1. Ada
  2. Editorial
  3. Tiba & afya
  4. Maumivu yangu ya kichwa yana maana gani?

Maumivu yangu ya kichwa yana maana gani?

Mtu anayehisi maumivu ya kichwa akiwa ofisini.

Makadirio yanaonyesha kuwa 96% miongoni mwetu tumeshapatwa na maumivu ya kichwa wakati fulani. 1 Kwa bahati mbaya, huo ndiyo ukweli ulivyo katika maisha. 

Isitoshe, kuelewa kinachosababisha maumivu ya kichwa inaweza kuwa ni changamoto kubwa. Kuna takriban aina 150 tofauti za maumivu ya kichwa, na nyingi kati ya hizo zina visababishi na dalili tofauti. Lakini je, unafahamu kuwa eneo la maumivu ya kichwa linaweza kutoa ishara ya nini kinasababisha maumivu hayo?

Embu tuone baadhi ya aina za kawaida za maumivu ya kichwa, yanaathiri sehemu gani ya kichwa, na yanaweza kuwa na maana gani.

Aina za kawaida za maumivu ya kichwa na maeneo yake

Maumivu ya pande zote mbili za kichwa

Maumivu ya kichwa yanayoathiri pande zote mbili za kichwa huitwa maumivu ya kichwa ya aina ya msongo. Kwa kuwa hii ndiyo aina ya kawaida ya maumivu ya kichwa, inawezekana imeshawahi pia kukutokea.

Watu mara nyingi huelezea maumivu ya kichwa ya msongo kama maumivu yasiyo makali na yenye kubana pande zote mbili za kichwa. Kwa kawaida, hayagongigongi. Badala yake, ni maumivu yalipooza na endelevu. Maumivu ya kichwa ya aina ya msongo kwa kawaida hudumu kwa angalau dakika 30 na yanaweza kuendelea kwa siku kadhaa.

Baadhi ya visababishi vya kawaida vya maumivu ya kichwa ya msongo ni pamoja na:

  • Kutolala vya kutosha
  • Msongo
  • Maumivu ya misuli katika kichwa na shingo
  • Unywaji mwingi wa vinywaji vyenye kafeini

Maumivu ya kichwa ya aina ya msongo mara nyingi huisha yenyewe na kwa kawaida siyo dalili ya ugonjwa fulani.

Upande mmoja wa kichwa

Maumivu ya kipandauso (Migraine)

Kipandauso ni sababu ya kawaida ya maumivu ya kichwa yanayoathiri upande mmoja wa kichwa. Takriban mwanamke 1 kati ya 5 na mwanaume 1 kati ya 15 hupatwa na maumivu ya kichwa ya aina hii. 2

Kipandauso kwa kawaida husababisha maumivu ya kichwa yanayogonga upande mmoja pamoja na dalili nyingine zinazoweza kujumuisha:

  • Kichefuchefu na kutapika
  • Kuathirika kirahisi na mwanga na sauti
  • Ugumu wa kuzingatia mambo

Pamoja na dalili tajwa, baadhi ya watu hupatwa na "aura" pindi wanapokabiliwa na maumivu ya kipandauso. Aura ni mvurugiko wa uwezo wa kuona, kuongea, na kuhisi ambao kwa kawaida hutokea kabla au wakati wa maumivu ya kipandauso. Kwa watu wengi, hali hiyo ni ishara za mwanzo kwamba wanakabiliwa na kipandauso.

Vichocheo vya kipandauso hutofautiana baina ya watu walioathirika. Hata hivyo, kipandauso kinaweza kusababishwa na:

  • Hedhi
  • Msongo
  • Uchovu
  • Baadhi ya vyakula na vinywaji

Maumivu yanaweza kudumu kwa muda wowote kuanzia saa 1 hadi siku 3.

Maumivu ya upande mmoja wa kichwa (Cluster headaches)

Maumivu ya upande mmoja wa kichwa kwa kawaida hutokea mara chache.

Mara nyingi maumivu husika huhisiwa karibu na tundu la jicho, na huwa ni makali ambayo hudumu kwa muda wa kati ya dakika 15 na masaa 3. Yanaweza kutokea mara kadhaa ndani ya siku moja.

Wakati wa shambulizi la maumivu ya upande mmoja wa kichwa, mara nyingi watu huonekana kuwa ni wenye wasiwasi au hasira. Wanaweza kuonyesha dalili zingine pia, zikiwemo:

  • Macho mekundu yenye machozi
  • Kulegea na kuvimba kwa kope 1
  • Kunywea kwa mboni katika jicho 1
  • Kutokwa jasho usoni
  • Kuziba pua upande mmoja au kutokwa kamasi

Haifahamiki hasa ni nini husababisha maumivu makali ya upande mmoja wa kichwa, ingawa inaonekana kuna sababu ya kimaumbile, na watu wanaovuta sigara wanaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi.

Mbele ya kichwa

Maumivu ya kichwa ya sinasi (Sinus)

Maumivu ya kichwa karibu na macho, mashavu, na paji la uso yanaweza kutokea baada ya maambukizi ya virusi, kama vile mafua, au wakati mtu ana homa inayosababishwa na vumbi au mizio.

Maumivu ya kichwa ya sinasi mara nyingi huambatana na dalili nyingine, kama vile:

  • Pua kuziba
  • Kutokwa kamasi puani
  • Uchovu
  • Kupungua uwezo wa kunusa

Kwa kuwa maumivu ya kichwa ya sinasi na kipandauso yana dalili zinazofanana, inawezekana kuyachanganya. Tafiti zinaonyesha kwamba zaidi ya 90% ya maumivu ya kichwa ya sinasi kwa hakika husababishwa na kipandauso. 3 Maumivu ya kichwa ya sinasi kwa kawaida hudumu kwa muda mrefu kuliko maumivu ya kipandauso, na mara nyingi hudumu kwa siku kadhaa kwa wakati mmoja. Pia, baadhi ya dalili za kipandauso, kama vile kichefuchefu na aura, haziambatani na maumivu ya kichwa ya sinasi.

Maumivu ya kichwa yanayosababishwa na kuacha kunywa kafeini

Unaweza kuhisi maumivu eneo la mbele kichwani ikiwa utapunguza ghafla unywaji wako wa kafeini.

Mara nyingi huanza kama maumivu na shinikizo nyuma ya macho, maumivu ya kichwa ya kafeini yanaweza kufika hadi kwenye paji la uso. 

Maumivu ya kichwa yanayosababishwa na kuacha kunywa kafeini siyo makali na huisha baada ya siku chache. Ikiwa unajaribu kupunguza unywaji wa kafeini, ni vizuri kufanya hivyo hatua kwa hatua ili kuepuka kuhisi maumivu ya kichwa yanayosababishwa na kuacha kunywa kafeini.

Kichwa na shingo nzima

Maumivu ya kichwa yanayogonga ghafla kama mlipuko wa radi (thunderclap headaches) huathiri kichwa na shingo nzima. Ni maumivu makali, na watu wanaopata aina hii ya maumivu ya kichwa mara nyingi huyaelezea kama "maumivu ya kichwa mabaya kuliko yote katika maisha yao."

Watu wanaopatwa na maumivu ya kichwa ya "thunderclap" wanaweza pia kuhisi kichefuchefu, kutapika, na kutoshahimili mwanga mkali.

Maumivu ya kichwa ya "thunderclap" inaweza kuwa ni dalili ya kuvuja kwa damu katika ubongo na utando unaozunguka eneo hilo (subarachnoid hemorrhage), ambayo ni hali inayohitaji matibabu ya dharura. Ikiwa unahisi ukabiliwa na maumivu ya kichwa ya aina hii, unapaswa kutafuta msaada wa matibabu ya dharura.

Kutibu maumivu ya kichwa nyumbani

Kuna mambo kadhaa unaweza kufanya ili kupunguza maumivu ya kichwa. Yafuatayo ni mambo machache unayoweza kujaribu:

  • Kunywa maji zaidi.
  • Jaribu kupumzika, kwani msongo unaweza kufanya maumivu ya kichwa kuwa mabaya zaidi.
  • Tumia dawa za kutuliza maumivu, kama vile paracetamol, ibuprofen, au aspirini.
  • Hakikisha unapata usingizi wa kutosha.

Ikiwa unatumia dawa za kutuliza maumivu mara kwa mara ili kupunguza maumivu ya kichwa, unaweza kupata maumivu ya kichwa yanayojirudia mara baada ya dawa kuisha. Ikiwa unahisi maumivu ya kichwa kila mara, nenda kamuone daktari.

Wakati wa kumuona daktari

Kufahamu eneo la maumivu ya kichwa siyo njia inayofaa kwa 100% ya kutambua kinachosababisha maumivu husika. Ikiwa unakabiliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara, dawa za kutuliza maumivu hazisaidii, au maumivu yanaathiri kwa kiasi kikubwa maisha yako, ni wakati wa kwenda kumuona daktari.

Ikiwa unakabiliwa na dalili zifuatazo pamoja na maumivu makali ya kichwa, unapaswa kutafuta msaada wa matibabu ya dharura:

  • Maumivu ya taya wakati wa kula
  • Kuona ukungu au vitu viwili-viwili
  • Maumivu ya ngozi ya kichwa
  • Mikono au miguu kuwa dhaifu au kufa ganzi
  • Kichefuchefu au kutapika
  • Kutostahimili mwanga mkali

Unaweza kuanza kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yako sasa kwa kupakua app ya Ada.


  1. American Journal of Medicine (2017). Headache. Kimetumika tarehe 1 Agosti 2023.

  2. NHS (2022). Migraine. Kimetumika tarehe 1 Agosti 2023.

  3. NIH (2004). New thoughts on sinus headache. Kimetumika tarehe 1 Agosti 2023.x

Mwandishi:

Harry O’Connor
Harry O’Connor

Harry ni Mwandishi wa Ada katika Masuala ya Kisayansi.

Mhakiki wa kitiba:

Dk. Onder Kurtoglu
Dk. Onder Kurtoglu

Dk. Onder Kurtoglu ni meneja wa maudhui ya Kitiba wa Ada

Mfasiri:

Rungwe Hashim
Rungwe Hashim

Rungwe ni mwandishi na msimamizi wa maudhui ya Kiswahili ya Ada.