1. Ada
  2. Editorial
  3. Biashara & sekta
  4. Ufuatiliaji wa mwenendo wa afya ya akili wakati wa janga la ugonjwa

Ufuatiliaji wa mwenendo wa afya ya akili wakati wa janga la ugonjwa

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Watoto, mtu 1 kati ya watu 6 walio na umri wa chini ya miaka 18 ana uwezekano wa kuwa na tatizo la afya ya akili. Lakini cha kustaajabisha, 75% ya watu hao hawapati huduma ya afya wanayohitaji.1

Janga hili limevuruga maisha ya vijana duniani wakati wa kipindi muhimu zaidi kiukuaji kimaumbile kuliko vipindi vyote katika maisha yao. Hiyo inamaanisha kuwa tatizo hili la afya ya akili ni la muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Ili kuelewa athari za janga hili la ugonjwa wa korona kwa afya ya akili ya vijana, tulichunguza kwa kina takwimu za Ada ili kufahamu kinachoendelea.

Tulikagua tathmini 200,000 za Ada zilizokamilishwa kwa ajili ya watumiaji walio na umri wa chini ya miaka 18 katika kipindi cha kati ya Januari 2019 na Machi 2021. Tulijumuisha takwimu kutoka nchi 8 za Ulaya ili kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye hisia za watu (mood) katika uchanganuzi wetu wa takwimu.  

Ramani inayoonyesha nchi 8 tulizojumuisha katika utafiti wetu: Ureno, Uhispania, Ufaransa, Uingereza, Uswisi, Ujerumani, Austria, Rumania.

Embu tuangalie kile tulichogundua.

Janga la korona liliathiri vipi afya ya akili ya vijana?

Katika nchi zote 8, wastani wa sehemu ya tathmini inaonyesha kwamba kwa vijana walio na umri wa chini ya miaka 18, sonona iliongezeka kutoka 7.5% mwezi wa Machi 2020 hadi kufikia 12.6% mwezi wa Machi 2021. Hilo ni ongezeko la 67%.

Kwa ongezeko kubwa kama hilo la tathmini zinazoonyesha tatizo la sonona, tulichunguza takwimu kwa undani zaidi ili kuona kama tungeweza kubaini mambo yanayoweza kuwa yanasababisha.

Ongezeko la 67% la tathmini zinazoonyesha tatizo la sonona kwa vijana walio na umri wa chini ya miaka 18

Grafu inayoonyesha ongezeko la wastani wa 67% la idadi ya tathmini zilizofanywa na watumiaji walio na umri wa chini ya miaka 18 ambalo lilionyesha tatizo la sonona.

Je, tunaweza kutambua sababu zozote?

Kufungwa kwa shule wakati wa “lockdown” kumefanya iwe vigumu zaidi kwa watoto kujumuika, kujifunza, na kusitawi kama binadamu. Tulikisia kuwa hii inaweza kuwa sababu ya kuongezeka kwa viwango vya sonona tulivyoona katika takwimu zetu za tathmini.  

Kwa kutumia takwimu za kufungwa kwa shule kwa nchi zote 8 kutoka kwa “Covid-19 Government Response Tracker,”2, tulichanganua athari za kufunga shule kwa afya ya akili ya vijana. 

Grafu inayoonyesha ongezeko kubwa la kitakwimu la asilimia 3.1 katika tathmini zinazoonyesha tatizo la sonona miongoni mwa vijana walio na umri wa chini ya miaka 18 kutokana na kufungwa kwa shule.

Huu ni ugunduzi muhimu kwani unaweza kusaidia kutoa taarifa muhimu katika hatua za kukabiliana na janga la siku zijazo.

Thamani ya ufahamu wa takwimu za watu katika wakati halisi

Licha ya kupiga hatua katika utambuzi na matibabu ya magonjwa ya akili, watu wengi wenye matatizo ya afya ya akili hawapati kamwe huduma wanayohitaji. Uelewa mdogo wa masuala ya afya ya akili na unyanyapaa ni sehemu muhimu za tatizo hili.   

Kupitia utafiti wa mtumiaji na majaribio, tunagundua mara kwa mara kuwa watumiaji wengi wanapendelea usiri wa kuangalia afya zao za akili kupitia app ya Ada badala ya kupitia mwanadamu. Na ndivyo ilivyo pia kwa matatizo mengine ya kibinafsi ya afya. 

Usiri wa mtumiaji unamaanisha kuwa ufahamu wa takwimu kama hizi unaweza kusaidia mashirika ya afya kuelewa mahitaji ya afya ya watu wao na kubuni huduma za afya kwa watu ambao vinginevyo huenda wasiweze kamwe kupata utambuzi wowote wa matatizo yao. Yote hayo yanafanyika bila kufichua taarifa za kibinafsi za watumiaji.

Sababu nyingine zinazochangia watu walio na matatizo ya afya ya akili kutopata huduma wanazohitaji ni pamoja na ukosefu wa tambuzi za magonjwa kutokana na upatikanaji duni wa huduma, utambuzi wa ugonjwa usio sahihi kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya kitiba, na hata ujumuishaji mdogo wa magonjwa haya katika tathmini za dalili zinazowezeshwa na mfumo wa Akili Bandia (AI).

Kwa ujumuishaji mpana wa magonjwa, pamoja na kusaidia afya ya akili na watoto, takwimu za Ada zinaweza kusaidia mashirika kutambua mienendo ya magonjwa, kuchangia katika upangaji wa huduma za afya, na kusimamia afya za watu wao.

Jifunze zaidi kuhusu ubora wa kitiba katika Ada, au wasiliana nasi.


  1. The Children’s Society. “Children’s mental health statistics.” Kimetumika tarehe 28 Julai 2021.

  2. BSG. “Oxford COVID-19 Government Response Tracker.” Kimetumika tarehe 28 Julai 2021.

Mwandishi:

Alicia Mehl

Alicia anaongoza timu ya Ada ya Magonjwa ya Mlipuko & Afya ya Jamii