1. Ada
  2. Magonjwa
  3. Vidonda vya tumbo

Vidonda vya tumbo

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Vidonda vya tumbo ni nini?

Vidonda vya tumbo hufahamika kwa kiingereza kama Peptic Ulcer ni hali ambayo kuna kidonda kwenye tabaka la tumbo au sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo. Dalili kuu ni hisia ya kuungua katika sehemu ya juu ya tumbo baada ya kula. Dalili nyingine ni kiungulia, kubeua, tumbo kujaa gesi na kichefuchefu. Dalili za vidonda vya tumbo huongezeka kadiri muda unavyoenda.

Vidonda vya tumbo vinaweza kusababisha madhara ambayo huhitaji huduma ya dharura. Haya hujumuisha kutokwa damu au kuchimbika shimo katika tumbo la chakula. Madhara haya huweza kusababisha dalili kuanza kwa ghafla. Matibabu ya vidonda vya tumbo hutegemea sababu ya hali hii kutokea. Sababu hiyo ikishatambuliwa na kutibiwa, huwa na matokeo mazuri.

Dalili za vidonda vya tumbo

Dalili za vidonda vya tumbo ni pamoja na:

  • maumivu ya sehemu ya juu ya tumbo,
  • kiungulia,
  • kubeua,
  • tumbo kujaa gesi na
  • kichefuchefu. 1

Ikiwa kidonda kinatoa damu, unaweza kuona damu nyekundu au damu ilyovilia (damu nyeusi) kwenye kinyesi. Kutokwa damu kunaweza kuambatanishwa na uchovu na kukosa nguvu. Kama kidonda cha tumbo kinasababisha shimo kwenye utumbo, hii inaweza kusababisha maumivu ya ghafla ya tumbo, homa, kichefuchefu na kuzimia.

Vihatarishi

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo hutokea zaidi kwa watu wazima. Visa vingi husababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobater pylori. Sababu zingine za vidonda vya tumbo ni dawa dhidi ya inflamesheni (kama vile aspirin), unywaji mwingi wa pombe kwa muda mrefu na uvutaji wa sigara. 2

Hivyo basi, kuacha unywaji mwingi wa pombe na uvutaji sigara kunaweza saidia kuepuka madhara ya vidonda vya tumbo, kwani hupunguza uwezekano wa kuvipata. Uwepo wa magonjwa mengine na utumiaji wa dawa nyingine pia huweza kusababisha vidonda vya tumbo, lakini ni nadra sana.

Utambuzi

Utambuzi wa vidonda vya tumbo huweza kuhitajika kufanywa kwa kipimo cha endoscopy (kupitisha kifaa maalum chenye kamera mdomoni hadi tumboni). Vipimo vingine hufanywa wakati wa endoscopy ambavyo vinaweza kutambua chanzo cha vidonda vya tumbo. 3 Maambukizi ya Helicobacter pylori huweza kutambuliwa kwa kipimo cha urea kwenye pumzi.

Matibabu

Tiba ya vidonda vya tumbo huwa ni antibiotiki ambayo hulenga kutibu maambukizi ya bakteria yaliyosababisha vidonda hivyo.

Kama vidonda vya tumbo vimesababishwa na dawa, daktari wako anaweza kukushauri kuhusu hatari na manufaa ya kutumia hizo dawa. Haishauriwi kutumia maziwa mabichi au almaarufu “maziwa fresh” kama tiba ya vidonda vya tumbo. Maziwa hupunguza maumivu ya tumbo kwa muda mfupi lakini husababisha asidi tumboni kuongezeka. 3

Baadhi ya dawa husaidia kupunguza kiwango cha asidi inayozalishwa tumboni. Hizi zinahitajika wakati kidonda bado kinapona. Kama vidonda vinatoa damu au vinasababisha shimo kwenye utumbo, upasuaji wa dharura unaweza kuhitajika. Hii athari hutokea kwa nadra.

Kinga dhidi ya vidonda vya tumbo

Kutumia kwa makini dawa dhidi ya inflamesheni (kama vile aspirin) ni muhimu katika kuzuia vidonda vya tumbo, hasa kwa watu wazima. Kuacha au kupunguza kuvuta sigara huweza kusaidia kupunguza dalili na kuzuia vidonda vipya.

Ubashiri

Ikiwa sababu ya vidonda vya tumbo haijatambuliwa na kutibiwa, dalili huweza kuendelea kwa miezi au miaka. Kwa tiba sahihi, watu wengi hupona vizuri na huwa hawana matatizo endelevu. Inawezekana kuambukizwa tena na bakteria wa Helicobacter pylori, kwa hiyo vidondoa vya tumbo vinaweza kujirudia.