1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ugonjwa wa bawasiri

Ugonjwa wa bawasiri

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Bawasiri ni nini?

Bawasiri ni kuvimba kwa mishipa ya damu iliyopo ndani ya au katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa. Ni hali ambayo inaweza kusababisha nyama kujitokeza nje. Hivyo bawasiri inaweza kuwa bawasiri ya ndani au bawasiri ya nje. Ugonjwa huu unaweza kusababisha mwasho, maumivu na damu au kamasi kutoka wakati wa kujisaidia haja kubwa ingawa wakati mwingine hauna dalili. 1 Madhara ya bawasiri ya ndani ni pamoja na damu kutoka wakati wa kujisaidia, damu kuganda ndani ya mishipa ya damu na maumivu.

Kutokea kwa bawasiri kunaweza kuhusishwa na hali kama uzee, ujauzito, kuharisha au choo kufunga (constipation), saratani kwenye nyonga au kukaa kwa muda mrefu. Tiba ya bawasiri inategemea aina ya bawasiri na ukubwa wa tatizo. Matibabu ya bawasiri yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa au upasuaji mdogo.

Dalili za Bawasiri

Inakadiriwa 40% ya watu wenye bawasiri hawana dalili za moja kwa moja. 2 Dalili za bawasiri hujumuisha maumivu, mwasho na hisia ya kitu kinachokera katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa. Baadhi ya watu hupata shida kujisaidia haja kubwa na hutokwa damu wanapojisaidia. Wakati mwingine mishipa ya damu huweza kujitokeza nje. Ikiwa hali hii inatokea, inawezekana kuhisi uvimbe mdogo katika eneo husika.

Vihatarishi vya Bawasiri

Bawasiri hutokea pale shinikizo huongezeka kwenye mishipa ya damu inayozunguka njia ya haja kubwa. Hii huweza kuwa matokeo ya kitu kinachokandamiza utumbo, kama vile wakati wa ujauzito, au huweza kutokea kutokana na kujikamua sana wakati wa haja kubwa kutokana na kufunga choo au kuharisha kwa muda mrefu. Hali hii hutokea sana na hutokea zaidi kadri umri unavyoongezeka. Watu wenye uzito wa kupita kiasi wana uwezekano mkubwa wa kupata bawasiri. Vitu vingine vinavyoongeza hatari ya kupata bawasiri ni pamoja na:

  • Kubeba vitu vizito mara kwa mara
  • Kukohoa au kutapika mara kwa mara
  • Kujamiiana kinyume na maumbile
  • Historia ya bawasiri kwenye familia
  • Magonjwa yanayoathiri njia ya haja kubwa
  • Kukaa kwa muda mrefu
  • Uzee na matatizo ya kutopata choo. 1

Utambuzi wa Bawasiri

Utambuzi hufanywa na daktari kwa kuchukua maelezo ya mgonjwa na kuchunguza njia ya haja kubwa. Uchunguzi wa njia ya haja kubwa hujumuisha kuangalia eneo hili na kuingiza kidole kwa upole kuchunguza sehemu ya ndani ya njia ya haja kubwa. Kama bawasiri hazionekani kirahisi, au sababu ya kutoka damu haijaeleweka vizuri, uchunguzi wa ziada huweza kufanywa ili kuhakikisha hamna sababu nyingine ya dalili hizi.

Matibabu ya Bawasiri

Bawasiri inatibika na kuna njia mbalimbali za kutibu bawasiri. Tiba halisi ya bawasiri ni kuhakikisha kupata choo kilaini na kuepuka kufunga choo, ili kuepuka hali kuwa mbaya zaidi. Krimu za kupaka na dawa za kuingiza katika njia ya haja kubwa (suppositories) zinaweza kusaidia kupunguza kuvimba, mwasho na maumivu. Dawa hizi hupatikana katika maduka ya dawa. Kuna matibabu mengine ambapo sindano au kamba hutumika ili kupunguza ukubwa wa mishipa ya damu. Dawa ya bawasiri sugu ni upasuaji.

Kinga ya Bawasiri

Kuhakikisha unapata choo kilaini husaidia kuzuia bawasiri na kupunguza kujirudia kwa dalili za bawasiri. Hii huwezekana kwa kula vyakula vyenye nyuzinyuzi (fiber),kunywa maji ya kutosha, kuwa na uzito unaofaa, kuepuka kukaa kwa muda mrefu, kuepuka kujikamua wakati wa haja kubwa na kuepuka kubeba vitu vizito mara kwa mara. 3

Ubashiri wa Bawasiri

Bawasiri ni hali inayoweza kukera lakini mara nyingi hazina madhara mabaya kwa afya ya binadamu. Ugonjwa huu unaweza kuisha wenyewe ndani ya wiki. Bawasiri mara nyingi hujirudia, na huzidi kuwa mbaya kadiri muda unavyoenda.