1. Ada
  2. Editorial
  3. Tiba & afya
  4. Kupunguza hatari: ugonjwa wa kisukari aina ya 2

Kupunguza hatari: ugonjwa wa kisukari aina ya 2

Mfano watu wenye ugonjwa wa kisukari wakikagua kiwango cha sukari katika damu

Labda umeshasikia kitu kinaitwa glukosi. Ni aina ya sukari unayopata kutoka kwenye chakula unachokula, na ni chanzo kikuu cha nguvu katika mwili wako. Glukosi inasaidia ubongo wako ufikirie, misuli yako isogee, na viungo vyako vifanye kazi. 

Mwili wako umekuza taratibu changamani za kuchakata glukosi kwa zaidi ya miaka milioni. Lakini iwapo taratibu hizo zitaacha kufanya kazi ipasavyo, unaweza kuugua.  

Aina ya 2 ya kisukari ni ugonjwa wa kawaida wenye uhusiano na glukosi. Unaathiri watu wengi zaidi leo kuliko wakati mwingine wowote. Hivyo basi, ni muhimu ukaelewa jinsi ya kupunguza hatari yako ya kupata ugonjwa huu. 

Tujifunze kuhusu ugonjwa wa kisukari, tuangalie kwa karibu aina ya 2 ya kisukari, na tambua ni nini unaweza kufanya leo ili kupunguza hatari yako ya kuupata.

Ugonjwa wa kisukari ni nini?

Kabla ya kuzungumza kuhusu ugonjwa wa kisukari, acha kwanza tuangalie jinsi mwili wako unavyopata glukosi.  

Unapokula chakula, mfumo wako wa kumeng’enya hukichakata na kutengeneza glukosi. Glukosi hiyo inapoingia kwenye damu yako, husababisha kongosho lako kutoa homoni inayoitwa insulini. Insulini huzunguka mwilini mwako kupitia damu, na hii huwezesha seli kupata glukosi na kuitumia kuleta nguvu mwilini. 

Unaweza kuifikiria insulini kama funguo isiyoonekana kwa macho inayoruhusu glukosi kuingia kwenye seli. 

Wakati ufunguo huo haupo au unaacha kufanya kazi, glukosi katika mwili wako haiwezi kwenda mahali  popote. Ikiwa viwango vyako vya glukosi katika damu vinabaki kuwa juu sana kwa muda mrefu, unaweza kuanza kujihisi mgonjwa. Huo ndiyo ugonjwa wa kisukari. 

Kuna aina kuu 2 za ugonjwa wa kisukari: aina ya 1 na aina ya 2.

Aina ya 1 hutokea wakati mfumo wa kinga mwilini unashambulia kongosho ili lisiweze kutoa insulini ya kutosha. Katika hali fulani, kongosho linaweza kuacha kabisa kutoa insulini.1

Aina ya 2 hutokea wakati kongosho linapopunguza uzalishaji wa insulini au wakati insulini haiathiri seli namna ifaavyo.2

Baada ya kuzitambulisha kwa ufupi aina hizi mbili za ugonjwa wa kisukari, tunaendelea na makala hii kwa kuzingatia aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari.

Ni yapi yanayohusiana na aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari?

Aina ya 2 ya kisukari ni ugonjwa ulioenea zaidi duniani.3

Ni nani aliye katika hatari?

Kila mtu ana kiwango tofauti cha hatari ya kupata aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. Kiwango cha hatari kinahusishwa na mtindo wa maisha, umri, au sababu za kimaumbile (jenetiki). Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazopelekea mtu kuwa kwenye hatari ya kupata aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari:4

  • kuwa na uzito wa kupita kiasi
  • kutokujishughulisha kimwili
  • kuwa na umri wa miaka 45 au zaidi
  • kuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari aina ya 2 katika familia
  • kuwa na asili ya Waafrika Weusi, Waafrika wa Karibiani, au Asia ya Kusini.

Ni muhimu kukumbuka kwamba unaweza kupata aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari bila kuwa na historia yoyote ya ugonjwa huo katika familia. Na pia kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia haimaanishi kuwa utaupata.5 Jambo la msingi zaidi ni kuelewa sababu zinazoathiri kiwango chako cha hatari ya kuupata.

Nini hutokea unapokuwa na aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari?

