya mgonjwa kutokwa jasho jingi kuliko kawaida, joto la mwili hurudi katika kiwango cha kawaida au hata kiwango chini ya kawaida. Wakati mwingine, katika maambukizi ya awali, wagonjwa huwa hawapati hali hii, lakini huwa wana vipindi vya homa wakati wa mchana.

Dalili nadra za malaria

Katika baadhi ya matukio, mtu anaweza kupata: 5

  • Maumivu ya tumbo
  • Uchovu, yaani kukosa usingizi au kuduwaa na kutojishughulisha
  • Kichefuchefu
  • Kutapika
  • Kuharisha, hasa kwa watoto
  • Upungufu wa damu
  • Manjano
  • Ugumu wa kupumua
  • Kupoteza hamu ya kula

Madhara ya malaria yanayoweza kuhatarisha maisha huweza kutokea ikiwa malaria haijatibiwa au imesababishwa na Plasmodium falciparum. Madhara haya hujumuisha matatizo ya kupumua, ini na figo kushindwa kufanya kazi, pamoja na matatizo ya ubongo na mfumo wa neva.

Mara nyingi, maumivu ya tumbo hutokea ndani ya wiki ya kwanza au ya pili ya kuumwa malaria. Hii mara nyingi husababishwa na inflamesheni ya ini na wengu. Idadi kubwa ya seli nyekundu za damu hufichwa kwenye ini na wengu, pamoja na kwenye viungo vingine vikuu. Ikiwa wengu linaongezeka ukubwa, linaweza kupasuka na kusababisha kuvuja damu nyingi sana ndani ya tumbo, hali ambayo huhitaji matibabu ya dharura. 6

Visababishi

Malaria kwa binadamu husababishwa na kimelea kinachojulikana kama Plasmodium, hususani aina ya P. falciparum, P. malariae, P. ovale, P. vivax na P. knowlesi, ambacho husambazwa kwa kung’atwa na mbu aliyeambukizwa. Kung’atwa mara moja tu na mbu aliyeambukizwa huweza kusababisha malaria.

Mbu jike wa Anopheles pekee ndio anaweza kusambaza malaria. Mbu anapomng’ata mtu aliyeambukizwa, anachukua kiwango kidogo cha damu chenye vimelea vya malaria visivyoweza kuonekana kwa macho. Wiki moja baadaye, mbu anaponyonya damu tena, vimelea hivi hujichanganya na mate ya mbu na huingia ndani ya mtu anayeng’atwa.

Sio kila wakati mbu wenye maambukizi anapomng’ata mtu, mtu huyo atapata malaria. Idadi ya vimelea ambavyo mbu anabeba huathiri uwezekano wa mtu kupata maambukizi ya malaria. Baadhi ya mbu huweza kuwa na idadi kubwa ya vimelea, na kuwafanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kuusambaza ugonjwa huu. 7

Malaria iliyosambazwa na mbu pia hutegemea mambo fulani ya hali ya hewa, kama vile joto na unyevu wa kutosha unaomwezesha mbu wa Anopheles kuzaana na kuishi. Hii ndo sababu malaria hutokea kwenye maeneo ya tropiki.

Hali ya hewa ya joto pia huchochea tabia za binadamu zinazoweza kuongeza uwezekano wao wa kung’atwa na mbu kati ya mida ya jioni na alfajiri, mida ambayo mbu wanaosababisha malaria hung’ata watu zaidi. Mifano hujumuisha shughuli za nje kama vile camping, kulala nje na pia kuvaa nguo nyepesi na fupi zinazosababisha ngozi nyingi zaidi kuwa wazi na katika hatari ya kung’atwa na mbu.

