1. Ada
  2. Maambukizi ya awali ya kaswende

Maambukizi ya awali ya kaswende

Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba

Imesasishwa tarehe

Muhtasari

Kaswende ni ugonjwa wa zinaa (STD) unaosababishwa na maabukizi ya bakteria. Kaswende inayotambuliwa katika hatua za awali hujulikana kama hatua ya kwanza ya kaswende (primary syphilis). Hali hii huwaathiri vijana zaidi.

Dalili za awali ni pamoja na vidonda vidogo kwenye sehemu za siri na tezi za limfu kuvimba. Ugonjwa huu huathiri sehemu tofauti za mwili, kwa hiyo dalili za baadaye hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Kutumia kinga wakati wa kujamiiana huweza kupunguza uwezo wa kupata kaswende.

Antibiotiki hutumiwa kutibu maambukizi haya. Kwa matibabu ya mapema na sahihi, watu wengi hupona vizuri.

Jaribu app ya Ada bure kwa tathmini ya awali ya dalili.

Hatari

Kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum. Kama maambukizi hayajatambuliwa na kutibiwa, maambukizi ya kaswende husababisha vipindi vya dalili, na hivi hujulikana kama kaswende ya hatua ya kwanza, ya pili na ya tatu. Inaweza kuchukua miaka kadhaa kutoka hatua ya kwanza hadi ya tatu. Vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24 huathirika zaidi.

Dalili

Dalili za awali za kaswende ni kidonda kwenye sehemu za siri, mdomo au makalio, na tezi za limfu kwenye kinena kuvimba. Dalili hizi kawaida huisha ndani ya wiki kadhaa na mara nyingine dalili hizi zinaweza zisitambulike.

Ugonjwa unavyoendelea, aliyeathirika anaweza kupata vipele, homa, maumivu ya viungo, kupoteza nywele, viuvimbe vidogo kwenye sehemu za siri na maumivu ya misuli. Hatua za baadaye za kaswende huendelea polepole ndani ya miaka, na huathiri moyo, ubongo na sehemu nyingine za mwili. Hii inaweza kusababisha dalili tofauti, kama vile kuishiwa pumzi, kuchanganyikiwa, kusahau, kupoteza uratibu na uharibifu wa neva na vinginevyo.

Utambuzi

Utambuzi hufanywa kulingana na dalili, uchunguzi wa kimwili na vipimo vya damu kwa uwepo wa protini dhidi ya kaswende. Utambulizi mara nyingi hufanywa wakati wa uchunguzi wa kawaida, kwa sababu kaswende inaweza isisababishe dalili zozote, au dalili zisizo za kawaida.

Kama kuna kidonda, sampuli ya majimaji kutoka kwenye kidonda huweza pia kuchunguzwa kwa uwepo wa bakteria. Hamna kipimo kimoja cha kutambua magonjwa yote ya zinaa. Tafadhali ongea na mtaalamu wa afya kwa taarifa zaidi.

Matibabu

Kaswende hutibiwa kwa antibiotiki. Vipimo hufanyika baada ya matibabu ili kuhakikisha maambukizi yametibiwa kikamilifu.

Kinga

Kutumia kinga wakati wa kujamiiana huweza kuzuia maambukizi mapya ya kaswende. Wanawake wajawazito wanapaswa kuchunguzwa (kupimwa bila kuwa na dalili) ili kuzuia kusambaza bakteria hawa kwa mtoto.

Utabiri

Kwa utambuzi na matibabu ya mapema, watu wengi hupona vizuri na hawana matatizo ya kudumu. Kaswende isiyo tibiwa inaweza kusambaa katika sehemu nyingine za mwili, na kusababisha uharibifu wa mishipa ya damu, ubongo na neva.