Kufanya kazi ukiwa nyumbani
Kuna mengi ya kupenda kuhusu kufanyia kazi nyumbani: hakuna kusafiri kwenda na kurudi kutoka kazini, siku za kuvaa pajama za kulalia au kaptura, na kwa wengi wetu, uboreshaji wa utendaji wa kazi. Utafiti wa hivi karibuni uligundua kwamba kufanya kazi katika maeneo ya nje na ofisi (remote work) kuliwafanya watu waboreshe utendaji wao wa kazi kwa 7% zaidi ya wenzao wanaofanyia kazi ofisini.1
Lakini maamuzi ya kufanyia kazi nyumbani yanaweza kuleta changamoto mpya kwa afya yako ya akili na mwili. Kuwa na utaratibu wenye manufaa kiafya, kufanya kazi kwa usalama, na kuendeleza mawasiliano na wafanyakazi wenzako kunaweza kuwa ni shida wakati unafanya kazi maeneo ya nje na ofisi.
Tujifunze ni hatua gani unaweza kuchukua ili kuhakikisha unaendelea kubaki salama, mwenye afya, na mwenye furaha wakati unafanya kazi ukiwa nyumbani.
Endeleza utaratibu
Kutoka nyumbani na kwenda eneo jingine kila siku kwa ajili ya kazi hujenga desturi katika maisha yako, husaidia kudumisha afya bora na ustawi.2 Unapofanyia kazi nyumbani, unahitaji kufanya bidii zaidi ili kuendeleza desturi hizo. Vifuatavyo ni vidokezo vyetu muhimu katika kufanikisha hilo.
Dumisha utaratibu wako wa kawaida wa kulala
Mazoea mazuri ya kulala ni muhimu kwa afya yako ya akili na mwili.3 Kwahiyo ifikapo usiku, jaribu kwenda kulala mapema na hakikisha unatega kengele yako ya saa ili ikuamshe asubuhi.
Vaa kwa ajili ya kazi
Utafiti unaonyesha kwamba watu huboresha utendaji wa kazi wanapokuwa wamevaa nguo zenye maana yenye kuwakilisha jambo fulani (symbolic meaning).4 Hiyo inamaanisha kuvaa kwa ajili ya kazi kunaweza kukusaidia kuongeza tija kazini. Hakuna haja ya kuvaa suti na tai, ila jaribu kuwa na siku maalumu za uvaaji wa pajama za kulalia. Na siku nyingine vaa kama vile unakwenda kazini.
Funga kompyuta yako baada ya kazi
Mipaka thabiti kati ya maisha yako ya kazi na binafsi ni muhimu ili kukuzuia kupata uchovu mwingi. Hivyo basi, hakikisha unaacha kufanya kazi baada ya muda wa kazi na tenga muda kwa ajili yako na maisha yako binafsi.
Fanya kazi kwa usalama
Bila afya na usalama wa kufanyia kazi ofisini, inabaki kuwa ni jukumu lako kuhakikisha unatunza afya yako vizuri ukiwa kazini. Vifuatavyo ni vidokezo vyetu muhimu kuhakikisha unaendelea kuwa salama kadiri iwezekanavyo.
Tengeneza sehemu ya kazi yenye kusaidia afya yako na utendaji wako
Unaweza kushawishika kufanya kazi ukiwa kitandani au kwenye sofa. Lakini kutumia masaa mengi ya kazi ukiwa umejikunja sehemu kunaweza kuathiri afya yako ya akili na mwili.5 Badala yake, wekeza katika upatikanaji wa mwanga wa kutosha. Pia nunua meza na kiti sahihi kwa ukaaji na usimamaji wako mzuri wakati ukifanya kazi ili uwe na sehemu ya kufanyia kazi iliyo salama kwa afya yako.
Pumzika mara kwa mara
Unapokuwa hauna usumbufu kutoka kwa wafanyakazi wenzako kama ilivyo kawaida katika mazingira mengi ya kiofisi, ni rahisi masaa kupita ukiwa unazingatia majukumu yako ya kazi. Lakini lazima ukumbuke kupumzika mara kwa mara ili kusogeza mwili wako na kupumzisha macho yako. Ili kufanikisha hilo, kwanini usijaribu mbinu iitwayo “Pomodoro”? Mbinu ya Pomodoro inaweza kutumika kwa kufuata hatua zifuatazo:
- Zingatia jukumu 1 la kazi kwa dakika 25.
- Chukua dakika 5 za mapumziko. Hiyo tayari ni Pomodoro 1.
- Baada ya Pomodoro 4, jitunze kwa dakika 30 za mapumziko.
Kuwa mbunifu katika kutumia muda wako wa mapumziko: jinyooshe, tembea, au taamali (meditate) - fanya chochote ndani ya muda huo isipokuwa kazi.
Tenga muda wa mazoezi
Utafiti unaonyesha wafanyakazi wa ofisini hutumia 81.8% ya muda wao wa kazi wakiwa wamekaa.6 Bila kuwa na ulazima wa kusafiri kutoka nyumbani kwenda kazini na kutembea kutoka chumba kimoja cha mkutano kwenda kingine, ni muhimu zaidi unapofanyia kazi nyumbani ukafanya jitihada zaidi kushughulisha mwili wako katika siku. Kwa maana hiyo, kusudia kupata dakika 30 za mazoezi ya mwili ya wastani kwa siku.
Endeleza mshikamano na wafanyakazi wenzako
Mahusiano ya kijamii ni moja ya faida ya kazi za ofisini. Mazungumzo ya mara kwa mara na mahusiano ya kijamii na wafanyakazi wenzako vinahitajika kwa ajili ya afya yako ya akili na mwili.7 Vifuatavyo ni vidokezo vyetu muhimu vya kuendeleza mshikamano na wafanyakazi wenzako wakati unafanyia kazi nyumbani.
Ongeza kiwango cha mawasiliano
Kufanyia kazi maeneo ya mbali na ofisini kunaweza kuleta hisia za kutengwa miongoni mwa washirika wa timu ya kazi. Lakini wakati hamko pamoja, mawasiliano mazuri ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hakikisha unawasiliana mara kwa mara na meneja wako na timu yako. Endeleeni kujulishana kuhusu utekelezaji wa majukumu yenu ya kazi ili muweze kusaidiana kikamilifu.
Pendelea zaidi kutumia video
Mawasiliano ni zaidi ya maneno unayotumia.8 Matumizi ya mawasiliano kupitia video yanaonyesha pia mkao, ishara ya uso, ishara za mikono, na toni ya sauti. Kwahiyo inapowezekana, pendelea zaidi kutumia simu za video kuwasiliana na wafanyakazi wenzako.
Ni sawa kusema hapana
Hata hivyo, simu za video za mara kwa mara zinaweza hatimaye kukuchosha kihisia na kimwili.9 Kwahiyo ukiona imetosha, usisite kuzima kamera.
Kwa kufanya mabadiliko kadhaa, ni rahisi kutunza afya yako wakati ukifanyia kazi nyumbani.
Emma Harrington and Natalia Emanuel. Working Paper. “'Working' Remotely? Selection, Treatment, and Market Provision of Remote Work (JMP)”. Kimetumika: Machi 2021.
Heintzelman, S.J. & King L. A. SPSP, (2018), doi: 10.1177/0146167218795133
Watson, N. F., et al. JCSM, (2015), doi: 10.5665/sleep.4716.
Adam, H., & Galinsky A., D. JESP, (2012), doi: 10.1016/j.jesp.2012.02.008
BBC. “What happens when you work from bed for a year” Kimetumika Machi 2020.
Parry, S. & Straker L. BMC Public Health, (2013), doi: 10.1186/1471-2458-13-296.
Sirven, N. & Debrand, T. Soc Sci Med, (2008), doi: 10.1016/j.socscimed.2008.09.056.
Park, S. G., and Park, K. H. Korean J Med Educ. (2018), doi: 10.3946/kjme.2018.94.
Harvard Business Review. “How to combat Zoom fatigue” Kimetumika Machi 2020.