Mara chache sana, malaria huweza kusambazwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine, bila ya mbu kuhusika. Hii huweza kutokea kupitia damu tu, kwa mfano katika matukio yafuatayo:

  • Kupandikizwa kiungo
  • Kuongezewa damu
  • Kutumia sindano na mtu mwingine
  • Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wake ambaye bado hajazaliwa

Visa vya malaria kutokana na kuongezewa damu iliyoambukizwa ni nadra sana. 8

Aina za malaria

Kila aina ya malaria hutofautiana katika muda wa dalili kutokea baada ya kung’atwa na mbu. Vimelea huweza kubakia, kukua na kuongezeka kwenye seli za ini kwa miezi kabla havijaingia kwenye seli nyekundu za damu. Hii hutambulika kitaalamu kama “incubation period” (kipindi kati ya kuambukizwa na dalili kutokea).

Punde tu vimelea vya malaria vinapoingia kwenye damu, vinatofautiana katika urefu wa mzunguko wa kujigawanya, ambapo vimelea vipya hutoka nje ya seli nyekundu za damu. Hii husababisha vipindi vya homa, vinavyojulikana kama mzunguko wa homa.

Baadhi ya aina za Plasmodium huweza kusababisha maambukizi kujirudia, kwa sababu vimelea hujificha kwenye ini na baada ya miezi au miaka kadhaa ya mtu kung’atwa huingia kwenye damu na kusababisha maambukizi kujirudia.

Malaria hugawanywa katika aina mbili kuu: malaria isiyo kali (benign malaria) na malaria inayoweza kuhatarisha maisha (malignant malaria). Malaria isiyo kali kwa kawaida haina dalili kali na ni rahisi kutibu.

Aina tano za vimelea vya Plasmodium vinavyoweza kusababisha malaria kwa binadamu ni:

  1. P. falciparum: Hii ni aina ya malaria inayoweza kuhatarisha maisha (malignant malaria) na huweza kuwa mbaya sana, na wakati mwingine kusababisha kifo. Kwa kawaida dalili hutokea baada ya takribani siku 7 hadi 14, lakini huweza kutokea hadi hata baada ya mwaka. Mwanzoni mzunguko wa homa unaweza usitabirike na homa hutokea kila siku. Baada ya wiki moja homa hujirudia kila siku ya 3. Maambukizi ya aina hii ya malaria hayawezi kujirudia.
  2. P. Vivax: Hii ni aina ya malaria isiyohatarisha maisha. Kwa kawaida dalili hutokea baada ya takribani siku 12 hadi 17, na hujumuisha homa inayojirudia kila siku ya tatu. Aina hii ya malaria huweza kusababisha maambukizi kujirudia.
  3. P. ovale: Hii ni aina ya malaria isiyohatarisha maisha. Kwa kawaida dalili hutokea baada ya takribani siku 15 hadi 18, na hujumuisha homa inayojirudia kila siku ya 3. Aina hii ya malaria huweza kusababisha maambukizi kujirudia.
  4. P. malariae: Hii ni aina ya malaria isiyohatarisha maisha. Kwa kawaida dalili hutokea baada ya takribani siku 18 hadi 40, na hujumuisha na homa inayojirudia kila siku ya nne. Isipotibiwa, vimelea huweza kukaa mwilini na kusababisha dalili kwa miaka mingi.
  5. P. knowlesi: Hii ni aina ya malaria inayoweza kuhatarisha maisha (malignant malaria) na huweza kuwa mbaya sana, na wakati mwingine kusababisha umauti. Kwa kawaida dalili hutokea takribani baada ya siku 9 hadi 12, na hujumuisha homa inayojirudia kila siku. Maambukizi ya aina hii ya malaria hayawezi kujirudia.
  6. Ni vizuri kujua: Plasmodium knowlesi mara nyingi huchanganywa na Plasmodium malariae inapochunguzwa kwenye darubini. Hata hivyo, inaweza kuwa mbaya zaidi, na wakati mwingine inaweza kusababisha malaria inayoweza kuhatarisha maisha, na yenye uwezekano mkubwa wa kusababisha kifo. 9

Utambuzi

Kwa kuwa hamna dalili maalum za ugonjwa huu, ni muhimu kwa mtu kumuona daktari na kueleza uwezekano wa kuwa na malaria ikiwa anapata homa ndani ya mwaka baada ya kutembelea eneo lililoathirika na malaria.

