1. Ada
 2. Magonjwa
 3. Upungufu wa madini ya chuma

Upungufu wa madini ya chuma

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Upungufu wa damu mwilini una maana gani?

Upungufu wa damu kutokana na kupungua kwa madini ya chuma mwilini ni kati ya aina kuu za upungufu wa damu. Ni hali ambayo mwili unakuwa hauna madini ya chuma ya kutosha ili kutengeneza hemoglobini. Hemoglobini ni protini kwenye seli nyekundu za damu ambayo ni muhimu katika kusafirisha oksijeni kwenye tishu za mwili. 1

Hali hii hutokea zaidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa, ingawa inaweza kumathiri mtu mwenye umri wowote. Sababu za hali hii kutokea hujumuisha kutoka damu kwa muda mrefu, na magonjwa sugu ya mfumo wa kumeng'enya chakula. Kula lishe yenye kiwango kidogo cha vyakula vyenye madini ya chuma pia huweza kuwa chanzo ya hali hii kutokea.

Dalili za upungufu wa damu ni pamoja na uchovu, udhaifu, kukosa nguvu na kuishiwa pumzi. Wale walioathirika pia huweza kuwa na ngozi iliyopauka na kupoteza nywele, na kucha kuwa dhaifu. Matibabu kwa kawaida hujumuisha kutumia virutubisho vya madini ya chuma na kuongeza madini ya chuma kwenye lishe. 2

Watu wengi hupona vizuri kwa kutumia virutubisho na kwa kutibu chanzo ya hali hii kutokea.

Vihatarishi vya upungufu wa madini ya chuma

Upungufu wa damu humaanisha kuwa mwili hauna hemoglobini ya kutosha ili kusafirisha oksijeni mwilini. Madini ya chuma ni muhimu katika uzalishaji wa hemoglobini kwenye seli nyekundu za damu. Upungufu wa damu hutokea ikiwa mwili hauna madini ya chuma ya kutosha.

Mara nyingi hii hutokea mtu akipoteza kiwango kikubwa cha damu. Hali hii pia huweza kutokea wakati wa ujauzito ambapo mwili huitaji kiwango kikubwa zaidi cha madini ya chuma. Inaweza pia kutokea baada ya muda ikiwa mtu hawezi au hapati madini ya chuma ya kutosha kwenye lishe. Upungufu wa madini ya chuma ni kati ya visababishi vikuu vya upungufu wa damu na wanawake walio katika umri wa kuzaa huathirika zaidi. Watoto, vijana na wazee, watu wenye uzito kupita kiasi pia wamo hatarini kukabiliwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini. 1

Dalili za upungufu wa madini ya chuma mwilini

Watu wenye upungufu wa damu kiasi mara nyingi hawana dalili. Dalili za kawaida ni pamoja na: 3

 • Uchovu
 • Kushindwa kuzingatia kazini or masomoni
 • Usahaulifu
 • Kupungua uwezo wa kufanya mazoezi
 • Nywele kupoteza uimara wake, na hata kupoteza nywele
 • Kucha kuvunjika kirahisi
 • Vidonda na michubuko kuchukua muda mrefu kupona
 • Ulimi kuuma
 • Vidonda kwenye kingo za mdomo
 • Ugonjwa unaofanya miguu isitulie (restless legs syndrome)
 • Watoto wachanga wenye upungufu wa madini ya chuma wanaweza kuchelewa kukua
 • Hamu au kula vitu visivyo kawaida kuliwa, kama vile udongo, chaki au makaa (pica syndrome)
 • Matatizo ya kupumua
 • Kupauka kwa ngozi
 • Maumivu ya kichwa

Dalili zingine, ambazo hujitokeza mara chache zinaweza kujumuisha: 4

 • Ugumu wa kumeza
 • Chakula kuwa na ladha isiyo ya kawaida
 • Mwasho
 • Kusikia mlio au kelele kichwani (tinnitus)

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na dalili na historia ya matibabu. Vipimo vya damu hufanywa ili kuchunguza viwango vya hemoglobini pamoja na idadi na ukubwa wa seli nyekundu za damu. Viwango vya madini ya chuma pia hupimwa. Vipimo vingine huweza kuhitajika ili kutambua chanzo cha upungufu wa madini. Kipimo cha endoscopy, ambapo kamera hupitishwa mdomoni ili kuangalia mfumo wa umeng'enyaji chakula, huweza kufanywa kwa ajili ya utambuzi.

Matibabu

Ikiwa upungufu wa madini ya chuma husababishwa na ugonjwa mwingine, basi ugonjwa huu hupaswa kutibiwa. Hii huweza kuzuia upungufu zaidi wa madini ya chuma au matatizo katika ufyonzaji wa madini haya.

Ikiwa mtu aliyeathirika hana matatizo yoyote ya ufyonzaji wa madini ya chuma, wanapaswa kula vyakula vyenye madini ya chuma. Dengu, wali wa kahawia na maharage hupendekezwa zaidi. Mboga za majani na matunda yaliyokaushwa kama vile aprikoti na mizambarau pia husaidia. Samaki, nyama na mayai pia vina viwango vya juu vya madini ya chuma. Watu wenye uwekezaji mdogo mwilini wa madini ya chuma huweza kutumia virutubisho.

Ikiwa viwango vya madini ni chini sana na mtu anahitaji viwango vikubwa ya madini ya chuma, basi madini haya huweza kuongezwa mwilini kupitia mishipa ya damu. 6

Kinga

Lishe yenye manufaa kiafya huweza kuzuia hali hii. Kula vyakula vya kutosha vyenye madini ya chuma ni muhimu. Kwa kuwa wanawake wajawazito wapo kwenye hatari zaidi ya kupata upungufu wa damu, wanapaswa kuzingatia kutumia virutubisho.

Hitimisho

Upungufu wa madini ya chuma ni tatizo la kiafya ambalo linaweza kuathiri watu wa rika zote, lakini mara nyingi huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa, watoto, vijana, na wazee. Dalili zinaweza zisizoonekane au kutambulika mwanzoni, lakini zinaweza kuwa mbaya zaidi na kuathiri ubora wa maisha ya mtu ikiwa hali hii haitatibiwa mapema. Kutambua na kutibu upungufu wa madini ya chuma ni muhimu ili kuhakikisha kuwa mwili unapata oksijeni ya kutosha kwa ajili ya tishu na viungo vyote. 

Njia bora za kukabiliana na upungufu wa madini ya chuma ni pamoja na kula lishe yenye madini ya chuma, kutumia virutubisho inapohitajika, na kutibu magonjwa au hali nyingine zinazosababisha upungufu huu. Kwa kuwa hali hii inaweza kudhibitiwa kwa urahisi kwa kufanya mabadiliko madogo kwenye lishe na mtindo wa maisha, ni muhimu kwa watu kuelewa umuhimu wa lishe bora na ufuatiliaji wa afya zao. 

Maswali Yanayoulizwa Mara Kwa Mara (FAQs)

S: Vyakula vyenye madini ya chuma ni vipi?
J: Vyakula vyenye madini ya chuma ni pamoja na nyama nyekundu, kuku, samaki, maharage, dengu, spinach, brokoli, na mboga za majani zenye rangi ya kijani kibichi. Pia, vyakula kama karanga, mbegu, mayai, na matunda yaliyokaushwa kama aprikoti na mizambarau yana kiwango kizuri cha madini ya chuma.

S: Ni nini tiba ya upungufu wa damu mwilini?
J: Tiba ya upungufu wa damu mwilini hujumuisha matumizi ya virutubisho vya madini ya chuma na kuboresha lishe ili kuhakikisha ulaji wa kutosha wa vyakula vyenye madini ya chuma. Ikiwa upungufu wa madini ya chuma husababishwa na ugonjwa mwingine, ugonjwa huo unapaswa kutibiwa kwanza. Katika hali mbaya, madini ya chuma yanaweza kuongezwa mwilini kupitia mishipa ya damu.

S: Ni zipi dalili za upungufu wa damu mwilini?
J: Dalili za upungufu wa damu mwilini ni pamoja na uchovu, udhaifu, kupumua kwa shida, kupauka kwa ngozi, na maumivu ya kichwa. Dalili nyingine zinaweza kujumuisha kukatika kwa kucha, kunyonyoka kwa nywele, kingo za kinywa kupasuka, na ugumu wa kumeza. Kwa baadhi ya watu, dalili hizi zinaweza zisiwe kali na zisionekane mwanzoni.