Watu wenye aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari wanaweza kupata dalili kadhaa. Zifuatazo ni baadhi ya dalili ambazo ni kawaida kutokea:6

  • kwenda haja ndogo mara nyingi sana, haswa wakati wa usiku
  • kuhisi kiu kuliko kawaida
  • kuhisi uchovu sana
  • kupungua uzito bila sababu
  • mikato au vidonda kuchukua muda mrefu kupona
  • uwezo hafifu wa kuona (kuona ukungu).

Baadhi ya watu hawatambui dalili zao kwa muda mrefu. Kwahiyo ni muhimu uelewe ni nini kinakuweka hatarini. Ikiwa haujatibiwa, aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari inaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.  

Madaktari hutibuje aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari? 

Kupitia mchanganyiko wa dawa za kupunguza viwango vya glukosi kwenye damu na mabadiliko mazuri katika mtindo wa maisha, watu wengi wenye aina ya 2 ya kisukari wanaishi maisha ya kawaida.

Kwa watu wengi, hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kadiri muda unavyokwenda. Lakini tafiti mpya zinaonyesha kwamba mtu mwenye ugonjwa wa kisukari aina ya 2 kwa muda wa hadi miaka 6 anaweza kurudi kwenye hali yake ya kawaida kiafya kupitia umakini katika upunguzaji uzito na usimamizi wa afya.5

Unawezaje kupunguza hatari yako?

Elewa hatari iliyo mbele yako

Aina ya 2 ya kisukari inaweza kuchukua miaka kupevuka, na baadhi ya watu hawatambui dalili zozote mpaka wamechelewa sana. Kwahiyo kwa kadiri unavyoelewa zaidi kuhusu vihatarishi vyako, ndivyo utakavyokuwa umejidhatiti vizuri zaidi kutambua kitu chochote cha kushangaza na kufanya maamuzi sahihi ya mtindo wa maisha.

Mwanzo mzuri ni kuangalia kiwango chako cha hatari kwa kutumia kikokotoo cha mtandaoni cha ukaguzi wa hatari ya aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. Unaweza pia kumuuliza daktari wako kuhusu hatari yako.  

Tabia zenye manufaa kiafya husaidia sana

Kudumisha uzito wa mwili ambao ni mzuri kiafya na kujishughulisha (link to “kujishugulisha” article) kunaweza kusaidia kupunguza hatari yako ya kupata aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. Zaidi ya hilo, pia utajihisi ni mwenye afya zaidi na furaha zaidi.

Tafiti zinaonyesha kwamba hata dakika 30 tu za kutembea haraka kila siku zinaweza kupunguza hatari yako ya kupata aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari.7 Kwahiyo vaa viatu vyako vya kutembelea na uende kutembea bila kuhofia kupata kesi ya uzururaji.

Lishe bora pia itasaidia. Ila usijali: kwani hiyo haimaanishi kupiga marufuku vyakula vyako vyote uvipendavyo.8 Jambo la muhimu zaidi ni kuzingatia ulaji wa kiasi. Hiyo inamaanisha kula mara kwa mara milo kamili usiyozidisha ujazo. 

Jaribu kupanga ratiba ya chakula chenye afya kwa wiki. Kuwa na friji iliyojaa chakula kinachofaa itakusaidia kuepuka kukosa kula na kula kupita kiasi. Na bado unaweza kustahili kufurahia chakula au kitafunio ukipendacho. 

Kwa kufanya mabadiliko machache kadhaa, ni rahisi kutunza afya yako.


  1. Atkinson, M. A., Cold Spring Harb Perspect Med, (2012), doi: 10.1101/cshperspect.a007641.

  2. Galicia-Garcia, U,. Int. J. Mol. Sci., (2020), doi: 10.3390/ijms21176275.

  3. WHO. “Diabetes.” Kimetumika Februari 3, 2021.

  4. CDC. “Diabetes Risk Factors.” Kimetumika Februari 3, 2021.

  5. Lean. M. EJ., The Lancet, (2018), doi: https://doi.org/10.1016/S0140-6736(17)33102-1.

  6. CDC. “Diabetes Symptoms.” Kimetumika Februari 3, 2021.

  7. Loreto C. D., Diabetes Care, (2005), doi: 10.2337/diacare.28.6.1295.

  8. NIH. “Diabetes Diet, Eating, & Physical Activity.” Kimetumika Februari 3, 2021.

Mwandishi:

Harry O’Connor
Harry O’Connor

Harry ni Mwandishi wa Ada katika Masuala ya Kisayansi.

Mfasiri:

Rungwe Hashim
Rungwe Hashim

Rungwe ni mwandishi na msimamizi wa maudhui ya Kiswahili ya Ada.