Homa ya nyani: kile tunachofahamu
Huenda umeshasikia kwamba ugonjwa unaoitwa kwa Kiingereza "Monkeypox" au kwa Kiswahili "homa ya nyani" au "ndui ya nyani," unasambaa katika maeneo kadhaaa duniani, ambayo kwa kawaida huwa hayaathiriki na ugonjwa huu.
Kama ilivyo kwa watu wengi wanaosikia habari hizi, huenda ukawa pia na maswali. Leo tupo hapa kuyajibu kwa ajili yako.
Hivyo basi, ikiwa unataka kuelewa kinachoendelea kuhusu homa ya nyani, hii ni makala yako.
Nini kinachoendelea
Mamlaka za masuala ya afya zinachukua tahadhari kwasababu wanasayansi wamegundua matukio ya homa ya nyani katika maeneo ya Ulaya, mabara ya Amerika, na Australia Mamlaka zina wasiwasi kwasababu homa ya nyani ni nadra kutokeo nje ya nchi za Afrika ya Kati na Magharibi
Kufikia tarehe 23 Julai 2022, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa sasa wa homa ya nyani kuwa ni Dharura ya Afya ya Umma Duniani
Wakati tukiandika makala hii, visa 32,000 vilikuwa vimetambuliwa katika nchi ambazo kwa kawaida homa ya nyani haienei, na angalau watu 4 wamekufa kutokana na mlipuko wa ugonjwa huu
Visa vingi vinavyohusishwa na mlipuko wa ugonjwa huu vimetokea kwa wanaume wanaoshiriki tendo la kujamiiana na wanaume wenzao
Homa ya nyani ni nini?
Homa ya nyani ni kirusi ambacho wanasayansi walikibaini kwa nyani kwa mara ya kwanza mwaka 1958, na jina hili la "Monkeypox" ndiyo lilitokana na ugunduzi huo Kirusi hiki kilibainika kwa binadamu kwa mara ya kwanza mwaka 1970 Ugonjwa wa homa ya nyani unatoka kwenye familia moja ya kirusi kinachofanana na kama kile cha ugonjwa wa ndui (smallpox), lakini hakisababishi ugonjwa hatari sana kama ilivyo kile kinachosababisha ugonjwa wa ndui
Wakati tukiandika makala hii, WHO iko katika mchakato wa kufafanua majina mapya ya kirusi cha homa ya nyani na aina zake
Kuna aina 2 za homa ya nyani: clade I (zamani ilifahamika kama aina ya Bonde la Kongo) na clade II (zamani ilifahamika kama aina ya Afrika Magharibi)
Uchunguzi wa kipimo cha PCR unaonyesha kuwa mlipuko wa sasa umesababishwa na clade II, ambayo huwa na dalili zisizo kali zaidi kuliko clade I
Dalili za homa ya nyani ni zipi?
Kwa watu walio wengi, homa ya nyani sio ugonjwa wenye kuhatarisha maisha. Lakini unaweza kusababisha dalili kali, kuvuruga maisha ya kila siku, na unaweza kuhusishwa na unyanyapaa wa kijamii
Homa ya nyani kwa kawaida husababisha homa na vipele venye muonekano usio wa kawaida, lakini dalili nyingine ni pamoja na
- Maumivu ya kichwa
- Maumivu ya mgongo
- Maumivu ya misuli
- Kuvimba kwa tezi za limfu
Vipele vya homa ya nyani kwa kawaida hujitokeza usoni, mikononi, na miguuni, ingawa vinaweza pia kuathiri sehemu nyingine za mwili Hatimaye vipele hugeuka vigaga na kwisha
Wanawake wajawazito, watoto, na watu wenye kingamwili dhaifu wanaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata dalili kali za ugonjwa huu
Je, kuna matibabu ya homa ya nyani?
Kuna chanjo ya ugonjwa wa ndui, ambayo inaweza kuwa na ufanisi wa hadi 85% katika kuzuia homa ya nyani Pia kuna dawa za kuzuia virusi ambazo zinaweza kuwa na mafanikio dhidi ya ugonjwa wa homa ya nyani
Hata hivyo, kwa watu wengi waliopata maambukizi hawahitaji matibabu kwani ugonjwa huisha wenyewe ndani ya wiki mbili
Homa ya nyani husambaaje?
Maambukizi ya homa ya nyani yanaweza kutokea kutokana na kugusana na wanyama au watu walioathirika Virusi husambaa kupitia mgusano wa ngozi kw angozi (pamoja na mgusano wakati wa kujamiiana), mgusano wa majimaji ya mwili, na matone anayotoa mtu wakati wa kupiga chafya, kukohoa, au hata kuzungumza
Ingawa mlipuko wa sasa unaathiri zaidi wanaume wanaoshiriki tendo la kujamiiana na wanaume wenzao, ugonjwa wa homa ya nyani hautambuliki kama ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya kujamiiana (STD)
Kwanini homa ya nyani inasambaa sasa?
Kuongezeka kwa idadi ya visa vya homa ya nyani kunaweza kuwa kunatokana na kuishia kwa chanjo za ugonjwa wa ndui duniani kote zilizotumika katika miaka ya 1980 Hii ina maana watu wengi wenye umri wa chini ya miaka 45 wana kinga duni dhidi ya homa ya nyani na virusi vingine vinavyofanana na hivyo.
Je, nahitaji kuwa na wasiwasi kuhusu homa ya nyani?
Mamlaka za masuala ya afya zinachukua tahadhari kwasababu hii ni hali isiyo ya kawaida. Lakini wanasayansi wengi wanakubaliana kuwa mlipuko huu hautasababisha janga kama la COVID-19.
Jambo la kwanza, homa ya nyani siyo kirusi kipya. Tayari tuna chanjo na matibabu ambayo yana ufanisi dhidi ya ugonjwa huu. Pia, homa ya nyani husambaa polepole zaidi kuliko COVID-19, na dalili ya vipele venye muonekano tofauti ina maanisha ni rahisi kujua ikiwa umeathirika na unahitaji kujitenga na watu wengine.
Kwa kadiri visa vya maambukizi zinavyoongezeka, jitihada za kukabiliana na ugonjwa huu zitahitajika. Lakini hiyo haimaanishi kuwa kuna sababu yoyote ya kuwa na hofu.
Nawezaje kujikinga dhidi ya homa ya nyani?
Mtu yoyote anaweza kuambukizwa ugonjwa wa homa ya nyani na kuambukiza wengine. Njia bora zaidi ya kujikinga binafsi na kuwakinga wengine ni kufanya yafuatayo
- Kukaa nyumbani na kuwasiliana na daktari ikiwa unaonyesha dalili
- Kuepuka kugusana ngozi kwa ngozi na mtu yoyote ambaye ana dalili
- Kuvaa barakoa ikiwa unaongea kwa karibu na mtu aliye na dalili
- Kuosha mikono yako mara kwa mara
- Kusafisha vitu na sehemu zake ambazo huguswa mara kwa mara
- Ikiwa wewe ni mwanaume anayeshiriki tendo la kujamiiana na wanaume wengine, epuka kushiriki tendo husika na wapenzi wapya mpaka pale mlipuko wa ugonjwa huu utakapodhibitiwa.