Maambukizi mengine yanaweza kuwa na dalili kama za malaria, kama vile homa ya matumbo (typhoid), VVU, homa ya dengue, homa ya uti wa mgongo au homa kutokana na virusi zinazosababisha utokwaji damu (viral hemorrhagic fevers), kutokana na mishipa ya damu kupasuka. Mara nyingi maambukizi ya malaria hutambuliwa kimakosa kama maambukizi ya virusi, homa ya mafua, maambukizi ya tumbo (gastroenteritis) au homa ya ini. Jaribu app ya Ada kufanya tathmini ya dalili bure. Au pata maelezo zaidi kuhusu jinsi app yetu ya kukagua dalili inavyofanya kazi kabla ya kuijaribu.

Kwa kawaida, daktari huchunguza historia ya mtu na huuliza kuhusu kusafiri katika maeneo ya kitropiki. Uchunguzi wa kimwili pia huweza kufanywa ili kuchunguza kama wengu au ini limeongezeka ukubwa.

Kipimo cha damu huweza kufanywa ili kuthibitisha utambuzi. Baada ya uchunguzi wa maabara, sampuli ya damu huweza kuonyesha:

  • Ikiwa kuna malaria
  • Aina ya malaria iliyopo
  • Ikiwa maambukizi yamesababishwa na aina ya vimelea ambavyo dawa fulani hushindwa kuviua
  • Ikiwa maambukizi yamesababisha upungufu wa damu
  • Ikiwa maambukizi yameathiri viungo vyovyote muhimu

Utambuzi sahihi wa malaria na aina halisi ya maambukizi ya Plasmodium ni muhimu:

  • Ili kuhakikisha matibabu sahihi kwa matokeo mazuri
  • Kutokana na hofu ya ongezeko la malaria isiyoweza kutibiwa na dawa (drug-resistance), ambayo imeenea kwenye maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huu.

Wakati mwingine malaria huchukua muda kuonekana kwenye kipimo cha damu. Hii hutokea zaidi kwa watu wajawazito, ambapo idadi kubwa ya vimelea huweza kuwepo kwenye kondo la uzazi, bila kuwepo katika sehemu nyingine za mwili. 10 Ikiwa malaria haionekani kwenye kipimo cha damu, kipimo kingine kinaweza kufanywa siku kadhaa baadaye.

Matibabu

Inawezekana kutibu malaria nyumbani ikiwa dalili sio kali. Lakini, ikiwa maambukizi yamesababishwa na Plasmodium falciparum, au ikiwa kuna madhara zaidi, mtu kwa kawaida anahitaji kutibiwa na kuwa chini ya uangalizi hospitalini.

Ikiwa malaria inatambuliwa na kutibiwa haraka, watu wengi hupona vizuri. Hata hivyo, matibabu huweza kumfanya mtu ahisi udhaifu na uchovu kwa wiki kadhaa baada ya maambukizi kuisha.

Kuna aina tofauti za dawa za malaria. Dawa itakayopendekezwa hutegemea:

  • Aina halisi ya plasmodium inayosababisha malaria
  • Ikiwa dawa za malaria zimetumiwa wakati wa kusafiri
  • Ukali wa dalili

Zaidi ya dawa moja, au mbadala, huweza kupendekezwa ikiwa mtu anapata madhara kutokana na dawa, au ikiwa dawa hiyo haina athari yoyote kwa kimelea halisi.

Dawa nyingi zinazotumika kuzuia malaria pia huweza kutumika kutibu malaria. Hata hivyo, ikiwa umetumia dawa fulani kuzuia malaria, inashauriwa usitumie dawa hiyo hiyo kutibu malaria.

Aina fulani za malaria, kama vile Plasmodium vivax na Plasmodium ovale, zina hatua kwenye mzunguko wa maisha ya malaria ambapo vimelea hivi huweza kuishi kwenye ini kwa miezi kadhaa, hata miaka, na kujitokeza baadaye, na kusababisha malaria kutokea tena. Ikiwa mtu anatambulika kuwa na moja ya aina hizi za malaria, kwa kawaida atapewa dawa za kuzuia maambukizi kujirudia.

Inawezekana kupata dawa za dharura ambazo mtu anaweza kubeba ikiwa anaenda vijijini na kutumia dawa hizi kujitibu ikiwa inashukiwa ana malaria hadi pale huduma za afya zitakapopatikana.

Kinga

Profilaksisi ya malaria (malaria prophylaxis) ni semi ya kitaalamu ya matibabu ya kuzuia maambukizi ya malaria. Njia kuu za kuzuia malaria ni kwa kutumia dawa za malaria, kitaalamu hii hujulikana kama “Chemoprophylaxis”, na kuepuka kung’atwa na mbu.

Kwa sasa hamna chanjo ya malaria, ingawa jitihada za kutengeneza chanjo tofauti bado zinaendelea.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kanuni tano, zinazojulikana kama ABCDE za kuzuia malaria: 11

  • Awareness (Ufahamu). Unaposafiri kwenda kwenye eneo lenye malaria, fahamu hatari ya kupata malaria, muda unaochukua dalili za malaria kutokea, na uwezekano wa dalili hizi kuchelewa kutokea pamoja na dalili kuu.
  • Bite prevention (Kuzuia kung’atwa). Kutumia dawa ya mbu yenye ufanisi, kama vile diethyltoluamide (DEET), na vyandarua wakati wa kulala.
  • Chemoprophylaxis (Kutumia dawa kuzuia maambukizi). Tumia dawa dhidi ya malaria ikiwa zinahitajika, kuanzia wiki mbili kabla ya kuingia kwenye eneo lenye malaria na kufuata dozi ya dawa ya kila siku au kila wiki.
  • Diagnosis (Utambuzi). Inapaswa kufanyiwa utambuzi na kupata matibabu ikiwa homa inatokea wiki moja au zaidi baada ya kufika kwenye eneo linalojulikana kuwa na malaria na hadi miezi mitatu au hata zaidi baada ya kuondoka kwenye eneo hili, ingawa ni nadra sana kwa dalili kutokea baada ya miezi mitatu.
  • Environments (Mazingira). Epuka kuwa ndani ya au karibu na maeneo ambayo mbu huzaliana, kama vile mabwawa, haswa katika mida ya jioni na usiku.

Mara nyingi sana, wasafiri hupata malaria kutokana na kutotumia dawa zao kwa usahihi, aidha kwa sababu wamekosa baadhi ya dozi au dawa hazijatumika kwa muda ulioshauriwa kabla na baada ya kuondoka kwenye eneo lenye malaria.

Dawa za kuzuia kupata malaria kwa kawaida hazina madhara, lakini kwa baadhi ya watu madhara huweza kutokea. Madhara yanayotokea sana kutokana na dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu na kuharisha. Baadhi za dawa dhidi ya malaria huweza kuongeza athari ya mionzi ya jua, kwa hiyo ni muhimu kutumia mafuta ya kujikinga dhidi ya mionzi ya jua, wakati kwa wengine wanaweza kupata matatizo ya kulala na maumivu ya kichwa.

