Ugonjwa wa fangasi ukeni
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Fangasi ukeni ni nini?
Fangasi ukeni ni maambukizi ya kawaida ya midomo ya uke (vulva) na uke yanayosababishwa na fangasi inayoitwa candida. Ugonjwa huu hujulikana pia kama fangasi kwenye sehemu za siri.
Kandida mara nyingi huwepo katika viwango vidogo mwilini. Hata hivyo, katika baadhi ya visa, kuna uwezekano fangasi hawa kuwepo kwa wingi na kusababisha maambukizi. Huu kwa kawaida siyo ugonjwa unaosambazwa kwa njia ya kujamiiana (STI). Lakini, wakati mwingine unaweza kusambazwa kati ya wapenzi.
Dalili kuu hujumuisha mwasho ukeni, maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana, na uchafu mweupe na mzito kutoka ukeni. Tiba ya fangasi ukeni inategemea uamuzi wa mtaalamu kulingana na hali ya mgonjwa na inaweza kutibika kirahisi kwa dawa.
Wakati mwingine maambukizi haya yanaweza kujirudia. Yanaweza kutokea katika vipindi vya msongo, hasa kwa watu wenye kisukari au magonjwa ya mfumo wa kinga. 1
Dalili za Fangasi Ukeni
Dalili kuu za maambukizi haya ni mwasho na hisia ya kuungua kwenye uke na midomo ya uke. Uchafu mweupe na mzito pia huweza kutokea. Baadhi ya watu pia huweza kupata maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana. 1
Vihatarishi vya Fangasi Ukeni
Chanzo cha fangasi ukeni ni fangasi wajulikanao kitaalamu kama “candida albicans,” ambao kwa kawaida huishi mwilini. Katika baadhi ya visa, kandida huweza kuongezeka na kusababisha maambukizi. 2 Haya ni maambukizi ya kawaida sana kwa wanawake na yanaweza kumuathiri mwanamke wa umri wowote.
Haya siyo maambukizi yanayosambazwa kwa njia ya kujamiiana (STI). Hata hivyo hutokea zaidi kwa wale wanaoshiriki katika tendo la kujamiiana. Vihatarishi vingine hujumuisha matumizi ya antibiotiki na ujauzito. Watu wenye udhaifu wa mfumo wa kinga au kisukari pia wapo kwenye hatari zaidi. 3
Baadhi ya watu huona kuwa hatari ya kupata maambukizi haya huweza kuongezeka wanapokuwa katika hali ya hewa ya joto na unyevu.
Utambuzi wa Fangasi Ukeni
Utambuzi kwa kawaida hufanywa kulingana na dalili na uchunguzi wa kimwili. Ikiwa utambuzi haujathibitishwa, sampuli ya majimaji ya ukeni huweza kuchukuliwa na kupimwa kwa uwepo wa fangasi. 4
Matibabu ya Fangasi Ukeni
Tiba ya fangasi ukeni hutegemea kiwango cha maambukizi na dalili alizonazo mgonjwa. Matibabu hujumuisha dawa dhidi ya fangasi.
Dawa ya kutibu fangasi ukeni huweza kupakwa kama krimu kwenye midomo ya uke, kuingizwa kama vidonge vya ukeni au kumezwa kama vidonge. Ni rahisi kunywa vidonge, lakini krimu na vidonge vya ukeni hupoza mwasho na maumivu ya ngozi. Kwa kawaida hakuna ulazima wa mtu kutibiwa ikiwa haonyeshi dalili zozote. 5
Njia za asili kutibu fangasi ukeni zinaweza kusaidia kuleta nafuu, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa baadhi ya njia hizi zinaweza kuwa na madhara mengine (side effects). Hata hivyo, tiba mbadala za kutibu fangasi ukeni, kama vile kitunguu saumu na mchai zinaungwa mkono na tafiti za kisayansi. 6
Kinga ya Fangasi Ukeni
Jinsi ya kujikinga na fangasi ukeni ni pamoja na kudumisha usafi sehemu za siri kwa maji safi, kuepuka kuvaa nguo za ndani zisizoruhusu joto na unyevu kutoka huweza kusaidia kuzuia maambukizi haya. Hasa katika maeneo yenye hali ya hewa ya unyevunyevu.
Pia inaweza kuwa na manufaa kuepuka vidonge vya antibiotiki ikiwa matibabu mengine kama vile krimu yapo. Watu wenye kisukari wanapaswa kukumbuka kuwa ni muhimu kudumisha kiwango kizuri cha sukari mwilini. Hii huweza kuzuia maambukizi haya kutokea.
Ingawa ugonjwa haumbukizwi kwa njia ya kujamiiana, ni vyema kuepuka michubuko wakati wa tendo la ndoa kwani michubuko hutengeneza mazingira mazuri kwa fangasi kuzaliana. 7
Ubashiri wa Fangasi Ukeni
Dawa ya fangasi ukeni kama utumiaji wake ulivyofafanuliwa hapo juu, huwa ina ufanisi sana na watu wengi hupata nafuu ndani ya wiki. Hata hivyo, ni kawaida kwa maambukizi kujirudia.