1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ugonjwa wa kisonono

Ugonjwa wa kisonono

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Kisonono ni nini?

Kisonono ni maambukizi ya bakteria wanaosambazwa kwa njia ya ngono na bakteria anayeitwa Neisseria gonorrhoeae. Hali hii wakati mwingine huitwa 'the clap'. Hii ni hali ya kawaida. Kisonono mara nyingi huambukiza urethra (mrija kati ya kibofu cha mkojo na ngozi) pamoja na shingo ya kizazi kwa wanawake.

Dalili za kawaida ni maumivu wakati wa kukojoa na uchafu kutoka kwenye mrija wa mkojo. Watu wengi wenye kisonono hawana dalili, na hugunduliwa kuwa na hali hii kwa vipimo vya uchunguzi (kupima watu ambao hawana dalili).

Kisonono hutibiwa kwa antibiotiki. Mpenzi wako lazima pia atibiwe. Hali hii ikitibiwa katika hatua za mwanzo, watu wengi hupona vizuri na huwa hawana matatizo endelevu. Maambukizi yasiyotibiwa yanaweza kusababisha madhara, ikiwa ni pamoja na utasa.

Kisonono na dalili zake

Kisonono mara nyingi haisababishi dalili zozote. Wote wanaume na wanawake wanaweza kuwa na maumivu kama ya kuungua wakati wa kukojoa. Wanaume wanaweza kuwa na uchafu mweupe au wa njano unaotoka kwenye uume, maumivu wakati wa kumwaga manii au korodani iliyovimba. Wanawake wanaweza kuwa na uchafu mweupe au wa njano unaotoka kwenye uke, kutokwa damu ukeni baada ya kujamiiana au katikati ya vipindi vya hedhi na maumivu kwenye sehemu ya chini ya tumbo.

Ikiwa kuna maambukizi ya kisonono kwenye sehemu nyingine za mwili, dalili zinaweza kujumuisha koo kuuma, maumivu wakati wa kupata haja kubwa au uchafu kutoka kwenye njia ya haja kubwa. Ikiwa mtoto mchanga anapata maambukizi haya kutoka kwa mama yake wakati wa kuzaliwa, anaweza kuwa na maambukizi ya jicho (kikope) au maambukizi ya koo.

Vihatarishi vya ugonjwa wa kisonono

Kisonono mara nyingi husambazwa kwa njia ya kujamiiana bila kutumia kinga na mtu aliyeambukizwa. Pia, inawezekana kwa mtoto mchanga kupata ugonjwa huu kutoka kwa mama yake wakati wa kuzaliwa.

Watu wenye umri kati ya miaka 15 na 35 wana uwezekano mkubwa wa kupata kisonono. Watu wanaojamiiana bila kutumia kondomu huongeza hatari ya wao kupata kisonono.

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na sampuli kutoka kwenye eneo lililoathirika (uume, uke, njia ya haja kubwa au koo) inayoonyesha uwepo wa bakteria aina ya Neisseria gonorrhoeae. Kuna uwezekano wa kuwa na dalili za kisonono wakati wa uchunguzi za sehemu za siri za mwanamke. Hamna kipimo kimoja cha kutambua magonjwa yote ya zinaa. Tafadhali ongea na mtaalamu wa afya kwa taarifa zaidi.

Matibabu ya kisonono

Je, kuna dawa ya kisonono? Kisonono hutibiwa kwa antibiotiki. Ni muhimu kumwambia mtu au watu unaohusiana nao kimapenzi kuhusu utambuzi, ili na wao pia waweza kutibiwa haraka iwezekanavyo.

Kinga ya maambukizi ya kisonono

Kutumia kondomu wakati wa kujamiiana huzuia maambukizi ya kisonono. Matibabu ya washirika wa ngono ni muhimu ili kuzuia maambukizi mapya na kuenea zaidi kwa maambukizi.

Ubashiri

Maambukizi haya yasipotibiwa, yanaweza kusababisha makovu na kupungua kwa upana wa urethra (mrija kati ya kibofu cha mkojo na ngozi). Kisonono isiyotibiwa pia huweza kusababisha utasa kwa wanaume na wanawake.

Wanawake wapo kwenye hatari ya kupata madhara kama vile, makovu na kupungua kwa ukubwa wa mirija ya fallopian (mirija ambayo mayai husafari kutoka kwenye ovari hadi kwenye tumbo la uzazi) na maambukizi kwenye nyonga na sehemu ya chini ya tumbo.


Washirikishe wengine kwenye makala hii: