1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Mimba kuharibika

Mimba kuharibika

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Kuharibika kwa mimba ina maana gani?

Kuharibika kwa mimba ni changamoto ya kawaida kutokea katika miezi ya mwanzo ya ujauzito, ambapo kiinitete (embryo) au kijusi kinachokua hufa tumboni, kwa sababu za kimaumbile au kwa sababu ya mambo mengine, kama vile matumizi ya baadhi ya dawa, ambazo hazifai kutumiwa wakati wa ujauzito. Neno ‘mimba kuharibika’ au kwa Kiingereza ‘miscarriage’ hutumika kuelezea hali husika inapotokea katika wiki 20 za mwanzo za ujauzito. 

Hali ya kuharibika kwa mimba inayotokea katika miezi mitatu ya mwanzo (wiki ya 1 - 12 ya ujauzito) hufahamika kama kuharibika kwa mimba mapema (early miscarriage). Hali ya kuharibika kwa mimba inayotokea  katika miezi mitatu ya pili (wakati wa wiki 13 - 20 ya ujauzito) kufahamika kama kuharibika kwa mimba kulikochelewa (late miscarriage). Hali ya kufa kwa kijusi tumboni ambayo hutokea baada ya wiki ya 20 ya ujauzito hufahamika kama uzazimfu (stillbirth), yaani mtoto huzaliwa akiwa amekufa. 1

Dalili za mimba kuharibika ni pamoja na kutokwa na damu ukeni, maumivu ya misuli na tumbo, lakini pia inawezekana kuharibika kwa mimba kusiwe na dalili zozote, na mimba nyingi zinazoharibika hutambuliwa kwa kipimo cha ultrasound wakati wa uchunguzi wa kawaida. Watu wengi huwa na hali ngumu kisaikolojia baada ya mimba kuharibika, hasa ikiwa hali hiyo imetokea wakati wa ujauzito uliopangwa. Takriban asilimia 20 ya wanawake, ambao huharibikiwa na mimba, huwa na dalili za sonona na wasiwasi, ambazo njia mbalimbali za matibabu ya kukabiliana nazo zinapatikana. Kwa watu wengi, huzuni inayohusishwa na kuharibika kwa mimba huanza kupungua karibu miezi 4 baada ya kuharibika kwa mimba. 2

Dalili za kuharibika kwa mimba

Uwezekano wa dalili za kuharibika kwa mimba kwa ujumla ni sawa, iwe hali hiyo imetokea katika miezi mitatu ya mwanzo (kuharibika kwa mimba mapema) au katika miezi mitatu ya pili (kuharibika kwa mimba kulikochelewa). Inawezekana pia mimba kuharibika bila mtu kuwa na dalili yoyote, na baadhi ya mimba zinazoharibika hugundulika tu wakati wa uchunguzi wa kawaida wa afya ya mjamzito. Hali hiyo ikitokea, kwa kawaida huwa kuna dalili zifuatazo

  • Maumivu ya tumbo
  • Kutokwa na damu ukeni
  • Kutokwa majimaji au chembechembe za damu ukeni
  • Kukaza kwa misuli ya tumbo (cramping)
  • Kutokuwa tena na dalili za ujauzito, kama vile kupungua kichefuchefu au maumivu ya kichwa na matiti kuuma yakiguswa.

Mtu anayekabiliwa na hali ya mimba kuharibika anaweza kuwa na uwezekano wa dalili moja au zaidi, lakini uwepo wa dalili hizo hauashirii kila wakati kwamba hali ya kuharibika kwa mimba inatokea: inawezekana pia kuwa na mojawapo ya dalili husika kama sehemu ya ujauzito wenye afya, au dalili hizo zinaweza kuwepo kutokana na tatizo lingine ambalo halihusiani na kuharibika kwa mimba.

Sababu nyingine za uwepo wa dalili za kuharibika kwa mimba ni pamoja na:

  • Kutokwa na damu kidogo ukeni (implantation bleeding). Hali hii hutokea katika baadhi ya mimba wakati yai lililorutubishwa (tungwa mimba) hushikamana na utando wa tumbo la uzazi.
  • Mimba inayoendelea kukua vizuri kiafya. Maumivu, kukaza kwa misuli ya tumbo, kutokwa damu ukeni, kutokwa majimaji ni dalili za kawaida za ujauzito wa miezi ya mwanzo. Hata hivyo, kutokwa na damu ukeni sambamba na maumivu ya tumbo au kukaza kwa misuli ya tumbo kunaweza kuashiria kuharibika kwa mimba kuliko uwepo wa mojawapo ya dalili hizi pekee.
  • Mimba nje ya tumbo la uzazi (ectopic pregnancy). Pia hufahamika kama mimba nje ya mirija (tube pregnancy). Hali hii hutokea wakati kiinitete kinapotunga nje ya tumbo la uzazi. Kama ilivyo kwa kuharibika kwa mimba, maumivu ya tumbo na kutokwa na damu ukeni ni dalili kuu mbili za mimba iliyotungwa nje ya tumbo la uzazi.
  • Hali isiyo ya kawaida wakati wa ujauzito (molar pregnancy). Hii hutokea wakati uvimbe wa seli zisizo za kawaida hukua kwenye tumbo la uzazi, badala ya kiinitete chenye afya. Kama ilivyo kwa kuharibika kwa mimba, kutokwa na damu ukeni ni dalili kuu ya ujauzito ambao seli zisizo za kawaida zimekua kwenye tumbo la uzazi.

Watu wengi huwa na wasiwasi kwamba wanakabiliwa na hali ya kuharibika kwa mimba ikiwa dalili zozote zinazohusiana na hali hiyo zikitokea, hasa kutokwa na damu ukeni na inashauriwa kutafuta msaada wa matibabu haraka ili kufanyiwa uchunguzi ikiwa kuna tatizo. Mtu anaweza kufanyiwa uchunguzi wa ujauzito wa miezi ya mwanzo kwa kipimo cha ultrasound ili kubaini ikiwa kweli anakabiliwa na hali ya mimba kuharibika, na kugundua matatizo mengine yoyote ya kiafya yanayohusiana na ujauzito. Watu wanaokabiliwa na dalili zinazoweza kuhusishwa na kuharibika kwa mimba wanaweza pia kufanya tathmini ya dalili kwa kutumia app yetu ya afya bila malipo.  

Aina za kuharibika kwa mimba

Aina ya kuharibika kwa mimba hutegemea mambo haya yafuatayo: 3

  • Ni wakati gani katika kipindi cha ujauzito wa kawaida kuharibika kwa mimba hutokea
  • Ikiwa kuharibika kwa mimba kunahusisha kuathirika kwa chembe zote za ujauzito au sehemu ya ujauzito huo, kifuko cha tumbo la uzazi, au utando wa pembezoni mwa kifuko, ambao huifadhi kijusi kinachokua katika tumbo la uzazi
  • Ni mara ngapi mhusika amekabiliwa na hali ya kuharibika kwa mimba

Aina kuu za kuharibika kwa mimba ni:

  1. Kuharibika kwa mimba mapema, yaani katika miezi mitatu ya mwanzo (first trimester) ya ujauzito
  2. Kuharibika kwa mimba kunakochelewa, yaani katika miezi mitatu ya pili (second trimester)
  3. Kuharibika kwa mimba kwa mara kwa mara, yaani kwa zaidi ya mimba 3 mfululizo

Ujauzito unaofahamika kitaalam kama wa kikemikali (chemical pregnancy), yaani ule ujauzito ulio katika hatua ya mwanzo sana, ambayo kabla hata kipimo cha ultrasound hakijaweza kubaini kijusi.

Kuharibika kwa mimba mapema

Hali ya kuharibika kwa mimba ambayo hutokea katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo (wakati wa wiki 12 za mwanzo za ujauzito) hufahamika kama kuharibika kwa mimba mapema. Hii ndiyo aina ya kawaida ya kuharibika kwa mimba na mara nyingi husababishwa na kasoro za kromosomu (kasoro zinazohusiana na DNA ya kijusi) au kasoro zinazoathiri kondo (placenta). 

Kuharibika kwa mimba kulikochelewa

Hali ya kuharibika kwa mimba ambayo hutokea katika miezi mitatu ya pili (wakati wa wiki 13 - 20 za ujauzito) hufahamika kama kuharibika kwa mimba kulikochelewa. Hali hii hutokea mara chache sana kuliko kuharibika kwa mimba mapema, na mara nyingi husababishwa na: 

  • Matatizo ya kiafya yanayotokana na kasoro katika tumbo la uzazi au mlango wa tumbo la uzazi
  • Mbinu vamizi za kugundua magonjwa ya kijusi
  • Protini ya damu ya mwanamke mjamzito kutoendana na ya mtoto, na kusababisha mfumo wake wa kinga kukabiliana na kuharibu seli za damu za mtoto (rhesus isoimmunisation)
  • Matatizo ya kiafya ya muda mrefu (sugu) yanayomuathiri mjamzito, kama vile ugonjwa unaoathiri utendaji wa kawaida wa ovari ya mwanamke, ambao kitaalamu hufahamika kama polycystic ovarian syndrome
  • Mjamzito kuambukizwa magonjwa, ambayo yanaweza kuwa ni yale yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana; kwa mfano klamidia
  • Maambukizi kutokana na kula chakula kisichofaa (food poisoning) chenye bakteria wa aina fulani kama vile salmonella, toxoplasmosis na listeria

Kuharibika kwa mimba mara kwa mara

akriban mtu 1 kati ya 100 hukabiliwa na hali ya mimba kuharibika mara kwa mara, yaani mimba kuharibika mara tatu au zaidi kwa mfululizo. 4 Watu wanaokabiliwa na hali hii mara kwa mara wanaweza kufanyiwa vipimo ili kubaini ikiwa kuna sababu ya msingi. Kwakuwa uwezekano wa mtu kuharibikiwa na mimba huongezeka kwa kadiri umri unavyoongezeka, mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 35 hufanyiwa vipimo hivi baada ya mimba ya miezi mitatu ya mwanzo kuharibika mara mbili. 

Sababu ya (za) msingi za kuharibika kwa mimba zitatibiwa itakapowezekana. Hata hivyo, sababu huwa haibainiki kila wakati baada ya vipimo kufanyika. Kutokubainika kwa sababu ya kuharibika kwa mimba mara kwa mara si kwamba ni jambo baya: watu wengi wanaokabiliwa na hali ya mimba kuharibika mara kwa mara bila sababu dhahiri huishia kuwa na ujauzito wenye maendeleo mazuri kiafya wakati mwingine wanapokuwa katika hali hiyo, bila kuhitaji matibabu zaidi. 5

Ujauzito wa kikemikali

Mimba nyingi zinazoharibika hutokea mapena sana katika hatua za ujauzito, kabla hata ya mtu kufahamu kwamba alikuwa amepata mimba. Hali hii hufahamika kitaalam kama chemical pregnancy, na hutokea takriban wiki ya 5 ya ujauzito - kwa kawaida kabla ya dalili za ujauzito kujitokeza na mara nyingi kabla ya kiinitete kinachochipukia kuweza kuonekana kwa kipimo cha ultrasound. Baadhi ya watu, hasa wale wanaojaribu kupata mimba, wanafahamu wakati mimba ikiwa kwenye hatua ya kikemikali, kwani inaweza kugundulika katika hatua hii ya awali kwa kutumia kipimo cha kubaini ujauzito. Katika ujauzito wa kikemikali, yai linalorutubishwa hushindwa kuishi kwenye tumbo la uzazi. Baada ya mimba kuharibika, vipimo vya kubaini ujauzito husika vitakavyofanyika baada ya hapo vitakuwa na matokeo hasi. Inawezekana kwa mtu aliye na ujauzito wa kikemikali kutofahamu kuhusu ujauzito na kuharibika kwa ujauzito husika, hasa ikiwa mtu hakuwa akijaribu kupata ujauzito. Hali hii huweza kutokea kwasababu dalili kama vile maumivu ya tumbo na/ au kupungukiwa damu zinaweza kuonekana kuwa sehemu ya hedhi yao inayofuata.   

Ni vyema kufahamu: Aina nyingi za uzazi wa mpango (njia za kuzuia mimba), kama vile kidonge kilichochanganywa au kidonge chenye projesteroni tu (mini) hufanya kazi ya kupunguza utando wa tumbo la uzazi. Dawa hizi kwa kawaida hutumika kwa makusudi ili kuzuia ujauzito. Njia mojawapo ya kufanya hivyo ni kuzuia yai lililorutubishwa kupandikizwa kwenye utando wa tumbo la uzazi. Wakati yai lililorutubishwa halipandiki kwasababu ya matumizi ya njia bora za uzazi wa mpango, hii haihesabiki kuwa ni ujauzito wa kikemikali.  

Mambo hatarishi yanayosababisha kuharibika kwa mimba

Sababu zifuatazo huenda zisiwe sababu pekee kwa mtu anayekabiliwa na hali ya kuharibika kwa mimba, lakini ni sehemu ya vihatarishi vikubwa katika kuharibika kwa mimba:

  • Kuwa na umri wa zaidi ya miaka 35
  • Uvutaji wa sigara au tumbaku
  • Unywaji wa pombe
  • Kutumia zaidi ya 200 mg za kafeini kwa siku (kikombe kimoja au viwili)
  • Matumizi mabaya ya dawa za kulevya 
  • Kuwa na uzito kupita kiasi
  • Kuwa na magonjwa fulani sugu, kama vile kisukari
  • Kuwa na baadhi ya maambukizi ya bakteria na virusi, kama vile klamidia au salmonella

Ingawa machapisho mengi yanaonyesha kimakosa kwamba unywaji wa pombe kiasi unaweza kukubalika wakati wa ujauzito, lakini kwa mujibu wa Miongozo ya Lishe ya 2015 - 2020 inayokubalika na wengi, watu ambao ni wajawazito au wanaoweza kuwa wajawazito hawapaswi kunywa kiasi chochote cha pombe.

Tunza makala ya ujauzito yenye afya >>

Utambuzi

Utambuzi wa kuharibika kwa mimba mara nyingi hufanywa kulingana na dalili, kama vile kutokwa damu ukeni na maumivu ya tumbo, pamoja na mchanganyiko wa vipimo. Vipimo hivi huweza kujumuisha vifuatavyo:

  1. Kipimo cha gonadotropini ya korionik ya binadamu (hCG)
  2. Uchunguzi wa  fupanyonga (pelvis
  3. Kipimo cha ultrasound
  4. Uchunguzi wa moyo wa kijusi

Ni muhimu kwa daktari au madaktari wanaohusika katika kuchunguza kuharibika kwa mimba kuwa na uhakika kwamba kijusi hakiko hai. Uhakiki huu unaweza kuhusisha baadhi ya vipimo tajwa au vyote na/ au kusubiri hadi muda wa wiki kati ya uchunguzi wa kwanza na wa mwisho, ili kukamilisha utambuzi. Muda huu wa kusubiri kabla ya kuthibitisha utambuzi inawezakana kuwa mgumu kisaikolojia. Hata hivyo, vipimo vya utambuzi vinafanyika kwa njia hii ili: 

  • Kupunguza uwezekano wowote wa kufanyika makosa katika utambuzi
  • Kuhakikisha kwamba matibabu yoyote hayatafanyika katika namna itakayohatarisha usalama wa mimba inayoendelea kukua

Katika miezi mitatu ya pili ya ujauzito (katika kipindi cha kuharibika kwa mimba kulikochelewa), kuna uwezekano kukawa hakuna haja ya vipimo ili kuthibitisha utambuzi. Kuharibika kwa mimba kunaweza kuthibitishwa kwa uwepo wa dalili zinazojumuisha:

  • Maumivu ya tumbo
  • Kutokwa damu
  • Kutoa mfuko wa ujauzito unaotambulika au chembe inayotambulika kuwa na uhusiano na ujauzito
  • Kuzaa kijusi (kisicho hai) 

Katika tukio la namna hii, vipimo kama vile vya uchunguzi wa maiti (autopsy) kwenye chembe za ujauzito au uchunguzi wa kondo unaweza kufanyika ili kusaidia kubainisha uwezekano wa visababishi vya kuharibika kwa mimba. 6

Kipimo cha hCG 

Gonadotropini ya korionik ya binadamu (hCG) ni homoni inayozalishwa na kondo wakati wa ujauzito. Kipimo hiki kinaweza kuwa:

  • Uchunguzi wa uwepo wa homoni ya hCG. Uchunguzi huu hufanyika ili kugundua ikiwa kuna homoni ya hCG katika damu au hakuna, na hivyo kuthibitisha kuwepo au kutokuwepo kwa ujauzito. Hiki ni kipimo cha mkojo na mara nyingi ni kipimo kinachotumika katika hatua za awali kubaini ikiwa mtu ni mjamzito. 
  • Uchunguzi wa kubaini kiwango cha homoni ya hCG. Uchunguzi huu hufanyika ili kujua kiasi sahihi cha hCG katika damu. Hiki ni kipimo cha damu ambacho hufanywa na daktari ili kupata taarifa zaidi kuhusiana na ujauzito husika. Uchunguzi unaweza kurudiwa baada ya siku au wiki ili kuhakikisha ikiwa viwango vya homoni ya hCG vya mtu vinaongezeka, pungua, au imarika. 

Katika ujauzito wenye maendeleo mazuri kiafya, viwango vya homoni ya hCG  huendelea kuongezeka maradufu katika damu wakati wa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, na kufikia kilele chake ifikapo karibu na wiki ya 11 ya ujauzito na kupungua kidogo katika kipindi cha miezi mitatu ya pili ya ujauzito. Ikiwa viwango vya homoni ya hCG vinaanza kupungua katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, hii inawezekana kuwa ni ishara ya kuharibika kwa mimba. 

Pale inapowezekana, kipimo cha hCG hufanywa sambamba na uchunguzi wa ultrasound, uchunguzi wa moyo wa kijusi, na uchunguzi wa fupanyonga kabla ya kuthibitisha kuharibika kwa mimba. Hata hivyo, katika matukio ambayo hakuna kifaa cha ultrasound, kipimo cha damu cha hCG kinaweza kuwa njia kuu ya kuthibitisha utambuzi unaoshukiwa wa kuharibika kwa mimba. 6

Uchunguzi wa fupanyonga

Uchunguzi wa fupanyonga ili kutambua kuharibika kwa mimba hufanywa na daktari wa masuala ya uzazi (obstetrician), yaani daktari aliyebobea katika mambo ya uzazi (wakati wa kujifungua mtoto), na/ au daktari wa magonjwa ya wanawake (gynecologist), yaani daktari aliyebobea katika mfumo wa uzazi wa mwanamke.

Wakati wa uchunguzi wa fupanyonga, mtu huvaa gauni la hospitali linalompa uhuru wa kujisogeza, na kulala chali, huku miguu yake ikiinuliwa juu kwa kifaa maalum, ili uke na mlango wa tumbo la uzazi (cervix) viweze kuchunguzwa kwa urahisi. Wakati wa utambuzi wa kuharibika kwa mimba, daktari atakagua uwepo wa ishara kuu mbili zinazoashiria kuharibika kwa mimba, ambazo ni: 

  • Uwepo wa chembe/damu kwenye mlango wa tumbo la uzazi/uke
  • Kufunguka (kutanuka) kwa mlango wa tumbo la uzazi

Kipimo cha Ultrasound

Ultrasound ni mbinu ya upigaji picha ambayo hutumia mawimbi ya sauti kuunda picha ya kijusi kinachokua katika tumbo la uzazi la mjamzito. Ni taratibu isiyo na maumivu na isiyohusisha upasuaji ambayo inaweza kufanyika kwa kutumia skena kwa njia mbili tofauti, yaani: 7

  • Kupitia uke (transvaginal), kwa kawaida kabla ya wiki ya 11 ya ujauzito. Katika utaratibu huu, kifaa cha skena huingizwa ukeni.
  • Kupitia tumbo (transabdominal), kwa kawaida kuanzia wiki ya 11 - 12 ya ujauzito. Jeli maalum hupakwa kwenye ngozi ya sehemu ya chini ya tumbo, na skena hupitishwa juu ya eneo hilo.

Katika utambuzi wa kuharibika kwa mimba, madaktari watazingatia viashiria mbalimbali kwenye picha za ultrasound. Picha hizi zinaweza kuonyesha hatua iliyofikia hali ya kuharibika kwa mimba na ni aina gani ya kuharibika huko inayotokea. Viashiria vya kuharibika kwa mimba vinaweza kujumuisha:

  • Mfuko wa ujauzito ulio tupu katika tumbo la uzazi
  • Uwepo wa chembe za ujauzito lakini hakuna kijusi katika tumbo la uzazi
  • Kijusi au kiinitete ni kidogo kuliko ipasavyo kwa hatua hii ya ujauzito
  • Hakuna mapigo ya moyo wa kijusi, ikiwa ujauzito umefikia hatua ya kubainika, kwa kawaida baada ya wiki 7 za ujauzito

Uchunguzi wa moyo wa kijusi

Kutokuwepo kwa mapigo ya moyo wa kijusi (mapigo ya moyo ya mtoto) ni sababu kuu katika utambuzi wa kuharibika kwa mimba. Uchunguzi wa moyo wa kijusi ni aina maalum ya uchunguzi kwa ultrasound. Moyo wa kijusi unaweza kuchunguzwa kwa njia ya ultrasound kuanzia takriban wiki 7 za ujauzito. Kuanzia wiki 13 - 14, sehemu 4 za moyo na mishipa mikubwa inaweza kuonekana dhahiri, na matatizo mengi ya moyo pia yanaweza kubainika katika hatua hii. 8

Kama ilivyo kwa uchunguzi wa kawaida wa ultrasound, uchunguzi wa moyo wa kijusi ni utaratibu usio na maumivu na usiohusisha upasuaji, ambao unaweza kufanyika kwa njia ya uke au tumbo. 9

Matibabu

Ikiwa hali ya kuharibika kwa mimba inasababisha maumivu ya tumbo, dawa sahihi za kupunguza maumivu zitapendekezwa, na daktari wako atashauri kipimo sahihi. Ni muhimu kutotumia dawa yoyote, hata dawa za kupunguza maumivu, ambazo hazijaidhinishwa na daktari. 

Matibabu hutegemea aina ya kuharibika kwa mimba: 10

  • Baadhi ya hali za kuharibika kwa mimba hazihitaji matibabu ya kimwili, kwasababu hakuna chembe za ujauzito zilizobaki katika tumbo la uzazi. Hali hii hufahamika kama kuharibika kwa mimba kikamilifu.
  • Katika hali ya kuharibika sehemu fulani ya mimba, baadhi ya chembe za ujauzito hutoka kwenye tumbo la uzazi, lakini baadhi hubakia. Matibabu yanaweza kuhitajika ili kuondoa chembe zilizosalia kwenye tumbo la uzazi
  • Katika hali ya kuharibika mimba changa (missed miscarriage), kwa kawaida huwa hakuna maumivu wala damu, na kijusi kilichokufa hubakia ndani ya tumbo la uzazi. Wakati mwingine, chembe za ujauzito hutoka kwenye tumbo la uzazi, lakini aina fulani ya matibabu huweza kuhitajika ili kuondoa masalia ya kijusi. 

Katika hali ya kuharibika kwa mimba kikamilifu, na bila kupoteza damu nyingi, hakuna matibabu zaidi au upasuaji unaohitajika. Mtu husika atapewa maelezo rahisi ya namna ya kujihudumia. Pia atashauriwa kutoshiriki tendo la kujamiiana au kutoingiliwa ukeni kwa namna yoyote ile hadi pale damu inayohusishwa na kuharibika kwa mimba itakapoacha kutoka (kwa kawaida huchukua kipindi cha wiki 2 baada ya mchakato kuanza). Vipindi vya hedhi ya kawaida hurejea wiki 4 - 6 baada ya kuharibika kwa mimba. 

Katika hali ya kuharibika sehemu fulani ya mimba au kuharibika kwa mimba changa, utaratibu wa upasuaji au matibabu yanaweza kufanyika katika baadhi ya matukio ili kusafisha tumbo la uzazi kwa kuondoa chembe zote za kijusi na ujauzito. Inapowezekana, mapendekezo ya hatua za matibabu huachiwa aamue mtu aliyepoteza ujauzito. Utafiti uliofanyika na jarida la kitiba la "American Family Physician" ulionyesha kwamba matokeo bora ya afya ya akili baada ya kuharibika kwa mimba yanaweza kutarajiwa kuwepo ikiwa mapendekezo ya matibabu ya mtu aliyepoteza ujauzito yanaheshimiwa na kutekelezwa. Hali ya kuharibika kwa sehemu fulani ya mimba au kuharibika kwa mimba changa inaweza kudhibitiwa kwa njia ya kutarajia, kitiba, au kiupasuaji. 

Kuzuia kuharibika kwa mimba

Katika matukio mengi, haiwezekani kuzuia kuharibika kwa mimba. Hata hivyo, inawezekana kupunguza hatari ya kuharibika kwa mimba kuongeza uwezekano wa kutibu matatizo yoyote ya wakati wa ujauzito ambayo hutokea kabla ya kusababisha kuharibika kwa mimba. Hali hii huitaji utunzaji mzuri wa ujauzito, yaani mpango wa utunzaji wa ujauzito kabla ya kujifungua (antenatal care) ulioandaliwa na daktari wa mjamzito husika ili kuongeza uwezekano wa ukuaji wa ujauzito wenye afya.  

Utunzaji wa ujauzito kabla ya kujifungua kwa ujumla uhusisha: 

  • Kuwa na uchunguzi wa kitiba mara kwa mara ili kujua afya ya mjamzito na mtoto anayekua katika tumbo la uzazi
  • Kuepuka unywaji pombe, uvutaji sigara, na unywaji kafeini kupita kiasi na mambo mengine yanayohusishwa na hatari ya kuharibika kwa mimba 
  • Kuepuka mazingira na hali zinazohusishwa na ongezeko la hatari ya kuharibika kwa mimba
  • Kula mlo uliopendekezwa kwa wenye ujauzito
  • Kuhakikisha kwamba matatizo ya kiafya (pre-existing medical conditions) aliyonayo mjamzito ambayo yanaweza kuathiri ujauzito yanadhibitiwa ipasavyo kabla ya mimba kutungwa ili kupunguza athari zake kwa ujauzito  

Ikiwa una mpango wa kuwa mjamzito na unadhani kuwa unaweza ukawa na tatizo la kiafya ambalo halifanyiwa utambuzi kutokana na kukabiliwa na dalili zisizoeleweka, unaweza kufanya tathmini ya dalili bila malipo kwa kupakua app ya afya.

Hitimisho

ngawa tukio la kuharibika kwa mimba linaweza kuwa jambo la kuhuzunisha sana kwa mtu binafsi au wanandoa, kuelewa sababu zake, dalili zake, na njia za matibabu zinazopatikana kunaweza kutoa kiasi fulani cha faraja na utayari. Kufuata mapendekezo ya kupunguza hatari kupitia utunzaji wa kina wa ujauzito pia kunaweza kuwa muhimu katika kusaidia ukuaji wa ujauzito wenye afya. Kupata maarifa kuhusu hali ya kuharibika kwa mimba na udhibiti wake huwawezesha watu binafsi na kutoa mwanga juu ya umuhimu wa kuijadili na kuikabili mada hii ambayo mara nyingi ni mwiko kuijadili, huimiza mazungumzo ya wazi zaidi na yenye kuleta matumaini kuhusiana na suala la kuharibika kwa mimba.

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)

S: Je, papai linaweza kusababisha kuharibika kwa ujauzito ulio katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo?
J: Hofu ya kawaida miongoni mwa wanawake wajawazito ni usalama katika ulaji wa papai. Papai ambalo halijaiva au limeiva kiasi lina utomvu, ambao unaweza kusababisha kusinyaa kwa misuli ya tumbo la uzazi, na hivyo kusababisha uwezekano wa hatari katika ujauzito ulio katika hatua ya miezi mitatu ya mwanzo, pamoja na kuharibika kwa mimba. Hata hivyo, mapapai yaliyoiva kabisa kwa ujumla huesabika kuwa salama kuliwa wakati wa ujauzito. Daima wasiliana na mtoa huduma ya afya kwa ushauri (kulingana na hali yako) kuhusu lishe wakati wa ujauzito. 

S: Nini hutokea baada ya kuharibika kwa mimba?
J: Baada ya kuharibika kwa mimba, mwili wa mwanamke hupitia mabadiliko mbalimbali ya kimwili na kihisia. Kimwili, inaweza kuchukua muda wa wiki kadhaa kwa mizunguko ya hedhi kuwa ya kawaida na viwango vya homoni kutengemaa. Wanawake wanaweza pia kutokwa na damu na kubanwa misuli, sawa na dalili wanazokuwa nazo wakati wa vipindi vya hedhi. Katika suala la kihisia, kwa kawaida wanawake huhisi huzuni, masikitiko, na kupoteza, na ukubwa na muda wa uwepo wa hisia hizi hutofautiana miongoni mwa watu. Ni muhimu kupata ushauri wa kitiba kwa ajili ya kupona kimwili na kuzingatia ushauri wa vikundi vya msaada kwa ajili ya kupona kihisia. Kumbuka, ni muhimu kujipa muda wa kuhuzunika na kupona kimwili na kihisia. 

Q: Ni muda gani baada ya kuharibika kwa mimba mtu anaweza kujamiiana na/ au kujaribu kupata tena mimba?
A: Kwa watu wengi, kutokwa na damu ukeni kunakohusiana na kuharibika kwa mimba hudumu kwa kipindi cha chini ya wiki 2. Katika kipindi hiki cha kutokwa damu ukeni, tumbo la uzazi na mlango wa tumbo la uzazi vinaweza kubaki vimetanuka. Hali hii huweka eneo la uke katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya bakteria. Hatari ya kuambukizwa inaweza kupunguzwa kwa kuepuka tendo la kujamiiana mpaka pale damu itakapoacha kutoka. Baada ya kuharibika kwa mimba, inapendekezwa kusubiri mpaka baada ya hedhi inayofuata kwisha kabla ya kujaribu tena kupata mimba. Inawezekana kupata mimba mara tu yai jipya linapochomoza na kurutubishwa na manii (mbegu za kiume), hali ambayo inaweza kutokea mara tu mzunguko mpya wa uzazi unapoanza katika mwili wa mwanamke. Hivyo basi, ingawa inawezekana kuwa mjamzito mara tu baada ya kuharibika kwa mimba, kusubiri hadi hedhi inayofuata inapendekezwa kwa sababu 2 kuu, ambazo ni: kuongeza uwezekano wa kupanga kwa usahihi muda wa mimba mpya, na inaruhusu tumbo na mlango wa uzazi kurudi katika hali zao za kawaida baada ya kuharibika kwa mimba, kusaidia kuhakikisha uwepo wa mazingira salama kwa ukuaji wa kijusi katika tumbo la uzazi.