1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Ugonjwa wa kiharusi

Ugonjwa wa kiharusi

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Kiharusi ni nini?

Kiharusi cha muda mfupi , pia huitwa Transient ischemic attack (TIA), ni hali ya mfumo wa neva unaotokea ghafla na hudumu kwa muda mfupi. Hii husababishwa na mishipa ya damu kwenye ubongo kuziba kwa muda mfupi.

Dalili mara nyingi hazidumu zaidi ya saa moja lakini huweza kudumu hadi masaa 24. Dalili za kawaida ni kutoweza kuona, kushindwa kuongea vizuri, udhaifu wa uso, mkono au mguu.

Matibabu hulenga kuzuia hali hii kujirudia au kupata kiharusi kwa kufanya damu iwe nyembamba na kutibu hali ambazo huongeza uwezekano wa kupata kiharusi. Ingawa hali hii haisababishi madhara ya kudumu kwenye ubongo, ni onyo kuwa kiharusi kinaweza kutokea hivi karibuni. Watu ambao wamepata hali hii wanapaswa kuongea na daktari kuhusu njia za kuzuia kiharusi.

Dalili za ugonjwa wa kiharusi

Dalili za kiharusi cha muda mfupi hutofautiana baina ya mtu na mtu, lakini dalili zinadumu kwa muda mfupi tu. Mara nyingi dalili hudumu chini ya saa moja lakini huweza kudumu hadi masaa 24. Dalili za kiharusi cha aina hii ni pamoja na:

  • Kupoteza uwezo wa kuona
  • Kutoweza kuongea vizuri au shida ya kupata maneno
  • Udhaifu wa uso, mkono au mguu

Mabadiliko ya muda mfupi ya kitabia, kumbukumbu na mwenendo pia huweza kutokea.

Vihatarishi vya kiharusi cha muda mfupi

Kiharusi cha muda mfupi husababishwa pale mishipa ya damu kwenye ubongo inapoziba kwa muda mfupi. Hii husababisha upande wa ubongo kutopata oksijeni ya kutosha na kusababisha dalili.

Hali hii inaweza kuathiri mtu yoyote lakini hutokea zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 60. Magonjwa mengine, hasa kuwa na shinikizo la juu la damu, kisukari, hitilafu za mapigo ya moyo au kiwango kikubwa cha kolesteroli mwilini humweka mtu kwenye hatari ya kupata hali hii. Watu wanaovuta sigara au wenye ndugu waliopata kiharusi pia wapo kwenye hatari ya kupata hali hii.

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na dalili na uchunguzi wa mfumo wa neva. Baada ya kiharusi cha muda mfupi, vipimo vinaweza kufanywa ili kuchunguza vitu vinavyomweka mtu kwenye hatari ya kupata kiharusi hivi karibuni.

Hii hujumuisha vipimo vya damu, uchunguzi wa mishipa ya damu ya shingo kwa ultrasound na ikiwezekana MRI au CT ya kichwa.

Tiba ya kiharusi

Matibabu ya kiharusi hujumuisha kutumia dawa za kufanya damu iwe nyembamba. Kuwa na kiharusi cha muda mfupi huongeza hatari ya kupata kiharusi kwa hiyo ni muhimu kutibu magonjwa mengine kama vile shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha kolesteroli mwilini, hitilafu za mapigo ya moyo na kisukari.

Kinga ya kiharusi

Mabadiliko ya mienendo ya maisha kama vile kula vyakula vyenye manufaa kiafya, kufanya mazoezi kila siku, kuacha kuvuta sigara na kupunguza matumizi ya pombe huweza kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi cha muda mfupi na kiharusi kwa ujumla.

Udhibiti mzuri wa shinikizo la damu, kiwango cha kolesteroli na kisukari husaidia kuzuia hali hii. Watu wenye magonjwa yanayoongeza uwezekano wa damu kuganda kwenye moyo kama vile hitilafu za mapigo ya moyo wanapaswa kuzingatia kutumia dawa za kufanya damu iwe nyembamba.

Ubashiri

Kiharusi cha muda mfupi hakisababishi madhara ya kudumu kwenye ubongo. Hata hivyo hali hii ni ishara ya kuwa kuna hatari kubwa ya kupata kiharusi hivi karibuni. Watu wenye hali hii wanapaswa kumuona daktari na kushauriwa hatua za kuchukua ili kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi.


Washirikishe wengine kwenye makala hii: