1. Ada
 2. Editorial
 3. Tiba & afya
 4. Ufahamu wa afya ya akili ya wanaume

Ufahamu wa afya ya akili ya wanaume

Mfano wa mtu akizungumza na mtaalam wa tiba kuhusu afya yake ya akili

Uzoefu wako katika suala la afya ya akili unaweza kutegemea maumbile yako, uzoefu wa maisha, hali ya kijamii na kiuchumi, jinsia, na mengineyo. Kwa ufupi, huwa ni tofauti kwa kila mtu. 

Kwa wanaume wengi, kuelewa na kudhibiti afya ya akili kunaweza kuwa ni suala lenye changamoto za kipekee. 

Hivyo basi, tujifunze kuhusu afya ya akili ya wanaume, kwanini hatuizungumzii vya kutosha, na nini unaweza kufanya ili kuendelea kuidhibiti afya yako ya akili na kujali hali za wanaume katika maisha yako.

Vielelezo vya afya ya akili ya wanaume

Utafiti wa mwaka 2019 ulikadiria kuwa 24.5% ya wanawake walipata matatizo ya afya ya akili ikilinganishwa na 16.3% ya wanaume.1  

Kwa kuangalia takwimu hizi, inaonekana kana kwamba wanaume wachache zaidi wanaishi na matatizo ya afya ya akili.

Lakini tunapoangalia kwa karibu zaidi, tunaona kwamba takwimu hizi hazielezei tatizo kikamilifu: 

 • 76% ya matukio ya kujiua nchini Uingereza uhusisha wanaume.2
 • Wanaume wana uwezekano karibia mara 3 zaidi kuwa walevi kuliko wanawake.3
 • Wanaume wana uwezekano mkubwa wa kutumia na kufa kutokana na madawa haramu ya kulevya.4

Je, wanaume wanateseka na matatizo ya afya ya akili kimyakimya?

Kwanini wanaume hawazungumzi kuhusu afya ya akili?

Kutokana na uzoefu wangu kama daktari, wanaume hupata ugumu wa kipekee katika kuweka wazi na kujadili afya yao ya akili. Hii mara nyingi husababishwa na mashinikizo ya kijamii na unyanyapaa wa watu wenye matatizo ya akili.

Mawazo ya kizamani kwamba uanaume ni kuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kunaweza kumaanisha kuwa baadhi ya wanaume wanaona kama kutafuta msaada ni udhaifu. Na tunaliona hili kwenye takwimu: Nchini Uingereza, wanaume wanawakilisha  36% tu ya rufaa za huduma zinazohusiana na matatizo ya kisaikolojia.5

Wanaume pia wanaweza kupata wakati mgumu kutambua dalili za matatizo ya afya ya akili zinazowakabili. Kwa maana hiyo, kuna uwezekano mdogo zaidi kwa wao kutafuta msaada pale wanapouhitaji.6

Unaweza kufanya nini?

Vifuatavyo ni vidokezo 6 vya kukusaidia kudhibiti afya yako ya akili na kutunza afya za wanaume katika maisha yako.

Tambua kwamba vidokezo hivi havina manufaa kwa wanaume tu. Vinaweza kukusaidia kutunza afya yako bila kujali jinsia yako. 

Ongea na daktari wako

Ikiwa unakabiliana na dalili za matatizo ya afya ya akili, kamuone daktari. Inaweza ikawa ni suala lenye kuogopesha, lakini ni kazi ya daktari wako kufahamu masuala haya, na ni hatua bora ya kwanza yenye muelekeo wa kukuwezesha kujihisi vizuri zaidi.

Kuwa muwazi

Sisi wote tunapitia hali tofauti tofauti linapokuja suala la afya ya akili, kwahiyo hakuna sababu ya kuhisi aibu kuhusu hilo. Kwa kuzungumza na marafiki, ndugu, na wafanyakazi wenzako kunaweza kukufanya ujihisi vizuri zaidi. Kuwa muwazi pia husaidia kufanya mazungumzo kuhusu afya ya akili kuwa ya kawaida. 

Tumia muda na wapendwa wako

Mahusiano ya karibu na watu wengine ni muhimu sana kwa afya yako ya akili. Hilo lina ukweli hasa kwa watu wanaokabiliwa na tatizo la sonona.7

Fanya mazoezi

Ufanyapo mazoezi mwili hutoa endofini katika ubongo wako ambazo zinaweza kuboresha ustawi wako na kukuwezesha kuwa na afya njema. Mazoezi pia yamethibitishwa kusaidia kukabiliana na dalili za wasiwasi na sonona.8

Jiunge na kikundi kitakachokusaidia kuimarisha afya ya akili

Kuzungumza na watu wengine ambao wanakabiliwa na hali za kimaisha zinazofanana na zako kunaweza kukupa msaada wa kihisia. Pia kutakusaidia kupata maarifa ya kukuwezesha kudhibiti afya yako ya akili na wakati huo huo ukipata marafiki wapya.

Jali hali za wanaume katika maisha yako

Ikiwa una wasiwasi kuhusu rafiki au mwanafamilia, wasiliana naye. Ujumbe mfupi wa kujulia hali unaweza kusaidia sana. Sikiliza kwa makini na jitolee kusaidia. Wahimize kutafuta msaada kutoka kwa mtaalamu wa afya ikiwa wanahitaji na jitolee kuwasindikiza kwenye miadi na mtaalamu husika ikiwa wanaogopa. 

Mwisho, ni muhimu kukumbuka kwamba afya yako ya akili ni muhimu kama ilivyo afya yako ya mwili. Kwahiyo, tenga muda wa kutunza akili yako kama unavyotunza mwili wako.

Mpaka tutakapokutana kwenye makala nyingine, endelea kutunza afya yako.


 1. NIMH. “Mental Illness.” Kimetumika Mei 2021.

 2. Men’s Health Forum. “Key Data: Mental Health.” Kimetumika Mei 2021.

 3. hscic. “Statistics on Alcohol.” Kimetumika Mei 2021.

 4. Substance Abuse and Mental Health Services Administration. “National Admissions to Substance Abuse Treatment Services.” Kimetumika Mei 2021.

 5. NHS Mid Essex CCG. “Men’s Health Week.” Kimetumika Mei 2021.

 6. NIMH. “Men and Depression.” Kimetumika Mei 2021.

 7. Wang, J., et al. BMC Psychiatry, (2018), doi: 10.1186/s12888-018-1736-5.

 8. Cooney, G., et al. JAMA, (2014), doi: 10.1001/jama.2014.4930.

Mwandishi:

Cesare Paolino
Dk. Cesare Paolino

Dk. Paolino ni mmoja wa Wahandisi wetu wa Maarifa ya Kitiba.

Mfasiri:

Rungwe Hashim
Rungwe Hashim

Rungwe ni mwandishi na msimamizi wa maudhui ya Kiswahili ya Ada.