Dalili za UTI
Imeandikwa na Timu ya Ada ya Maarifa ya Kitiba
Imesasishwa tarehe
Maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI) ni nini?
Kabla ya kujadili dalili za UTI, kwanza tuelewe UTI ina maanisha nini. Maambukizi ya mfumo wa mkojo, ambayo mara nyingi hufahamikama kama “UTI” au maambukizi ya mkojo, kwa kawaida husababishwa na bakteria kutoka eneo la njia ya haja kubwa au sehemu za siri na kuenea kwenye kibofu. 1 Ikiwa maambukizi hayatotibiwa, yanaweza kuendelea kuenea, na hatimaye kufikia figo kama kiungo muhimu cha mwili kilichopo katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo (upper urinary tract).
Maambukizi ya UTI kwa kawaida huwapata zaidi wanawake, ingawa wanaume wanaweza pia kupata. Dalili za UTI zinaweza kujumuisha maumivu wakati wa kukojoa na kukojoa mara kwa mara, mkojo wenye harufu isiyo ya kawaida, mkojo uliochanganyika na damu, na maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo. Dalili ya homa, kichefuchefu, na maumivu katika sehemu ya juu ya tumbo inaweza kuwa ni ishara kwamba maambukizi husika yamefikia sehemu za juu za mfumo wa mkojo. Sehemu hizi hujumuisha figo pamoja na ureta, yaani mirija inayosafirisha mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili.
Kwa matibabu ya mapema ya antibiotiki, watu wengi hupona haraka. Hata hivyo, ikiwa UTI haitibiwi, hali ya maambukizi inaweza kufikia hatua mbaya na kusababisha matatizo kadhaa kiafya. 2
Aina za maambukizi ya mfumo wa mkojo
Maambukizi ya mfumo wa mkojo huweza kutokea sehemu yoyote ndani ya mfumo wa mkojo, ambayo ni pamoja na: 3
- Mrija wa mkojo (urethra), ambao hutoa mkojo nje ya mwili kutoka kwenye kibofu. Maambukizi ya mrija huu pia hufahamika kama urethritis
- Kibofu, ambacho ni kiungo kinachokusanya na kuhifadhi mkojo mwilini. Maambukizi ya kibofu pia hufahamika kama cystitis
- Ureta, ambayo ni mirija inayosafirisha mkojo kutoka kwenye figo hadi kwenye kibofu
- Figo, ambavyo ni viungo vinavyochuja uchafu kwenye damu na kuutoa mwilini kama mkojo. Maambukizi ya figo moja au zote mbili huitwa pyelonephritis
Matukio mengi ya maambukizi ya UTI huathiri kibofu na/ au mrija wa mkojo. Maambukizi haya hufahamika kama maambukizi ya mfumo wa mkojo katika sehemu ya chini (lower urinary tract). Hata hivyo, maambukizi yanaweza kusambaa kwa njia ya mirija ya mkojo na kufika juu kwenye figo. Katika matukio nadra, mirija ya njia ya mkojo huweza kupatwa na maambukizi. Hali hiyo ikitokea, hufahamika kama maambukizi ya mfumo wa mkojo katika sehemu ya juu (upper urinary tract). Maambukizi haya ya mfumo wa mkojo katika sehemu ya juu hutokea mara chache zaidi ya yale ya sehemu ya chini na huwa na dalili za UTI kali zaidi pamoja na athari mbaya zaidi. 2
Dalili za UTI
Dalili za maambukizi ya mfumo wa mkojo mara nyingi hutofautiana kati ya mtu na mtu. Mambo kama vile umri, jinsia, na aina ya UTI yanaweza kuchangia kwa usahihi dalili zinazojitokeza na kiwango cha ukali wa dalili hizo. 4 Hata hivyo, kuna baadhi ya dalili za kuzingatia ambazo kwa kawaida hujitokeza kama ishara ya maambukizi ya UTI.
Dalili za maambukizi katika sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo
Dalili za kawaida za maambukizi katika sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo ni pamoja na: 1 3 4 5
- Haja ya kukojoa ya ghafla na ya mara kwa mara
- Maumivu wakati wa kukojoa
- Kukojoa mkojo wenye harufu kali
- Mkojo uliochanganyika na damu na/ au wenye rangi ya mavunde
- Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo
Ni vyema kufahamu: Maambukizi katika sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo huwa na dalili zinazofanana kwa wanaume na wanawake. Hata hivyo, wanaume wanaweza pia kuhisi maumivu kwenye rektamu (sehemu ya mwisho ya utumbo mpana), wakati wanawake wanaweza kuhisi maumivu kwenye fupanyonga (pelvic). 6
Dalili za maambukizi katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo
Pamoja na dalili zilizotajwa hapo juu, uwepo wa dalili zifuatazo kunaweza kuashiria kwamba muathirika ana maambukizi katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo: 1 3 4 5
- Homa
- Kuhisi baridi
- Kichefuchefu na kutapika
- Maumivu na/ au kati ya fumbatio la juu na mgongo, ambayo hufahamika kama maumivu ya ubavuni (flank pain)
- Dalili za kuchanganyikiwa, kupoteza mwelekeo na/ au wasiwasi huweza kujitokeza, hasa kwa wagonjwa wenye umri mkubwa au wazee
Ni vyema kufahamu: Dalili za maambukizi katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo ni sawa kwa wanaume na wanawake. Ikiwa unakabiliwa na uwezekano wa dalili za UTI, kagua afya yako bure kwa app yetu ya afya.
Dalili za UTI kwa wazee
Watu wengi wanaopata maambukizi ya UTI huonyesha dalili kama zile zilizoorodheshwa hapo juu. Hata hivyo, watu wenye umri mkubwa wana uwezekano mdogo wa kuonyesha dalili ambazo kwa kawaida hujitokeza hasa kwenye maeneo ya viungo vya uzazi na mkojo. Hali hii inaweza kuwa inasababishwa na mabadiliko katika utendaji wa kinga mwilini kwa kadiri umri unavyoongezeka na uwezekano wa magonjwa ya ziada na matatizo ya kiafya yanayoathiri utendaji wa kawaida wa mwili. 7
Aidha, UTI inaweza kusababisha mabadiliko fulani ya kitabia kwa wazee, kama vile kuchanganyikiwa, wasiwasi au fadhaa au kupoteza mwelekeo (kutotambua walipo au waendako). Dalili hizo mara nyingi hufahamika kama delirium, yaani mapayo au weweseko. Watu wenye matatizo ya kiafya yanayohusiana na umri kama vile kupatwa na weweseko au dimenshia (ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu) wako katika hatari ya kupata dalili za UTI kali zaidi kwasababu huenda ikawawia vigumu kutoa taarifa kuhusu dalili zao na kutibiwa haraka. 8
Ingawa uhusiano huu kati ya UTI na hali ya weweseko kutokea umethibitishwa kiutafiti, bado haijulikani hasa kwanini weweseko huweza kutokea kwa wazee wenye maambukizi ya UTI. 9
Ni vyema kufahamu: Ikiwa mtu mzee anadhaniwa kuwa na maambukizi ya UTI, wasiliana na daktari haraka, kwani kipimo rahisi cha kuchunguza mkojo kwa kawaida hutosha kuthibitisha maambukizi.
Visababishi vya maambukizi ya UTI
Maambukizi ya mfumo wa mkojo karibia mara zote husababishwa na maambukizi ya bakteria. Maambukizi haya mara nyingi hutokea wakati bakteria atokaye eneo la haja kubwa au sehemu ya siri huingia kwenye njia ya mkojo na kupanda kupitia mrija wa mkojo hadi kwenye kibofu na/au figo. Inaaminika kuwa zaidi ya asilimia 85 ya UTI husababishwa na bakteria kutoka kwenye utumbo au ukeni. 10
Asilimia 80 ya UTI inaripotiwa kusababishwa na bakteria aina ya E. coli ambao wapo kwenye utumbo wa binadamu na wanyama. 1 Ya aina nyingi za E. coli ni sehemu ya usagaji chakula wenye afya wa binadamu. Hata hivyo, aina nyingine za bakteria huyu zinaweza kusababisha ugonjwa zinapotolewa nje ya njia ya utumbo.11
Kwa kawaida, bakteria yoyote inayoingia kwenye njia ya mkojo hutolewa nje na mkojo. Katika baadhi ya matukio, kiasi kidogo cha bakteria hubakia katika mfumo, na hii inaweza kusababisha maambukizi ya mfumo wa mkojo. Inawezekana pia kupata UTI wakati maambukizi ya bakteria kutoka mahali pengine mwilini kuenea kwa njia ya damu, na kufikia figo. 10 Hata hivyo, hali hii sio kawaida sana kutokea.
Katika matukio machache, maambukizi ya mfumo wa mkojo yanaweza pia kusababishwa na virusi, fangasi, na vimelea. 10
Vihatarishi vya maambukizi ya UTI
Maambukizi ya mfumo wa mkojo ni hali ya kawaida sana kutokea, hasa kwa wanawake, na huchangia kati ya asilimia 1 hadi 3 ya watu wanaofika hospitali kutafuta ushauri wa daktari. 2 Maambukizi ya UTI yanashika nafasi ya pili katika magonjwa ya kuambukiza yanayoathiri zaidi ya watu milioni 150 kila mwaka duniani. 12
Jinsia ni kihatarishi kikuu cha maambukizi ya mfumo wa mkojo. Maambukizi ya UTI kwa kawaida hutokea zaidi kwa wanawake kuliko wanaume, na inaaminika kuwa takriban nusu ya wanawake wote, kwa mfano 5 kati ya 10 watapata maambukizi kipindi fulani maishani. 2 Hata hivyo, chini ya umri wa miaka 50, ni wanaume wa 5 hadi 8 tu kati ya kila 10,000 hupatwa na UTI.3
Ingawa kuna idadi ya vihatarishi maalum kwa wanawake au wanaume, vihatarishi vingi havitegemei jinsia, na miongoni mwao ni hivi vifuatavyo: 1 5 10 13
- Maambukizi ya bakteria kwa njia ya mrija wa mkojo (urethra).Maambukizi ya UTI husababishwa mara nyingi na bakteria wanaoingia kwenye mrija wa mkojo na kusogea hadi kwenye kibofu cha mkojo. Hii inaweza kutokea wakati wa kujamiiana, au kutokana na usafi duni wa mwili.
- Tendo la kujamiiana. Tendo la kujamiiana linaweza kuongeza hatari ya kupata UTI. Kwa mfano, kujamiiana bila kinga (kondomu) kunaweza kuongeza hatari ya kuambukizwa bakteria au vijidudu vinavyosababisha UTI kutoka kwa mwenza wako. Pia, kujamiiana kwa njia ya mdomo au njia ya haja kubwa na kutumia vifaa vya ziada (kama midoli) huweza kuhamisha bakteria kutoka maeneo mengine hadi kwenye mrija wa mkojo, hasa ikiwa usafi hauzingatiwi ipasavyo.
- Afya ya uzazi au mambo yanayohusiana na ujauzito. Wanawake wajawazito wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata UTI kutokana na mabadiliko ya homoni na anatomia. Pia, mabadiliko katika mfumo wa mkojo wakati wa ujauzito yanaweza kuongeza hatari ya maambukizi.
- Umri. Uwezekano wa kupata maambukizi ya UTI huongezeka kwa kadiri umri unavyosogea. Umri unapokuwa zaidi ya miaka 50, matukio ya UTI huonekana kuongezeka kwa jinsia zote mbili, na kunakuwa na tofauti ndogo ya idadi za maambukizi kati ya wanaume na wanawake. Wanaume wazee (kama vile wenye umri wa miaka 70 na zaidi) wako katika hatari kubwa ya kupata UTI kwa sababu ya changamoto ya kwenda chooni au kupata haja ndogo kwa ukamilifu. Pia, wanawake wenye umri mkubwa baada ya kukoma hedhi wako katika hatari kubwa ya kupata UTI kutokana na kiwango kidogo cha estrojeni ya uke, ambayo inaweza kubadilisha hali ya uke.
- Mipira ya kupitisha mkojo (urinary catheters) huweza kusababisha bakteria kuingia kwenye njia ya mkojo.
- Kuziba kwa njia ya mkojo na hali zinazoweza kuharibu mtiririko wa mkojo, kama vile uwepo wa vijiwe kwenye figo, kufunga choo kwa muda mrefu (chronic constipation) au utendaj/ muundo wa mfumo wa mkojo usio wa kawaida.
- Kisukari, hasa ugonjwa wa kisukari aina ya 2, kutokana na viwango vya juu vya sukari kwenye mkojo kuongeza hatari ya maambukizi.
- Usafi duni wa mwili unaweza kuongeza uwepo wa bakteria kwenye eneo la mkojo.
- Kupunguza kutembea kunaweza kupunguza vipindi vya kuhitaji kukojoa, na hivyo kusababisha hatari zaidi ya maambukizi.
- Kudhoofika kwa mfumo wa kinga mwilini hupunguza uwezo wa mwili kujikinga na maradhi.
- Historia ya maambukizi ya UTI katika familia. Tafiti kadhaa zimehusisha historia ya maambukizi ya UTI kwa watu binafsi na katika familia kwa kubaini ongezeko la maambukizi makali ya kibofu (acute cystitis). Katika utafiti mmoja, 42% ya wanafamilia walikuwa na kawaida ya kupatwa na maambukizi ya kibofu, ikilinganishwa na 11% ya kundi lisilo na historia ya maambukizi ya UTI katika familia.
Mbali na vihatarishi tajwa hapo juu, matumizi ya dawa kwa muda mrefu au mara kwa mara, kama vile dawa za antibiotiki, yanaweza pia kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo.
Vihatarishi vya UTI kwa mwanamke
Wanawake huathirika zaidi na maambukizi ya mfumo wa mkojo kwasababu mrija wao wa mkojo ni mfupi. Hii inamaanisha kwamba maambukizi yanaweza kuenea katika mfumo wa mkojo kwa urahisi zaidi. Aidha, matundu ya njia ya haja kubwa na ya mkojo ya mwanamke yamekaribiana zaidi, na hivyo kuongeza hatari ya bakteria kuenea kati ya hizo sehemu mbili. 1
Zaidi ya sababu hizo tajwa hapo juu, wanawake pia huathirika na vihatarishi vya UTI vifuatavyo: 15 16 17 18
- Kujamiiana kunaweza kuchangia kuenea kwa bakteria wa sehemu za siri au wa njia ya haja kubwa, hasa kwa kushiriki tendo la kujamiiana na mtu mpya wakati kiwango cha tendo husika kwa kawaida huwa juu. Hata hivyo, UTI siyo ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya kujamiiana (STD).
- Dawa za viua-shahawa (spermicides) na mbinu zinazohusiana na uzazi wa mpango zinaweza kuharibu uwiano wa asili wa bakteria wenye manufaa ukeni.
- Matumizi ya dawa za antibiotiki yanaweza pia kubadilisha uwiano wa asili wa bakteria ukeni.
- Matumizi ya diaframu (njia ya uzazi wa mpango) inaweza kuweka shinikizo kwenye mrija wa mkojo wa mwanamke, na hivyo kusababisha uwezekano wa mkojo kutotoka ipasavyo kwenye kibofu.
- Ujauzito. Wakati tumbo la uzazi (uterus) likiendelea kukua, hali hiyo inaweza kuongeza uzito kwenye kibofu, na hivyo kusababisha uwezekano wa kibofu cha mkojo kushindwa kutoa mkojo vizuri.
- Kukoma hedhi kunaweza kusababisha mabadiliko ya homoni ambayo huathiri uwiano wa asili wa bakteria ukeni.
Vihatarishi vya UTI kwa mwanaume
Ingawa maambukizi ya mfumo wa mkojo si kawaida sana kutokea kwa wanaume ukilinganisha na wanawake, kuna vihatarishi kadhaa ambavyo ni vya kipekee kwa wanaume, kama vile 1 10 19 20
- Tezi-kibofu iliyotanuka au athirika, ambayo inaweza kuzuia kibofu cha mkojo kutoa mkojo vizuri.
- Wanaume ambao hawajatahiriwa wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya UTI kuliko wanaume waliotahiriwa.
- Kujamiiana kinyume na maumbile (anal sex). Inakubalika kuwa tendo la kujamiiana huongeza hatari ya maambukizi ya UTI kwa wanawake, lakini hatari hii ni ndogo kwa wanaume wanaoshiriki tendo hilo. Hata hivyo, ikiwa mwanaume anashiriki tendo la kujamiiana kinyume na maumbile, huwa kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa UTI.
Utambuzi wa maambukizi ya mfumo wa mkojo
Utambuzi wa maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida huanza kwa daktari kuuliza maswali kulingana na dalili na uchunguzi wa kimwili. Ni kawaida kwa daktari pia kuuliza kuhusu historia ya ushiriki wa tendo la kujamiiana, historia ya matibabu, na iwapo mhusika amewahi kupata maambukizi ya UTI. 21
Sampuli ya mkojo inaweza kuchukuliwa kwa vipimo ili kuthibitisha utambuzi wa maambukizi ya mfumo wa mkojo. Uchunguzi kwa kikaratasi maalum kinachochovywa kwenye sampuli ya mkojo (dipstick analysis) huweza kufanyika kwanza ili kubaini uwepo wa bakteria kwenye mkojo. Uchunguzi huo hutazama iwapo kuna mabadiliko fulani ya rangi kwenye kikaratasi husika ambayo yanaweza kuashiria viwango visivyo vya kawaida vya damu, sukari, au bakteria kwenye mkojo. Uchunguzi wa sampuli ya mkojo kwa hadubini kwa kawaida huweza kuthibitisha utambuzi, pamoja na aina ya bakteria aliyesababisha maambukizi. 1
Ikiwa maambukizi katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo yanashukiwa, daktari anaweza pia kupendekeza vipimo vya damu ili kuthibitisha kuwa maambukizi hayajaenea kwenye damu 22
Watu wanaopata maambukizi ya UTI ya mara kwa mara au sugu wanaweza kufanyiwa vipimo vya ziada ili kubaini ikiwa kuna tatizo au kasoro zozote zinazosababisha hali hiyo kujirudia. Vipimo hivyo huweza kujumuisha: 1 23
- Uchunguzi wa kibofu na figo kwa kipimo cha ultrasound, ambacho hutumia mawimbi ya sauti yasiyo na maumivu kutoa picha ya mfumo wa mkojo
- Uchunguzi wa CT au MRI kwa uchanganuzi wa kina zaidi wa mfumo wa mkojo
- Kipimo cha cystoscopy, ambacho kamera ndogo huingizwa kwenye mrija wa mkojo kwa uchunguzi wa mrija husika na kibofu
Ikiwa una hofu kuwa wewe binafsi au mtu unayemfahamu anaweza kuwa anakabiliwa na maambukizi ya UTI, tumia app yetu ya afya ili kutathmini dalili bila malipo. Au tambua jinsi kikagua dalili chetu kinavyofanya kazi.
Wakati wa kumuona daktari kwa maambukizi ya mfumo wa mkojo
Maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida huhitaji kumuona daktari ili kuthibitisha utambuzi na kupata matibabu. Wakati wote inashauriwa kumuona daktari ikiwa vikundi vya watu wafuatao vinashukiwa kuwa na maambukizi ya UTI: 2 9 24 25
- Watoto
- Wazee
- Wanaume
- Wanawake wajawazito
- Mtu yeyote ambaye hajawahi kupatwa na maambukizi ya UTI
- Mtu yeyote anayetoa mkojo uliochanganyika na damu
- Mtu yeyote mwenye dalili za maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo
- Mtu yeyote ambaye dalili zake zimejitokeza tena baada ya matibabu
Baadhi ya watu wanaopatwa na UTI mara kwa mara wanaweza kupewa na daktari wao namna tofauti za kudhibiti maambukizi, kama vile antibiotiki za muda mrefu na za kipimo cha chini (low-dose antibiotics). 26 Katika matukio haya maalum, dalili za mwanzo za maambukizi ya UTI, zinaweza kudhibitiwa nyumbani, na kumuona daktari sio lazima kila wakati.
Katika matukio ya UTI yasiyo makali, uvimbe wa kibofu (cystitis) huweza kupona wenyewe bila kuhitaji matibabu. Hata hivyo, magonjwa mengine kama vile malengelenge ya sehemu za siri au uvimbe ukeni (vaginal thrush) huweza kudhaniwa kimakosa kuwa ni uvimbe wa kibofu. Hivyo, watu wasio na uhakika ikiwa wana uvimbe wa kibofu wanapaswa kumuona daktari. 27
Wakati wa kumuona daktari kwa maambukizi ya mfumo wa mkojo
Maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida huhitaji kumuona daktari ili kuthibitisha utambuzi na kupata matibabu. Wakati wote inashauriwa kumuona daktari ikiwa vikundi vya watu wafuatao vinashukiwa kuwa na maambukizi ya UTI: 2 9 24 25
- Watoto
- Wazee
- Wanaume
- Wanawake wajawazito
- Mtu yeyote ambaye hajawahi kupatwa na maambukizi ya UTI
- Mtu yeyote anayetoa mkojo uliochanganyika na damu
- Mtu yeyote mwenye dalili za maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo
- Mtu yeyote ambaye dalili zake zimejitokeza tena baada ya matibabu
Baadhi ya watu wanaopatwa na UTI mara kwa mara wanaweza kupewa na daktari wao namna tofauti za kudhibiti maambukizi, kama vile antibiotiki za muda mrefu na za kipimo cha chini (low-dose antibiotics). 26 Katika matukio haya maalum, dalili za mwanzo za maambukizi ya UTI, zinaweza kudhibitiwa nyumbani, na kumuona daktari sio lazima kila wakati.
Katika matukio ya UTI yasiyo makali, uvimbe wa kibofu (cystitis) huweza kupona wenyewe bila kuhitaji matibabu. Hata hivyo, magonjwa mengine kama vile malengelenge ya sehemu za siri au uvimbe ukeni (vaginal thrush) huweza kudhaniwa kimakosa kuwa ni uvimbe wa kibofu. Hivyo, watu wasio na uhakika ikiwa wana uvimbe wa kibofu wanapaswa kumuona daktari. 27
Matibabu ya maambukizi ya mfumo wa mkojo
Kwa matibabu ya haraka, watu wengi walio na maambukizi ya mfumo wa mkojo hupona kabisa. Kwa kawaida, dawa huitajika ili kupambana na maambukizi. Pia kuna tiba kadhaa zinazoweza kutumika nyumbani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza athari za maambukizi.
Dawa za maambukizi ya mfumo wa mkojo
Kwa kuwa maambukizi ya mfumo wa mkojo mara nyingi husababishwa na bakteria, yanaweza kutibiwa kwa antibiotiki. Kwa mwongozo, matibabu ya antibiotiki kwa kawaida hugawanywa katika makundi mawili. 1 28
- UTI isiyo kali, ambayo hutokea kwa mtu mwenye afya njema na utendaji wa kawaida wa figo
- UTI kali, ambayo kwa kawaida hutokea kwa watu ambao huathiriwa kwa urahisi na maambukizi ya mfumo wa mkojo au dawa kushindwa kufanya kazi
Aina ya antibiotiki inayotumika na muda wa matibabu hutofautiana kulingana na ukali wa maambukizi na historia ya matibabu ya mtu aliyeathirika. Dalili za UTI zisizo kali kwa kawaida huisha ndani ya siku 3 za matibabu ya antibiotiki, wakati watu wenye UTI kali wanaweza kuhitaji antibiotiki kwa muda wa hadi wiki mbili. 3
Bila kuzingatia sababu ya UTI, ni muhimu kumaliza dozi yote ya antibiotiki iliyopendekezwa, hata ikiwa dalili zinaonekana kuisha. Hii inaweza kusaidia kuzuia ukinzani wa antibiotiki (antibiotic resistance).
Katika matukio machache ambapo maambukizi ya mfumo wa mkojo husababishwa na virusi au fangasi, hali hii inaweza kutibiwa na dawa za kuzuia virusi au fangasi kwa utaratibu huo. 10
Tiba za nyumbani kwa maambukizi ya mfumo wa mkojo
Kwa ujumla haishauriwi kutibu maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa tiba za nyumbani tu, kwa sababu matibabu ya antibiotiki kwa kawaida huhitajika ili kuondoa maambukizi. Ni tu katika visa visivyo vikali sana vya uvimbe wa kibofu kwamba maambukizi yanaweza kwisha bila matibabu. 27 Hata hivyo, inawezekana kutumia nyumbani mbinu fulani za asili pamoja na matibabu ya antibiotiki ili kupunguza maumivu na kusaidia kumaliza maambukizi haraka. Tiba za namna hiyo zinaweza kujumuisha: 3 5 29
- Kunywa maji mengi, angalau lita 1.5 kwa siku, ili kusaidia kuondoa bakteria mwilini.
- Kuweka chupa ya maji ya moto au kitambaa kwenye tumbo au sehemu ya chini ya mgongo ili kupunguza maumivu katika maeneo hayo; hakikisha kuwa unafunga kifaa cha kutoa joto kwa kitambaa safi au taulo kabla ya kutumia ili kuepuka kuungua ngozi moja kwa moja.
- Kutumia dawa za kutuliza maumivu, kama vile paracetamol/acetaminophen au dawa zisizo za steroidal za kuzuia inflamesheni (NSAIDs) kama vile ibuprofen.
Kunywa juisi ya kranberi kumewahi kuthibitika kama njia ya matibabu yenye mafanikio katika kutibu maambukizi ya mfumo wa mkojo. Ingawa haina madhara, tafiti za hivi karibuni zinaonyesha juisi ya kranberi ina faida ndogo katika kutibu UTI. 15
Kujikinga na maambukizi ya mfumo wa mkojo
Maambukizi ya mfumo wa mkojo mara nyingi husababishwa na bakteria kuenea kutoka eneo la haja kubwa au eneo la viungo vya uzazi na kuingia kwenye mfumo wa mkojo. Hivyo basi, kuna njia kadhaa za kuzuia ambazo zinaweza kupunguza hatari ya kupata UTI: 1 3 30
- Kutumia kinga wakati wa kujamiiana au kuwa na mwenzi mmoja mnayeaminiana
- Kwenda haja ndogo baada ya kujamiiana
- Kwenda haja ndogo mara kwa mara (kukojoa)
- Kunywa maji mengi, angalau lita 1.5 kwa siku. Epuka pombe na kafeini, ambazo zinaweza kuathiri kibofu
- Kujisafisha vizuri baada ya kutumia choo ili kuepuka kueneza bakteria kutoka sehemu ya haja kubwa
- Kudumisha usafi wa mwili na eneo la viungo vya uzazi kuwa safi na kavu
- Kufuatilia dalili na kufanya vipimo mara kwa mara vya afya ya viungo vya uzazi
- Kuoga kwa maji ya mtiririko wa bomba la mvua (shower) badala ya kuoga kwenye beseni (bath)
Mbinu za kujikinga na UTI kwa wanawake
Mbali na njia za kuzuia tajwa hapo juu, wanawake wanaweza pia: 3 31 32 33
- Kuepuka njia za uzazi wa mpango ambazo zina dawa za viua-shahawa.
- Kuepuka kutumia diaframu kama njia ya uzazi wa mpango.
- Kuepuka kutumia bidhaa za kike kwenye maeneo ya viungo vya uzazi, kama vile dawa za kuondoa harufu na kuingiza maji kwa nguvu ukeni au maarufu kama “kupiga bomba” (douches), ambazo zinaweza kuathiri mrija wa mkojo.
Kujikinga UTI kwa antibiotiki
Kwa watu wanaokabiliwa na matukio ya mara kwa mara ya maambukizi ya mfumo wa mkojo, madaktari wanaweza kuchagua kupendekeza antibiotiki za muda mrefu na za kipimo cha chini. 1 Mbinu hii ya matibabu ya kuzuia inajulikana kama antibiotic prophylaxis, na inatumika ili kupunguza hatari ya maambukizi kujirudia.
Hatua za kuzuia zinaweza pia kupendekezwa kwa watu walio na mipira ya kupitisha mkojo, majeraha ya uti wa mgongo, na pia kwa wagonjwa wa kupandikiza figo (renal transplant) na wanawake wajawazito. 34
Madhara ya maambukizi ya mfumo wa mkojo
Maambukizi ya UTI ni hali ya kawaida sana, na watu wengi hupona haraka kwa matibabu ya antibiotiki. Hata hivyo, ikiwa haitatibiwa, maambukizi yanaweza kuenea katika mfumo wa mkojo, hali kuwa mbaya zaidi na kusababisha matatizo ya kiafya. 2
Katika baadhi ya matukio, maambukizi yanaweza kufika kwenye figo katika sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo, na maambukizi haya hujulikana kama pyelonephritis. Iwapo hayatotibiwa, yanaweza kusababisha madhara ya kudumu katika figo. 35 Madhara yanayoweza kutokea kutokana na UTI isiyotibiwa ni pamoja na: 36 37
- Kuota jipu ndani au karibu na figo
- Kuvimba kwa figo, pia inajulikana kama hydronephrosis
- Sepsisi, pia hujulikana kama sumu ya damu
- Prostatitis au tezi-kibofu kwa wanaume
Madhara yote haya ni makubwa na yanahitaji matibabu ya haraka.
Ujauzito na maambukizi ya mfumo wa mkojo
Wanawake wajawazito walio na UTI ambayo hukua na kusambaa kwenye figo wako katika hatari kubwa ya kupata madhara zaidi, ambayo yanaweza kuwaathiri wao na kijusi (fetus). Madhara hayo ni pamoja na upungufu wa damu, kushikwa na uchungu wa kuzaa kabla ya wakati, mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, na katika matukio machache sana, kuzaa mtoto aliyekufa. 24 26
Kwa bahati nzuri, matibabu ya mapema yanamaanisha kuwa maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa wanawake wajawazito yanaweza kutibiwa kwa mafanikio. Ikiwa mtu aliyeathirika ana maambukizi katika sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo, dozi ya vidonge vya kumeza ya antibiotiki ni njia ya kawaida ya matibabu. Ikiwa inadhaniwa kuwa maambukizi yamefikia sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo, daktari anaweza badala yake kupendekeza matibabu ya antibiotiki kwa njia ya kudunga sindano (intravenously) chini ya uangalizi maalum hospitalini. 24
Mara tu maambukizi yakiisha, daktari anaweza kuamua kupendekeza antibiotiki za kinga (prophylactic antibiotics) zenye kiwango cha chini cha dawa kwa muda uliosalia wa ujauzito ili kupunguza hatari ya maambukizi ya UTI kurudi. 24
Hali ya ujauzito inaweza kuongeza uwezekano wa kupata UTI. Hii ni kutokana na sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya homoni na tumbo la uzazi kuongezeka uzito, ambao husababisha shinikizo kwenye kibofu.
Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)
S: Nini husababisha maambukizi ya mfumo wa mkojo?
J: Maambukizi ya mfumo wa mkojo ni ya kawaida sana, hasa kwa wanawake, na mara nyingi husababishwa wakati bakteria kutoka kwenye utumbo au eneo la viungo vya uzazi huingia mwilini kupitia mrija wa mkojo. Hii inaweza kusababisha maambukizi katika mrija wa mkojo, kibofu, ureta au figo. Zaidi ya asilimia 85 ya UTI husababishwa kwa njia hii. UTI pia inaweza kusababishwa na maambukizi ya virusi, fangasi au vimelea, lakini hizi ni sababu ambazo kwa kawaida ni nadra kutokea.
S: Je, Wanaume wanaweza kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo?
J: Ndiyo, ingawa ni nadra kwa wanaume walio chini ya umri wa miaka 50. 37 Wanaume wana uwezekano mdogo wa kupata UTI kuliko wanawake kwa sababu mfumo wa mkojo wa kiume una kinga ya asili zaidi ya maambukizi, kama vile mrija wa mkojo mrefu na umbali zaidi kati ya mrija wa mkojo na sehemu ya haja kubwa. Kwa sababu hii, maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa wanaume yana uwezekano mkubwa wa kusababishwa na sababu za kiafya au kuathiriwa kwa urahisi na maambukizi ya UTI. 35
S: Je, watoto wanaweza kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo?
J: Ndiyo, maambukizi ya mfumo wa mkojo ni hali ya kawaida kwa watoto wachanga, watoto wanaoanza kutembea, na watoto kwa ujumla. Kwa hakika, ni maambukizi yanayosababishwa na bakteria ambayo kwa kawaida hutokea kwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili. 38 Kwa kawaida sababu ya UTI kwa watoto ni sawa na ile ya watu wazima: bakteria kutoka sehemu ya haja kubwa kuingia kwenye mfumo wa mkojo kupitia mrija wa mkojo. Baadhi ya watoto wanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata UTI kutokana na kutokuwa na mbinu bora za usafi wa mwili, kama vile kujifuta kwa karatasi ya chooni (toilet paper) kwa kutoka mbele kwenda nyuma baada ya kutumia choo. 39
S: Je, maambukizi ya mfumo wa mkojo yanahitaji matibabu?
J: Ndiyo, maambukizi ya njia ya mkojo kwa kawaida huhitaji dozi ya antibiotiki ili kutibu maambukizi. Ikiwa UTI imesababishwa na virusi au fangasi, dawa ya kuzuia virusi au fangasi inaweza kutumika badala yake. Kwa matibabu ya haraka, maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida huisha ndani ya siku chache. Iwapo haitatibiwa, UTI inaweza mara nyingi kuwa maambukizi makubwa zaidi na kusababisha madhara mengi kiafya, hivyo inashauriwa kumuona daktari. Matukio machache sana ya maambukizi ya kibofu/cystitis yanaweza kuisha yenyewe baada ya siku chache bila matibabu. Hata hivyo, bado inashauriwa kumuona daktari ikiwa mtu aliyeathirika ana hali nyingine yoyote ya kitiba, ni mjamzito au hana uhakika ikiwa ana maambukizi katika kibofu. Ikiwa dalili zinazidi kuwa mbaya, tafuta msaada wa matibabu.
S: Ni tiba gani za nyumbani zinafaa kwa kutibu maambukizi ya mfumo wa mkojo?
J: Maambukizi ya mfumo wa mkojo kwa kawaida huhitaji matibabu. Hata hivyo, kuna baadhi ya tiba za nyumbani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza athari na zinaweza kusaidia kutibu maambukizi haraka zaidi zinapotumiwa pamoja na matibabu rasmi. Hizi ni pamoja na:
- Kunywa maji mengi, angalau lita 1.5 kwa siku. Hii husaidia kukojoa mara kwa mara na inaweza kusaidia kuondoa bakteria mwilini
- Kuweka chupa ya maji ya moto au kitambaa kwenye tumbo au sehemu ya chini ya mgongo ili kupunguza maumivu katika maeneo hayo
- Kutumia dawa za kutuliza maumivu, kama vile paracetamol/acetaminophen au dawa zisizo za steroidal za kuzuia inflamesheni (NSAIDs) kama vile ibuprofen
S: Je, juisi ya kranberi inafaa katika kuzuia maambukizi ya mfumo wa mkojo?
J: Utafiti wa iwapo kutumia bidhaa za kranberi kunaweza kusaidia kuzuia maambukizi ya mfumo wa mkojo umekuwa na matokeo mchanganyiko. Utafiti mmoja unapendekeza kwamba mchanganyiko fulani unaopatikana katika kranberi unaweza kusaidia kuzuia bakteria wa aina ya E. koli kushikamana na kuta za mfumo wa mkojo na hivyo kupunguza hatari ya kuambukizwa.40 Hata hivyo, tafiti nyingine zimeonyesha kuwa manufaa ya juisi ya kranberi ni madogo 41 Hivyo basi, ingawa labda si hatari kutumia, bidhaa za kranberi si njia iliyothibitishwa ya matibabu ya UTI na haipaswi kuchukua nafasi ya matibabu rasmi katika hali yoyote.
S: Je, kuna hatari gani za maambukizi ya mfumo wa mkojo wakati wa ujauzito?
J: UTI inaweza kwa kawaida kutokea wakati wa ujauzito kwasababu ya mabadiliko ya homoni na kuongezeka kwa shinikizo kwenye kibofu kutokana na ukuaji wa tumbo la uzazi. Dalili ni sawa kwa wanawake wajawazito na wasio wajawazito. Hata hivyo, ikiwa haijatibiwa wakati wa ujauzito, UTI inaweza kusababisha madhara kama vile kushikwa na uchungu wa kujifungua kabla ya wakati, mtoto kuzaliwa na uzito mdogo na, katika matukio machache sana, kuzaa mtoto mfu. Matibabu ya UTI inayosababishwa na bakteria kwa kawaida hufanywa kwa antibiotiki. Kwa vile antibiotiki fulani zina madhara ambayo yanaweza kuathiri ukuaji wa kijusi, daktari atapendekeza antibiotiki tofauti ambazo ni salama kutumia wakati wa ujauzito. Kwa kupata matibabu, wanawake wengi wajawazito hupona kabisa bila kupata madhara zaidi kiafya.