1. Ada
 2. Editorial
 3. Tiba & afya
 4. Kupunguza muda wa skrini

Kupunguza muda wa skrini

Mfano wa watu wanaotazama skrini za simu zao karibu na shisha

Katika mifuko yetu, kwenye supamaketi, hata kwenye vifundo vya mikono yetu. Kama maono ya miaka ya 1960 kuhusu siku zijazo, skrini zipo kila mahali. Na hatuishi kuzitolea macho.

Hakuna namna ya kujinasua kutoka kwenye mtego wa skrini. Tunatumia muda mwingi kutazama skrini: kwa baadhi yetu, tunatazama sana zaidi ya vile tungependa kuukubali ukweli huo. Na kadiri kazi za nje ya ofisi na mijumuiko ya mtandaoni inavyozidi kuwa ni hali ya kawaida kwa wengi wetu, hata mawasiliano yetu ya ana kwa ana yanahamia kwenye skrini. Lakini je, muda wote huu wa skrini una manufaa yoyote kwetu? 

Kwa msaada wa Dk. Shubs, tuangalie jinsi gani muda wa skrini unaweza kuathiri afya yako, kiasi gani ni kingi kupita kiasi, na vidokezo kadhaa vya jinsi ya kupunguza.

Jaribu app ya Ada bure ili kutathmini dalili zinazohusiana na utazamaji wa skrini uliokithiri.

Je, skrini ni mbaya kwa afya yako?

Hakuna haja ya kuwa na hofu. Hakuna ushahidi halisi kwamba skrini huwasababishia watu wazima madhara makubwa ya moja kwa moja. Lakini kwa mujibu wa Dk. Shubs, utumiaji wa skrini wa kupita kiasi unaweza kuhusishwa na matatizo ya kiafya. Embu tuangalie baadhi ya matatizo ambayo ni ya kawaida kutokea.

Uchovu unaotokana na matumizi ya skrini

Maumivu ya kichwa na uchovu wa macho vinaweza kuhusishwa na matumizi ya kupindukia ya skrini. Hiyo inaweza kuwa inasababishwa na upepesaji wako mdogo wa macho wakati unafanya kazi kwa kutumia skrini ya kompyuta.1 Ukichanganya hili na uwepo wa muda mrefu kwenye mwanga mkali, kunaweza kusababisha uchovu, na maumivu ya macho na kichwa.

Matatizo ya kupata usingizi

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba utumiaji wa skrini wakati wa kulala unaweza kuvuruga usingizi wako. Kuwepo kwenye mwanga mkali wa skrini kabla ya kulala kunaweza kuzuia uzalishaji wa homoni ya melatonini, ambayo ni kemikali muhimu katika udhibiti wa ufanyaji kazi wa mwili wa binadamu.2 Usingizi duni unaweza hatimaye kuathiri afya yako na ustawi wako.

Maumivu

Watu huwa na kawaida ya kusahau kuhusu mkao wakati wanatumia vifaa vyao vya kielekroniki kwa muda mrefu. Lakini baada ya muda mrefu ukiwa umeinamia simu yako au kukaa ukitazama skrini ya kompyuta, unaweza kuanza kuhisi maumivu ya mgongo, shingo na bega.3

Je, kiasi gani cha utazamaji skrini ni kingi kupita kiasi?

Hakuna jibu la hakika la swali hilo. Dk. Shubs anapendekeza utumiaji wa wastani, kwa kusema “Muda wa skrini ni mada moto iliyo mezani kwa mjadala. Baadhi ya watu hutoa hoja kwamba kuna utiaji chumvi mkubwa katika suala la athari za muda wa matumizi ya skrini. Kuwe na uongezaji chumvi au hakuna, ni muhimu kukumbuka kwamba kwa kawaida wakati unatazama skrini yako, unakuwa haujichanganyi na wanajamii wenzako, haufanyi mazoezi, au haulali. Hatimaye hali hiyo inaweza kuanza kuathiri afya yako, utendaji, na ubora wa maisha. Hivyo basi, labda ni wazo zuri kwa wengi wetu kupunguza kidogo muda wetu wa matumizi ya skrini.”

Vidokezo vya kusaidia kupunguza muda wako wa matumizi ya skrini

Kuna mambo mengi unayoweza kujaribu. Lakni, hapa tutakupa mambo 5 tu yatakayokusaidia kuanza mchakato:

 1. Fuatilia ni muda gani unatumia kuangalia skrini: anza vitu muhimu kwanza. Hii ni njia bora ya kuanza kudhibiti kijanja muda wako wa matumizi ya skrini.
 2. Chukua mapumziko mafupi ya mara kwa mara. Ikiwa unafanya kazi na kompyuta, tenga dakika 5 za kukaa mbali na skrini yako kila baada ya saa 1 ili kupumzisha macho yako.
 3. Ondoa uwepo wa rangi kwenye taswira za skrini yako: kufanya skrini zako kukosa mvuto wa kuzitazama kumethibitika kusaidia kupunguza muda wa matumizi ya skrini.4
 4. Weka simu yako nje ya chumba chako cha kulala: wakati mwingine unapojiandaa kulala, soma kitabu kama mbadala wa kutumia simu yako.
 5. Futa app za mitandao ya kijamii kwenye simu yako: mitandao ya kijamii inaweza kuwa njia nzuri ya kuwasiliana na watu duniani. Lakini wote tuna hatia ya kujikuta tunaangalia ukurasa mmoja mpaka mwingine bila kufikiria. Kwanini usijaribu kuondoa kishawishi?

Skrini ni nzuri. Zinawezesha utoaji habari na mawasiliano ya watu. Lakini inawezekana kuwa na kiasi kingi mno cha kitu kizuri. Matumizi ya kupindukia ya skrini yanaweza kuathiri afya ya akili na mwili. Kwa kufanya mabadiliko machache ya tabia, unaweza kusitawisha uhusiano na skrini zako wenye manufaa kiafya.


 1. Patel, S., et al. Optom. Vis. Sci, (1991), doi: 10.1097/00006324-199111000-00010.

 2. Harvard Medical School. “Blue light has a dark side.” Kimetumika Desemba 18, 2020.

 3. Jung, SI., J Phys Ther Sci, (2016), doi: 10.1589/jpts.28.186.

 4. Holte, AJ., The Social Science Journal, (2020), doi: 10.1080/03623319.2020.1737461.

Mwandishi:

Harry O’Connor
Harry O’Connor

Harry ni Mwandishi wa Ada katika Masuala ya Kisayansi.

Mhakiki wa kitiba:

Dk. Shubhanan Upadhyay
Dk. Shubhanan Upadhyay

Dk. Upadhyay Mkurugenzi wetu wa Ubora wa Kitiba.

Mfasiri:

Rungwe Hashim
Rungwe Hashim

Rungwe ni mwandishi na msimamizi wa maudhui ya Kiswahili ya Ada.