1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ugonjwa wa typhoid

Ugonjwa wa typhoid

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Typhoid ni nini?

Enteric fever au homa ya matumbo ni maambukizi ya bakteria kwenye utumbo, lakini pia huweza kuathiri sehemu tofauti za mwili. Hali hii pia hujulikana kama homa ya typhoid au maambukizi ya typhoid.

Bakteria aina ya salmonella typhi na paratyphi hujulikana kusababisha ugonjwa huu. Kawaida maambukizi husambazwa kwa chakula na maji yaliyoambukizwa.

Watu wanaoishi kwenye miji yenye usafi duni wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Dalili za kawaida ni homa, maumivu ya tumbo, choo kufunga au kuharisha. Vipimo vya damu na haja kubwa hufanywa ili kufanya utambuzi wa ugonjwa wa typhoid.

Matibabu hujumuisha antibiotiki na kurudishia maji mwilini. Watu wengi hupata nafuu ndani ya siku au wiki chache baada ya matibabu kuanza. Inawezekana kupata chanjo. Ili kuepuka maambukizi ya typhoid, ni muhimu kuosha mikono mara kwa mara. Kupika chakula vizuri na kunywa maji yaliyochemshwa pia husaidia.

Dalili za typhoid

Kwa kawaida, dalili za typhoid ni pamoja na:

  • Homa
  • maumivu ya tumbo
  • kuharisha

Maumivu ya kichwa, kupoteza hamu ya kula na kuhisi kuumwa kwa ujumla pia huweza kuwa ni sehemu ya dalili. Katika baadhi ya matukio, watu hupatwa na tatizo la kufunga choo (constipation), badala ya kuharisha. Watoto wanaweza kuwa na hasira zaidi, kulia au kuamka usiku.

Visababishi vya ugonjwa wa typhoid

Mtu yeyote anaweza kupata homa ya typhoid. Watoto na vijana wapo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu. Hatari kubwa zaidi ipo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5. Sababu nyingine hatarishi ni kusafiri au kuishi kwenye nchi zenye matukio mengi ya ugonjwa wa typhoid. Maambukizi huweza kusambazwa kirahisi kwenye miji yenye usafi duni.

Utambuzi

Daktari anashuku ugonjwa huu baada ya kupata maelezo ya afya ya mtu husika. Hii hufuatiwa na uchunguzi wa kimwili. Vipimo vya maabara huweza kuthibitisha maambukizi kwenye sampuli ya damu na haja kubwa.

Matibabu ya ugonjwa wa typhoid

Je, kuna dawa za typhoid? Dawa za antibiotiki zimeonyesha uwezo mkubwa wa kutibu typhoid, na hivyo matibabu yake yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo. Baada ya kupata majibu kutoka maabara, matibabu yanaweza kubadilishwa. Pia ni muhimu kunywa maji ya kutosha ili kurudisha maji yaliyopotea mwilini kutokana na kuharisha. Zaidi ya hayo, watu walioambukizwa wanatakiwa kuchukua tahadhari na kutosambaza bakteria hawa kwa wengine. Wanapaswa kuosha mikono na kuepuka kuwatayarishia chakula wengine.

Kinga ya ugonjwa wa typhoid

Kuna chanjo ya ugonjwa huu ambayo hupendekezwa kwa watu ambao wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi. Katika maeneo yenye kesi nyingi za homa ya typhoid, ni muhimu kuosha mikono, kupika na kuosha chakula vizuri na kunywa maji yaliyochemshwa tu.

Ubashiri

Watu wengi wanaopata matibabu ya antibiotiki hupona ndani ya wiki 2 hadi 4. Kawaida, hamna madhara yoyote. Ikiwa matibabu ya antibiotiki hayajakamilika jinsi daktari alivyopendekeza, maambukizi yanaweza kujirudia na kuwa vigumu zaidi kutibu.


Washirikishe wengine kwenye makala hii: