1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ngiri ya Kinena

Ngiri ya Kinena

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Ngiri ni nini?

Ngiri ya kinena hufahamika kwa Kiingereza kama Inguinal Hernia. Ngiri katika eneo la kinena hutokea pale utumbo hujitokeza kwenye uwazi katika ukuta wa tumbo kwenye kinena. Ngiri kwenye kinena hutokea mara nyingi na huwaathiri zaidi wanaume.

Dalili kuu ni uvimbe kwenye kinena, ambao ukisukumizwa ndani unapotea kwa muda. Utambuzi hufanywa na daktari kwa kuchunguza uvimbe kwa kutumia kipimo cha ultrasound. Hali hii isipotibiwa inaweza kusababisha utumbo kunaswa na hivyo kushindwa kupatiwa damu na hatimaye kuoza. Hali hii hurekebishwa kwa upasuaji. Ngiri iliyonaswa ni hali ya dharura na inahitaji matibabu ya dharura kwa njia ya upasuaji. 1

Dalili za ngiri

Dalili za ugonjwa wa ngiri ni pamoja na uvimbe kwenye eneo la kinena au kifuko cha korodani. Uvimbe huu unaweza kusababisha maumivu, hasa wakati wa mazoezi. Uvimbe unaweza kupotea kwa muda mrefu pale unaposukumizwa ndani lakini baadaye hurejea.

Vihatarishi

Ngiri huweza kutokea katika kiungo chochote kinaposogea katika eneo la mwili ambalo kwa kawaida kiungo hicho hakitakiwi kuwepo. Ngiri ya kinena hutokea pale utumbo mdogo unapopita katika uwazi katika ukuta wa tumbo na kutokelezea kwenye kinena.

Uwazi huu unaweza kutokea kabla ya kuzaliwa, au baada ya kuzaliwa kutokana na umri, jeraha au udhaifu wa misuli. Vitu vinavyoongeza shinikizo kwenye tumbo, kwa mfano unene wa kupita kiasi, kikohozi cha muda mrefu, kujikamua sana wakati wa haja kubwa au kubeba vitu vizito, huongeza uwezekano wa kupata hali hii.

Hali hii kwa kawaida hujitokeza zaidi kwa wanaume, na watu wenye umri wa makamo. Hii ina maana hata wanawake pia hupatwa na hali hii. 2

Utambuzi

Utambuzi wa ugonjwa wa ngiri hufanywa kwa uchunguzi wa kimwili kwa kutumia kipimo cha ultrasound katika eneo la kinena.

Matibabu

Matibabu ya ngiri hujumuisha upasuaji wa kurekebisha uwazi kwenye ukuta wa tumbo. Njia moja ni kwa kuweka wavu katika eneo la kinena, ili kufunika uwazi uliosababisha ngiri. Hii hufanywa kwa njia ya upasuaji wa matobo unaofahamika kiitalam kama laparoscopic surgery.

Hivyo basi, tiba ya ngiri kwa wanaume na wanawake hufanyika baada ya utambuzi na kwa kawaida matibabu kwa njia ya upasuaji huwa na matokeo mazuri kwa ugonjwa huu. 2

Kinga

Kuepuka shughuli ambazo huongeza shinikizo katika tumbo, kama vile kujikamua wakati wa haja kubwa au kubeba vitu vizito, huweza kuzuia kupata hali hii, au huweza kuzuia ngiri kuwa kubwa zaidi.

Ubashiri

Upasuaji kwa kawaida hutibu hali hii. Ngiri isipotibiwa, huweza kusababisha utumbo kunaswa, ambayo mara nyingi husababisha maumivu makali, utumbo kuvimba au sehemu za utumbo kuoza. Hii inaweza kuhatarisha maisha.