Dawa dhidi ya malaria sio wakati wote zina ufanisi wa asilimia 100, ndio maana ni muhimu kuwa na tabia ya kujikinga dhidi ya kung’atwa na mbu ukiwa kwenye eneo lenye malaria. Diethyltoluamide (DEET) ni kati ya dawa ya mbu yenye ufanisi zaidi, na ikiwa dawa hii ina kati ya 10% hadi 30% ya DEET inaweza kutumika kwa watoto wachanga na watoto wenye umri zaidi ya miezi miwili, na wakati wa kunyonyesha. 12 Kwa watu wazima, viwango vikubwa vya DEET vinaweza kuzuia mbu kwa muda mrefu zaidi. Hata hivyo, viwango vinavyozidi 50% haviongezi kinga ya ziada. 13

Tabia nyingine zinazoweza kupunguza hatari ya mtu kung’atwa hujumuisha:

  • Kutumia vyandarua wakati wa kulala, haswa vile vyenye dawa za mbu, na kuhakikisha havina matobo.
  • Kujifunika vizuri ikiwa upo nje usiku.
  • Kalala kwenye chumba chenye kiyoyozi, kwa kuwa baridi hupunguza mbu.
  • Kuweka nyavu kwenye milango, madirisha na maeneo mengine ambayo mbu huweza kuingia ndani.
  • Kupulizia dawa ya mbu kabla ya kulala ili kuua mbu wowote walioingia chumbani wakati wa mchana.
  • Kutumia kifaa kinachotumia umeme kuyeyusha kidonge chenye pyrethroid na kutengeneza mvuke chumbani wakati wa usiku.

Vizuri kujua: Tiba ya mitishamba na homeopathi hazijaonyesha ufanisi katika kuzuia au kutibu malaria na hazishauriwi.

FAQs

S: Je malaria inaweza kuambukizwa?
J: Hapana, malaria haisambazwi kwa njia sawa kama mafua, kwa kuwa vimelea vya malaria havipatikani kwenye mate ya mtu. Pia haiwezi kusambazwa kwa kujamiiana. Njia pekee ambayo malaria inaweza kusambazwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine ni kupitia damu, kwa kuongezewa damu, kupandikizwa viungo, kutumia sindano moja na mtu mwigine au mama kumambukiza mtoto wake akiwa tumboni. Vinginevyo, malaria kwa kawaida husambazwa kwa kung’atwa na mbu jike aina ya Anopheles, aliyeambukizwa kwa kunyonya damu kutoka mtu mwenye malaria.

S: Je, kuna chanjo dhidi ya malaria?
J: Chanjo ya kwanza ya malaria duniani, inayojulikana kama RTS,S, inafanyiwa majaribio Ghana, Kenya na Malawi, kuanzia mwaka 2018. Hata hivyo, haipatikani kwa sasa. Licha ya miaka mingi ya utafiti, kwa sasa hamna chanjo ya malaria inayotumika kwa uuma. Utata wa kimelea cha malaria, Plasmodium, hufanya iwe vigumu kuitengeneza chanjo ya malaria.

S: Je, mtu anaweza kupata kinga dhidi ya malaria kutokana na kupata maambukizi ya malaria?
J: Baada ya kupata maambukizi ya malaria mara kadhaa, mtu anaweza kupata kinga nusu. Mtu huyu bado kwa kiwango kikubwa anaweza kupata maambukizi ya malaria, lakini inawezekana asipate aina kali ya malaria. Baada ya kukaa kwa muda fulani nje ya eneo lenye malaria, kinga hii huisha polepole. Visa vingi vya malaria katika wasafiri hutokea kwa wale waliohama na kwenda katika maeneo yasiyo na malaria, kisha kutembelea maeneo yenye malaria waliyokulia bila kutumia dawa dhidi ya malaria kwa kuamini kuwa bado walikiuwa na kinga.

S: Malaria inasababishwa na virusi au bakteria?
J: Malaria haisababishwi na virusi au bakteria. Malaria husababishwa na kimelea kinachoitwa Plasmodium, ambacho kwa kawaida husambazwa na mbu walioambukizwa. Mbu anaponyonya damu kutoka kwa mtu mwenye malaria, anavichukua vimelea hivi ambavyo vipo kwenye damu. Baada ya wiki moja, mbu anaponyonya damu kutoka kwa mtu mwingine, vimelea hivi huingia ndani ya mwili wake, na malaria husambazwa hivi.